Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 73 · Aya ya 20

Al-Muzzammil 73:20

المزمل

إِنَّ رَبَّكَ يَعْلَمُ أَنَّكَ تَقُومُ أَدْنَىٰ مِن ثُلُثَىِ ٱلَّيْلِ وَنِصْفَهُۥ وَثُلُثَهُۥ وَطَآئِفَةٌ مِّنَ ٱلَّذِينَ مَعَكَ ۚ وَٱللَّهُ يُقَدِّرُ ٱلَّيْلَ وَٱلنَّهَارَ ۚ عَلِمَ أَن لَّن تُحْصُوهُ فَتَابَ عَلَيْكُمْ ۖ فَٱقْرَءُوا۟ مَا تَيَسَّرَ مِنَ ٱلْقُرْءَانِ ۚ عَلِمَ أَن سَيَكُونُ مِنكُم مَّرْضَىٰ ۙ وَءَاخَرُونَ يَضْرِبُونَ فِى ٱلْأَرْضِ يَبْتَغُونَ مِن فَضْلِ ٱللَّهِ ۙ وَءَاخَرُونَ يُقَـٰتِلُونَ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ ۖ فَٱقْرَءُوا۟ مَا تَيَسَّرَ مِنْهُ ۚ وَأَقِيمُوا۟ ٱلصَّلَوٰةَ وَءَاتُوا۟ ٱلزَّكَوٰةَ وَأَقْرِضُوا۟ ٱللَّهَ قَرْضًا حَسَنًا ۚ وَمَا تُقَدِّمُوا۟ لِأَنفُسِكُم مِّنْ خَيْرٍ تَجِدُوهُ عِندَ ٱللَّهِ هُوَ خَيْرًا وَأَعْظَمَ أَجْرًا ۚ وَٱسْتَغْفِرُوا۟ ٱللَّهَ ۖ إِنَّ ٱللَّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌۢ

Maana

Hakika Mola wako Mlezi anajua ya kuwa hakika wewe unakesha karibu na thuluthi mbili za usiku, na nusu yake, na thuluthi yake. Na baadhi ya watu walio pamoja nawe kadhalika. Na Mwenyezi Mungu ndiye anayeukadiria usiku na mchana. Anajua kuwa hamwezi kuweka hisabu, basi amekusameheni. Basi someni kilicho chepesi katika Qur-ani. Anajua ya kuwa baadhi yenu watakuwa wagonjwa, na wengine wanasafiri katika ardhi wakitafuta fadhila ya Mwenyezi Mungu, na wengine wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo someni kilicho chepesi humo, na mshike Sala, na toeni Zaka, na mkopesheni Mwenyezi Mungu mkopo mwema. Na kheri yoyote mnayoitanguliza kwa ajili ya nafsi zenu mtaikuta kwa Mwenyezi Mungu, imekuwa bora zaidi, na ina thawabu kubwa sana. Na mtakeni msamaha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Hakika Mola wako Mlezi anajua ya kuwa hakika wewe unakesha karibu na thuluthi mbili za usiku, na nusu yake, na thuluthi yake. Na baadhi ya watu walio pamoja nawe kadhaalika. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye ukadiria usiku na mchana. Anajua kuwa hamwezi kuweka hisabu, basi amekusameheni. Basi someni kilicho chepesi katika Qur'ani. Anajua ya kuwa baadhi yenu watakuwa wagonjwa, na wengine wanasafiri katika ardhi wakitafuta fadhila ya Mwenyezi Mungu, na wengine wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo someni kilicho chepesi humo, na mshike Swala, na toeni Zaka, na mkopesheni Mwenyezi Mungu mkopo mwema. Na kheri yoyote mnayo itanguliza kwa ajili ya nafsi zenu mtaikuta kwa Mwenyezi Mungu, imekuwa bora zaidi, na ina thawabu kubwa sana. Na mtakeni msamaha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. [20]

[20] Hakika Mola wako Mlezi anajua kwamba wewe, Muhammad, unakesha pengine akali kuliko thuluthi mbili za usiku, na mara nyengine unakesha nusu ya usiku, na pia wanakesha baadhi ya masahaba zako kama ukeshavyo wewe. Na hapana anaye weza kuukadiria urefu wa usiku na mchana, na kudhibiti saa zake, ila Mwenyezi Mungu. Yeye anajua kuwa hamwezi kuhisabu baraabara kila sehemu katika sehemu za usiku na mchana. Kwa hivyo amekukhafifishieni. Basi someni katika Swala kilicho chepesi katika Qur'ani. Yeye anajua kuwa watakuwepo kati yenu walio wagonjwa, ambao watapata taabu kukesha usiku; na wengine wamo safarini kwa ajili ya biashara na kazi, wakitafuta riziki ya Mwenyezi Mungu. Na wengine wanapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kulitukuza Neno lake. Basi someni kilicho chepesi katika Qur'ani, na zishikeni baraabara faridha za Swala, na toeni Zaka iliyo kuwajibikieni, na mkopesheni Mwenyezi Mungu mkopo mwema, kwa kuwapa mafakiri kwa khiari juu ya hayo yaliyo kulazimuni. Na chochote cha kheri mnacho kitanguliza kwa ajili ya nafsi zenu, mtakuta thawabu zake kwa Mwenyezi Mungu zimekuwa bora zaidi kuliko hicho mlicho kiacha na kukitoa, na malipo mema zaidi. Na mtakeni msamaha Mwenyezi Mungu kwa vitendo viovu na kwa upungufu katika vitendo vyema. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya Waumini, na ni Mwenye kuwarehemu.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Hakika Mola wako, (ewe Mtume), Anajua kuwa wewe unasimama kwa swala ya Tahajudi kipindi cha usiku, wakati mwingine chini ya theluthi mbili za usiku, na wakati mwingine unasimama nusu yake, na wakati mwingine theluthi yake. Na wanasimama pamoja nawe kundi la Maswahaba wako. Na Allah Mtukufu, Peke Yake, Ndiye Anayekadiria usiku na mchana, na Anajua vipimo vyake na kipindi kinachopita na kinachobakia, cha mchana na usiku. Allah Mtukufu Anajua kwamba haiwezekani kwenu nyinyi kusimama usiku wote, hivyo basi akawafanyia mambo kuwa mepesi kwenu. Na msome kwenye Swala ya usiku kile kilichokuwa chepesi kwenu kukisoma katika Qur’ani. Allah Mtukufu anajua kuwa miongoni mwenu kuna wanaoelemewa na ugonjwa wasiweze kusimama usiku. Na kuna watu wengine wanatembea ardhini wakifanya biashara na kazi wakitafuata riziki za Allah Mtukufu za halali. Na kuna watu wengine wanapigana jihadi katika njia ya Allah Mtukufu kuliinua neno Lake na kutangaza dini Yake. Basi someni kutoka kwenye Qur’ani kile kilicho chepesi kwenu, na endeleeni kutekeleza faradhi za Swala, na toeni Zaka za lazima kwenu, na toeni sadaka za mali zenu katika njia za wema na hisani kwa kutaka radhi za Allah Mtukufu. Na chochote kile mnachokifanya miongoni mwa njia za wema na kheri na matendo ya utiifu, mtapata malipo yake na thawabu zake kwa Allah Mtukufu Siku ya Kiyama, na hiyo ni bora zaidi kuliko kile mlichokitanguliza duniani na ni chenye thawabu kubwa zaidi. Na mtake msamaha wa Allah Mtukufu katika hali zenu zote. Hakika Allah Mtukufu ni Msamehevu sana kwenu, ni Mwenye huruma na nyinyi.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Muzzammil

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net