İçeriğe geç
Tafsir As-Saadi - Swahili · Al-Baqara
Sure 2

Al-Baqara

Bu, as-Saʿdī’nin tefsirinin, IslamHouse.com’un saadi.islamenc.com adresinde yayımladığı hâliyle bir çevirisidir; o sitenin sayfalarından okunmuştur. Site, kimin çevirdiğini ya da hangi basılı neşri izlediğini söylemez ve metnini almak için hiçbir şart belirtmez; bu yüzden bunu gösterme hakkı doğrulanmamıştır. Kimse bunu basılı bir kitapla karşılaştırmadı ve hiçbir âlim gözden geçirmedi. Her bölüm, yorumladığı âyetlerin yanında durur; bu âyetler Tanzil’in Kur’ân metnidir, orada olduğu gibi gösterilir; sitenin kendine ait bir yorum vermediği bir âyet kendisinden önceki bölümle birlikte durur ve dizin böyle her âyeti adıyla anar. Sabīl bunun hiçbirini yazmamış ve çevirmemiştir.

Metin kaynağı:saadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)2026-10-22 tarihinde alındı

Ayet 143

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَـٰكُمْ أُمَّةً وَسَطًا لِّتَكُونُوا۟ شُهَدَآءَ عَلَى ٱلنَّاسِ وَيَكُونَ ٱلرَّسُولُ عَلَيْكُمْ شَهِيدًا ۗ وَمَا جَعَلْنَا ٱلْقِبْلَةَ ٱلَّتِى كُنتَ عَلَيْهَآ إِلَّا لِنَعْلَمَ مَن يَتَّبِعُ ٱلرَّسُولَ مِمَّن يَنقَلِبُ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ ۚ وَإِن كَانَتْ لَكَبِيرَةً إِلَّا عَلَى ٱلَّذِينَ هَدَى ٱللَّهُ ۗ وَمَا كَانَ ٱللَّهُ لِيُضِيعَ إِيمَـٰنَكُمْ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ بِٱلنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ 143

“Na vivyo hivyo, tumewafanya muwe Umma wa wastani.” Yani waadilifu na bora. Na kitu chochote kisichokuwa cha wastani, basi hicho ni cha kando kando, na ambacho kinaingia katika hatari. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu akaufanya Umma huu kuwa wastani katika mambo yote ya dini: Wastani katika Manabii - baina ya waliowainua juu kupindukia kiasi, kama vile Wakristo, na baina ya wale waliowadunisha, kama vile Mayahudi - kwa kuwaamini wote kwa namna inayostahiki. Na wastani katika Sheria, siyo kama kujifanyia ugumu kwa Mayahudi na mizigo yao, wala ulegevu wa Wakristo. Na katika mlango wa usafi na kula, wao siyo kama Mayahudi ambao haziwi swala zao sahihi isipokuwa wakiswalia katika masinagogi yao, na makanisa yao, na kwamba maji hayawasafishi kutokana na najisi. Nao pia wameharamishiwa vitu vizuri ili kuwaadhibu. Na pia siyo kama Wakristo ambao hawaoni unajisi wa chochote, na wala hawaharamishi chochote. Bali wameruhusu (kuwa chakula) chochote kinachotembea na kutambaa juu ya uso wa ardhi. Bali (Waislamu), usafi wao ndio usafi kamili zaidi na timilifu zaidi. Na Mwenyezi Mungu amewaruhusu vitu vizuri katika vyakula, vinywaji, mavazi na ndoa. Na akawaharimishia machafu katika hayo. Kwa hivyo, Umma huu una dini kamilifu zaidi, na maadili ya juu zaidi, na matendo bora zaidi. Na Mwenyezi Mungu aliwapa elimu, ustahimilivu, uadilifu, na wema ambao hakuwahi kuupa umma mwingineo. Ndio maana wakawa “Umma wa wastani,” wakamilifu wa kati na kati ili wawe “mashahidi juu ya watu”; kwa sababu ya uadilifu wao, na kuhukumu kwao kwa uadilifu. Nao watawahukumu watu wote miongoni mwa watu wa dini zote, na wala hawatahukumiwa wao na mwingine yule. Kwa hivyo, chochote ambacho Umma huu utashuhudia juu yake kuwa kinakubalika, basi hicho kitakubaliwa. Na chochote ambacho utashuhudia kuwa kinakatalika, basi hicho kitakataliwa. Na ikisemwa: Vipi itakubaliwa hukumu yao juu ya wengine, na hali ni kwamba kila mmoja wa wapinzani wawili haikubaliki kauli ya kila mmoja wao juu ya mwenziwe? Itasemwa: Kauli ya mmoja wa hao wapinzani wawili haikukubaliwa kwa sababu ya kuwepo kwa tuhuma. Ama iwapo tuhuma hiyo haipo, na uadilifu kamili ukapatikana, kama ilivyo katika umma huu, basi kinachokusudiwa ni kuhukumu kwa uadilifu na haki. Na sharti ya hayo ni kuwa na elimu na uadilifu. Na viwili hivyo vinapatikana katika umma huu. Basi ndiyo kauli yake ikakubaliwa. Na mwenye kushuku yeyote akishuku fadhila zake (umma huu), na akataka mwenye kuutakasa, basi ni yule mkamilifu zaidi wa viumbe, Nabii wao, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Ndiyo maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema, “na Mtume awe shahidi juu yenu.” Na miongoni mwa ushahidi wa umma huu juu ya watu wengine ni kwamba, itakapokuwa Siku ya Kiyama, na Mwenyezi Mungu akawauliza Mitume kuhusu kufikisha kwao ujumbe, na akawauliza umma wanaowakadhibisha kuhusu hilo. Nao wakakataa kuwa Mitume waliwafikishia, basi, hao Manabii watatafuta ushahidi wa umma huu, naye Nabii wao (umma huu) atawatakasa. Na katika Aya hii, kuna ushahidi wa kwamba Ijmaa ya umma huu ni hoja ya uhakika, na kwamba wao wamehifadhiwa kutokana na kukosea kwa sababu ya ujumla wa kauli yake “wastani”. Na kama ingewezekana kuwa wanaweza kukubaliana kukosea (kupotoka), basi hawangekuwa wastani isipokuwa katika baadhi ya mambo tu. Na kauli yake “ili muwe mashahidi juu ya watu” inalazimu kwamba, wakishuhudia juu ya hukumu ya kwamba Mwenyezi Mungu aliihalalalisha au aliiharamisha, au aliifanya kuwa lazima, basi umehifadhiwa (umma huu) katika hilo. Na ndani yake kuna kwamba uadilifu ni sharti katika kuhukumu, kushuhudia, kutoa fatwa, na mfano wa hayo.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Na hatukukifanya kibla ulichokuwa juu yake” ambacho ni kuelekea Bait Al-Maqdis mwanzoni “isipokuwa ili tupate kujua.” Yani elimu ambayo malipo na adhabu vinahusiana nayo. Vinginevyo, Yeye Mwenye Mwenyezi Mungu Mtukufu anajua mambo yote kabla ya kupatikana kwake. Lakini elimu hii (ya azali) haihusiani nayo malipo wala adhabu, kwa sababu ya ukamilifu wa uadilifu wake, na kusimamisha hoja juu ya waja wake. Bali matendo yao yanapopatikana, ndio yanatokea hapo malipo na adhabu. Yani tumeiweka sheria ya kuelekea Kibla hicho ili tumjue na kumtahini “yule anayemfuata Mtume” na kumwamini. Basi akawa anamfuata katika kila hali. Kwa sababu, yeye (Mtume) ni mja tu anayeamrishwa, anayeendeshwa. Na kwa sababu vitabu vilivyotangulia vilikwishasema kuwa ataelekea Al-Ka'ba. Kwa hivyo, muadilifu ni yule ambaye lengo lake ni haki, ambayo inazidishia imani yake na kumtii Mtume. Na ama mwenye kugeukia kwa visigino vyake, akaipa mgongo haki, na akafuata matamanio yake, basi yeye atazidisha ukafiri juu ya ukafiri wake, na kuchanganyikiwa juu ya kuchanganyikiwa kwake, na ataleta hoja batili iliyojengeka juu ya dhana potofu isiyokuwa na hakika. “Na kwa yakini, hilo lilikuwa” yani kukugeuza kutoielekea “jambo kubwa” yani gumu “isipokuwa kwa wale aliowaongoa Mwenyezi Mungu.” Basi wakatambua kwa hilo neema ya Mwenyezi Mungu juu yao, na wakashukuru, na wakakiria wema wake. Kwa maana aliwaelekeza kwenye nyumba hii tukufu, ambayo aliiboresha juu ya sehemu nyinginezo za ardhi, na akafanya kuikusudia kuwa nguzo katika nguzo za Uislamu, na yenye kuyabomoa dhambi na makosa. Na kwa sababu hii, (jambo hili) liliwawia rahisi, na likawa gumu kwa wasiokuwa wao. Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: “Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu.” Yani haimfailii wala haiendani na Yeye Mtukufu. Bali hilo ni miongoni mwa yasiyowezekana kwake. Kwa hivyo, akajulisha kwamba hilo haliwezekani kwake, na ni mustahili kwake kuipoteza imani yenu. Na katika hili kuna bishara njema kubwa kwa wale ambao Mwenyezi Mungu aliwapa neema ya Uislamu na imani kwamba Mwenyezi Mungu atawahifadhia imani yao, na wala hataipoteza. Na kuihifadhi kwake ni kwa aina mbili: Kuihifadhi kutokana na kupotea na kubatilishwa, kwa kuwahifadhi kutokana na kila chenye kuiondoa, na kuipunguza miongoni mwa mitihani inayoleta wasiwasi, na matamanio yenye kuzuia. Na (pili) kuihifadhi kwa kuwakuzia imani hiyo na kuwawezesha yale ambayo imani yao itaongezeka kwayo, na kutimia kwayo yakini yao. Kama vile alivyowaanzisha kwa kuwaongoa kwenye imani, hivyo basi atawahifadhia na kuwatimizia neema yake kwa kuikuza na kukuza malipo yake na thawabu zake, na kuilinda kutokana na kila chenye kuichafua. Bali, ikipatikana mitihani ambayo imekusudiwa kubainisha Muumini wa kweli kutokana na mwongo, basi hiyo huwasafisha Waumini na kudhihirisha ukweli wao. Na ni kana kwamba katika hili kuna kuondoa kile ambacho kingesemwa kwamba kauli yake; “na hatukukifanya kibla ulichokuwa juu yake isipokuwa ili tupate kumjua yule anayemfuata Mtume na yule anayegeukia kwenye visigino vyake.” Huenda ikawa ni sababu ya baadhi ya Waumini kuacha imani yao. Kwa hivyo, akaizuia fikira hii potovu kwa kauli yake; “na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu,” kwa kuweka kwake mtihani huu au (mitihani) isiyokuwa huu. Na waliingia katika hilo, wale waliokufa miongoni mwa Waumini kabla ya kugeuza kwa Al-Kaaba. Kwa maana, Mwenyezi Mungu hapotezi imani yao, kwa sababu walitekeleza amri ya Mwenyezi Mungu na wakamtii Mtume wake katika wakati wake. Na kumtii Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza amri yake katika kila wakati ni kama hivyo. Na katika aya hii, kuna ushahidi wa dhehebu la Ahlul-Sunnah wal-Jama'a kwamba imani inajumuisha matendo ya viungo. Na kauli yake; “kwa hakika, Mwenyezi Mungu kwa watu ni Mpole, Mwenye kuwarehemu.” Yani Yeye ni mwingi wa rehema kwao. Na katika upole wake na rehema yake kwao ni kwamba aliwakamilishia neema zake juu yao ambazo aliwaanzisha nazo. Na kwamba aliwapambanua na yule aliyeingia katika Imani kwa ulimi wake tu bila ya moyo wake. Na kwamba aliwajaribu kujaribu ambako kwa sababu yake imani yao iliongezeka, na daraja zao zikapanda kwa sababu yake. Na kwamba aliwaelekeza kwenye Nyumba ya heshima kubwa zaidi na tukufu zaidi ya (nyumba) zote.