Al-A'raaf 7:160
الأعرافوَقَطَّعْنَـٰهُمُ ٱثْنَتَىْ عَشْرَةَ أَسْبَاطًا أُمَمًا ۚ وَأَوْحَيْنَآ إِلَىٰ مُوسَىٰٓ إِذِ ٱسْتَسْقَىٰهُ قَوْمُهُۥٓ أَنِ ٱضْرِب بِّعَصَاكَ ٱلْحَجَرَ ۖ فَٱنۢبَجَسَتْ مِنْهُ ٱثْنَتَا عَشْرَةَ عَيْنًا ۖ قَدْ عَلِمَ كُلُّ أُنَاسٍ مَّشْرَبَهُمْ ۚ وَظَلَّلْنَا عَلَيْهِمُ ٱلْغَمَـٰمَ وَأَنزَلْنَا عَلَيْهِمُ ٱلْمَنَّ وَٱلسَّلْوَىٰ ۖ كُلُوا۟ مِن طَيِّبَـٰتِ مَا رَزَقْنَـٰكُمْ ۚ وَمَا ظَلَمُونَا وَلَـٰكِن كَانُوٓا۟ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ
Na tukawakatakata makabila kumi na mawili, mataifa mbali mbali. Na tulimfunulia Musa wakati kaumu yake walipomwomba maji kwamba: 'Lipige hilo jiwe kwa fimbo yako.' Mara zikabubujika kutoka humo chemchemi kumi na mbili, na kila watu wakajua pahali pao pa kunywea. Na tukawafunikia kivuli kwa mawingu, na tukawateremshia Manna na Salwa. 'Kuleni katika vizuri hivi tulivyowaruzuku.' Na hawakutudhulumu Sisi, bali walikuwa wakijidhulumu wenyewe.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na tuliwagawanya katika makabila kumi na mbili, mataifa mbali mbali. Na tulimfunulia Musa walipo muomba maji watu wake kumwambia: Lipige hilo jiwe kwa fimbo yako. Mara zikatibuka humo chemchem kumi na mbili, na kila watu wakajua mahali pao pa kunywea. Na tukawafunika kivuli kwa mawingu, na tukawateremshia Manna na Salwa. Tukawaambia: Kuleni vizuri hivi tulivyo kuruzukuni. Wala hawakutu- dhulumu Sisi, bali wamejidhulumu wenyewe. [160]
[160] Mwenyezi Mungu amezitaja neema zake juu ya kaumu ya Musa. Akafahamisha kuwa aliwafanya makundi thinaashara, (kumi na mbili) na akawafanya mataifa, na kila taifa likawa na mpango wao, ili kuzuia uhasidi na kukhitalifiana. Na walipo taka watu wake maji jangwani, alimfunulia Musa alipige jiwe kwa fimbo yake. Akalipiga, zikatibuka kutoka kwenye hilo jiwe chemchem kumi na mbili kwa idadi ya kabila zao. Kila kabila kati yao ilijua pahala pake makhsusi pa kunywa. Basi haikuwa huyu kumuingilia huyu. Na akajaalia kiwingu chende kuwapa kivuli chake katika jangwa, kuwakinga na mwako wa jua. Akawateremshia Manna, nacho ni chakula kwa sura kinafanana na mvua ya barafu, na tamu kama asali. Na akateremsha Salwa, naye ni ndege aliye nona. Na akawaambia: Kuleni hivi vinono tulivyo kuruzukuni katika tulivyo kuteremshieni. Lakini walijudhulumu nafsi zao, na wakazikufuru neema hizo, kwa kuzikataa na kutaka nyenginezo. Na Sisi hatukupata madhara kwa udhalimu wao, lakini upungufu wamepata wao.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na tuliwagawa watu wa Mûsã miongoni mwa Wana wa Isrãîl makabila kumi na mbili, kwa idadi ya Asbãṭ- wana wa Ya‛qûb-, kila kabila ikajulikana kupitia kiongozi wake. Na tulimpelekea wahyi Mûsã, walipotaka watu wake kwake maji ya kunywa waliposhikwa na kiu katika kuzunguka kwao, tukamwambia, «Lipige hilo jiwe kwa fimbo yako.» Akalipiga na pakabubujika chemchemi za maji sehemu kumi na mbili, na watu wa kila kabila, miongoni mwa yale makabila kumi na mbili, walijua mahali pao pa kunywa, hakuna kabila litakaloingia sehemu ya kunywa ya kabila lingine. Na tukawafinika kiwingu juu yenu, na tukawateremshia mann- kitu kinachofanana na gundi chenye ladha kama ya asali- na salwã- ndege wanaofanana na wale wanaoitwa sumânâ (tomboro), na tukawaambia, «Kuleni vitu vizuri tulivyowaruzuku.» Walivichukia na kuvichoka hivyo kwa muda mrefu wa kuvitumia na wakasema, «Hatutavumilia juu ya chakula kimoja.» Na wakataka kubadilishiwa kizuri walichonacho kwa ambacho ni kiovu. Na wao hawakutudhulumu sisi walipoacha kumshukuru Allah Mtukufu na kuacha kusimama na yale Aliyoyalazimisha Allah Mtukufu juu yao, lakini walikuwa wakizidhulumu nafsi zao, kwa kuwa walizikosesha kila jema na kuzipeleka kwenye shari na mateso.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net