سیدھے مواد پر جائیں
Tafsir As-Saadi - Swahili · Al-Baqara
سورت 2

Al-Baqara

یہ تفسیر السعدی کا ایک ترجمہ ہے جیسا IslamHouse.com اسے saadi.islamenc.com پر شائع کرتا ہے، اس سائٹ کے صفحات سے لیا گیا۔ سائٹ یہ نہیں بتاتی کہ اس کا ترجمہ کس نے کیا اور وہ کس چھپے ہوئے ایڈیشن کی پیروی کرتا ہے، اور اس کا متن لینے کی کوئی شرائط بیان نہیں کرتی، اس لیے اسے دکھانے کا حق تصدیق شدہ نہیں۔ کسی نے اسے چھپی ہوئی کتاب سے نہیں ملایا اور کسی عالم نے اس کا جائزہ نہیں لیا۔ ہر حصہ ان آیات کے ساتھ ہے جن پر وہ تبصرہ کرتا ہے، اور وہ آیات Tanzil کا قرآنی متن ہیں، جیسا وہاں ہے؛ جس آیت کی سائٹ اپنی الگ تفسیر نہیں دیتی وہ اپنے سے پہلے کے حصے کے ساتھ ہوتی ہے، اور فہرست ایسی ہر آیت کا نام لیتی ہے۔ سبیل نے اس میں سے کچھ نہیں لکھا اور نہ اس کا ترجمہ کیا۔

متن ماخوذ ازsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)2026-10-22 کو لیا گیا

آیت 3

ٱلَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِٱلْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ ٱلصَّلَوٰةَ وَمِمَّا رَزَقْنَـٰهُمْ يُنفِقُونَ 3

Kisha akawaeleza wachamungu kwa itikadi na vitendo vya ndani (vilivyofichika) na vitendo vya dhahiri, kwa sababu uchamungu unajumuisha hayo, akasema:

(3) “Ambao huyaamini ya ghaibu” kiuhakika. Na imani ni kusadiki kukamilifu kwa yale waliyojulisha Mitume, ambayo inajumuisha kunyenyekea kwa viungo. Na hili jambo halihusu kuamini katika mambo yanayoshuhudiwa kwa hisia. Kwa sababu, Muislamu na kafiri hawawezi kutofautishwa kwa hilo. Hakika, jambo hili linahusu kuyaamini ya ghaibu ambayo hatujawahi kuyaona wala kuyashuhudia, bali tunayaamini kwa sababu ya habari itokayo kwa Mwenyezi Mungu na habari itokayo kwa Mtume wake. Hii ndiyo imani ambayo anatofautishwa kwayo Muislamu na kafiri; kwa sababu ni kumsadiki tu Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Hivyo basi, Muumini anaamini kila alichojulisha Mwenyezi Mungu, au alichojulisha Mtume wake, sawa awe amekiona au hakukiona, na sawa alikifahamu na akakielewa, au akili yake na ufahamu wake haukuongoka kuyaelewa. Tofauti na Az-Zanaadiqa (waasi wakubwa) wanaokanusha mambo ya ghaibu, kwa sababu akili zao pungufu zenye kupuuza hazikuongoka kwayo; basi wakayakanusha wasiyoyaelewa elimu yake. Kwa hivyo, akili zao zikaharibika na fikra zao zikakorogeka. Na zikatakasika akili za Waumini wanaosadiki, walioongoka kwa uwongofu wa Mwenyezi Mungu. Na inaingia katika kuamini (mambo) ya ghaibu, kuamini yote aliyoeleza Mwenyezi Mungu ya ghaibu yaliyopita na yajayo, na hali ya Akhera, na uhakika wa sifa za Mwenyezi Mungu na jinsi zilivyo, na yale waliyosema Mitume kuhusu hayo. Kwa hivyo, wanaamini katika sifa za Mwenyezi Mungu na kuwepo kwazo, na wana yakini nazo, hata kama hawaelewi jinsi zilivyo. Kisha akasema “na hushika Swala,” na hakusema; hufanya swala, wala huleta swala, kwa sababu haitoshi katika hilo kufanya sura yake ya nje tu. Kwa maana, kushika swala, ni kuishika kwa nje kwa kukamilisha nguzo zake, wajibu wake, na masharti yake. Na kuishika kwa ndani kwa kushika roho yake, ambayo ni kuhudhuria moyo ndani yake, na kutafakari anachokisema na kutenda ndani yake. Na swala hii ndiyo aliyosema Mwenyezi Mungu kuihusu. “Hakika swala inazuilia (mambo) machafu na maovu,” na hii (swala) ndiyo ambayo ina malipo. Kwa maana hakuna malipo mazuri kwa mja katika swala yake isipokuwa kwa kile alichokielewa ndani yake. Na zinaingia katika swala, swala za faradhi na za sunnah. Kisha akasema “na hutoa katika tuliyowapa.” Inaingia ndani yake kutoa kwa lazima kama vile zaka, na kumpa matumizi mke, jamaa, watumwa na mfano wao, na pia kutoa kunakopendekezwa katika njia zote za heri. Na (Mwenyezi Mungu) hakutaja yule anayepewa (hapa) kwa sababu ya wingi wa sababu zake na aina mbali mbali za wastahiki wake, na kwa sababu kutoa kama kulivyo ni jambo la kujiweka kwalo karibu na Mwenyezi Mungu. Na alitumia neno “min (katika)” linalomaanisha baadhi (ya kitu), ili awatanabahishe kuwa yeye kwa hakika hakutaka kutoka kwao isipokuwa sehemu ndogo kutoka kwa mali zao, ambayo haina madhara kwao wala uzito wowote, bali wao wanafaidika kwa kuitoa, na pia ndugu zao wanafaidika kwayo. Na katika kauli yake “tuliyowapa.” Kuna ishara ya kwamba hizi mali ambazo zimo mikononi mwenu hazipatikani kwa nguvu zenu na uwezo wenu, bali ni riziki ya Mwenyezi Mungu ndiye aliyewapa na akawaneemesha kwacho. Na namna alivyowaneemesha na akawaboresha juu ya wengi katika waja wake, basi mshukuruni kwa kutoa baadhi ya kile alichowaneemesha kwacho, na wafarijini ndugu zenu wasiokuwa nacho (mafukara). Na Mwenyezi Mungu Mtukufu mara nyingi hukusanya kati ya swala na zaka katika Qur-ani, kwa sababu swala inajumuisha kumpwekesha mwabudiwa, nayo zaka na kutoa kwa ajili ya matumizi inajumuisha kuwafanyia ihsani (wema) waja wake. Kwa hivyo, anuani ya kufanikiwa kwa mja ni kumkusudia muabudiwa wake peke yake, na kufanya juhudi kwake katika kuwanufaisha viumbe. Kama vile anuani ya upotovu wa mja ni kutokuwa na mambo mawili haya, kwa hivyo akawa hamkusudii peke yake wala hafanyi ihsani.