Az-Zumar
Bu, as-Saʿdī’nin tefsirinin, IslamHouse.com’un saadi.islamenc.com adresinde yayımladığı hâliyle bir çevirisidir; o sitenin sayfalarından okunmuştur. Site, kimin çevirdiğini ya da hangi basılı neşri izlediğini söylemez ve metnini almak için hiçbir şart belirtmez; bu yüzden bunu gösterme hakkı doğrulanmamıştır. Kimse bunu basılı bir kitapla karşılaştırmadı ve hiçbir âlim gözden geçirmedi. Her bölüm, yorumladığı âyetlerin yanında durur; bu âyetler Tanzil’in Kur’ân metnidir, orada olduğu gibi gösterilir; sitenin kendine ait bir yorum vermediği bir âyet kendisinden önceki bölümle birlikte durur ve dizin böyle her âyeti adıyla anar. Sabīl bunun hiçbirini yazmamış ve çevirmemiştir.
Metin kaynağı:saadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)2026-10-22 tarihinde alındı
ٱللَّهُ نَزَّلَ أَحْسَنَ ٱلْحَدِيثِ كِتَـٰبًا مُّتَشَـٰبِهًا مَّثَانِىَ تَقْشَعِرُّ مِنْهُ جُلُودُ ٱلَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ ثُمَّ تَلِينُ جُلُودُهُمْ وَقُلُوبُهُمْ إِلَىٰ ذِكْرِ ٱللَّهِ ۚ ذَٰلِكَ هُدَى ٱللَّهِ يَهْدِى بِهِۦ مَن يَشَآءُ ۚ وَمَن يُضْلِلِ ٱللَّهُ فَمَا لَهُۥ مِنْ هَادٍ 23
{23} Mwenyezi Mungu Mtukufu anajulisha kuhusu Kitabu chake alichokiteremsha kwamba ni "hadithi nzuri kabisa." Kwani hadithi nzuri kabisa ni maneno ya Mwenyezi Mungu, na kitabu bora zaidi kilichoteremshwa katika maneno ya Mwenyezi Mungu ni Qur-ani hii. Na ikiwa ndiyo nzuri zaidi, basi inajulikana kuwa lafudhi zake ndizo fasaha zaidi na zilizo wazi zaidi, na kwamba maana zake ndizo maana tukufu zaidi. Kwa sababu ndiyo hadithi nzuri zaidi katika maana ya maneno yake. "Kitabu chenye kufanana" katika uzuri, kuelewana na kutotofautiana kwa namna yoyote ile, kiasi kwamba kila anapoizingatia mwenye kuzingatia na kuitafakari mwenye kutafakari, anaona namna kinavyoafikiana vyema - hata katika maana zake za ndani zaidi - jambo ambalo linawashangaza watazamaji na anakuwa na uhakika kuwa hakitoki isipokuwa kwa yule ambaye ni Mwenye hekima na ajuaye zaidi. Hii ndiyo maana ya kufanana mahali hapa. Ama katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Yeye ndiye aliyekuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake zimo Aya muhkam (zenye maana wazi). Hizo ndizo msingi wa Kitabu hiki. Na ziko nyingine za mifano," maana yake ni kwamba zinawachanganya watu wengi kuzifahamu, na kuchanganya huku hakuwezi kuondolewa isipokuwa kwa kuzirudisha kwa aya zilizo wazi. Ndiyo maana akasema: "Ndani yake zimo Aya muhkam (zenye maana wazi). Hizo ndizo msingi wa Kitabu hiki. Na ziko nyingine za mifano." Basi hapa akafanya kufanana huku ni katika baadhi yake, na hapo juu akakifanya chote ni chenye kufanana. Kwa sababu alisema: "Hadithi nzuri zaidi" ambayo ni sura na Aya. "Na kukaririwa;" yaani, vinakaririwa humo visa, hukumu mbalimbali, ahadi, vitisho, sifa za watu wema na sifa za watu waovu. Na yanakaririwa humo majina na sifa za Mwenyezi Mungu. Hili ni katika utukufu wake na uzuri wake. Kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu alipojua hitaji la viumbe juu ya maana zake zinazotakasa nyoyo, zinazokamilisha maadili, na kwamba maana hizi kwa nyoyo ni kama maji yanyweshwayo miti. Kwa sababu kila wakati miti inapokawia kunyweshwa maji, inapungua na hata labda inaweza kuharibika. Na kila mara inapomwagiliwa maji, inakuwa nzuri na inatoa kila aina ya matunda yenye faida. Basi vile vile moyo daima unahitaji kurudiliwa na maana ya maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kwamba ikiwa maana hizo zitarudiwa mara moja tu katika Qur-ani nzima, basi haitauathiri hata kidogo, na hakutakuwa na matokeo yaliyotakiwa kwayo. Ndiyo maana nikachukua njia hii adhimu katika tafsiri hii kwa kufuata mfano wa tafsiri yake. Hutapata ndani yake kuruka kutoka mahali hadi pahali pengine. Bali utapata maelezo ya kila sehemu pamoja na maana yake kamili, bila kuzingatia yale yaliyotangulia, yale yanayofanana nayo, hata kama baadhi ya maeneo yanakuwa yamerefushwa zaidi kuliko mengine na yenye manufaa zaidi. Kwa hivyo, msomaji wa Qur-ani ambaye anatafakari maana zake hafai kuacha kutafakari katika sehemu zake zote. Kwa sababu hilo linamfanya kupata heri nyingi na manufaa tele. Na kwa vile Qur-ani tukufu ina utukufu huu na ukubwa huu, iliathiri nyoyo za wenye ufahamu mkubwa walioongoka. Ndiyo maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: "husisimua kwacho ngozi za wenye kumhofu Mola wao Mlezi," kwa sababu ina vitisho na mambo ya kuhofisha yasumbuayo. "Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu," wakati yanapotajwa matumaini na mambo yanyotia moyo. Mara huwahimiza kutenda heri, na wakati mwingine huwatishia wasifanye maovu. "Hayo" aliyoyataja Mwenyezi Mungu kuhusiana na athari ya Qur-ani juu yao "ndiyo uwongofu wa Mwenyezi Mungu" kwa waja wake, na ambao ni katika fadhila zake na wema wake juu yao. "Kwa huo humwongoa amtakaye" katika waja wake. Na inawezekana kwamba kile kinachokusudiwa katika kauli yake: "hayo" ni Qur-ani tuliyowaelezea, "ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu" ambao hakuna njia nyingine inayoweza kufikisha ielekeayo kwa Mwenyezi Mungu ila kwa hiyo. "Kwa huo humwongoa amtakaye" katika waja wake miongoni mwa wale ambao nia zao ni njema. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Mwenyezi Mungu huwaongoa kwayo wenye kufuata radhi yake katika njia za salama." "Na ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza, basi hapana wa kumwongoa." Kwa sababu hakuna njia inayofikisha kwake ila kwa kuwezesha kwake na kuwezesha kurejea kwenye Kitabu chake. Kwa hivyo, kama hayo hayatotokea, basi hakuna njia iendayo kwenye uwongofu na hakutakuwa na chochote ila upotofu na mashaka yaliyo wazi.