Al-A'raaf 7:157
الأعرافٱلَّذِينَ يَتَّبِعُونَ ٱلرَّسُولَ ٱلنَّبِىَّ ٱلْأُمِّىَّ ٱلَّذِى يَجِدُونَهُۥ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِى ٱلتَّوْرَىٰةِ وَٱلْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِٱلْمَعْرُوفِ وَيَنْهَىٰهُمْ عَنِ ٱلْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ ٱلطَّيِّبَـٰتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ ٱلْخَبَـٰٓئِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَٱلْأَغْلَـٰلَ ٱلَّتِى كَانَتْ عَلَيْهِمْ ۚ فَٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ بِهِۦ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَٱتَّبَعُوا۟ ٱلنُّورَ ٱلَّذِىٓ أُنزِلَ مَعَهُۥٓ ۙ أُو۟لَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلْمُفْلِحُونَ
Wale ambao wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiyesoma wala kuandika, ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Taurati na Injili, anayewaamrisha mema na anawakataza maovu, na anawahalalishia vizuri, na anawaharamishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo ambayo ilikuwa juu yao. Basi wale waliomwamini yeye, na wakampa taadhima, na wakamnusuru, na wakaifuata nuru ambayo iliteremshwa pamoja naye, hao ndio waliofaulu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiye soma wala kuandika, wanaye mkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anaye waamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na ana waharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyo kuwa juu yao. Basi wale walio muamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyo teremshwa pamoja naye - hao ndio wenye kufanikiwa. [157]
[157] Na nawakusudia khasa wanao mfuata Mtume Muhammad, ambaye haandiki wala hasomi, na ambaye wanakuta sifa zake zimeandikwa katika vitabu vyao vya Taurati na Injili. Yeye anawaamrisha kila kheri na anawakataza kila shari. Na anawahalalishia vitu ambavyo tabia inaviona ni vizuri, na anawaharimishia vitu ambavyo tabia inavichukia kwa kuwa vina madhara, kama damu na mzoga. Na anawaondolea mizigo mizito na mikazo iliyo kuwa ikiwabana. Basi wanao usadiki Utume wake, na wakamsaidia, na wakamuunga mkono, na wakamnusuru na maadui zake, na wakaifuata Qur'ani aliyo teremshiwa pamoja naye kama nuru ya uwongofu, hao basi ndio wenye kufuzu, sio wenginewe ambao hawakumuamini.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Rehema hii nitawaandikia wale wanaomuogopa Allah Mtukufu na kujiepusha na mambo ya kumuasi, na wanaomfuata Mtume aliye Nabii, ambaye hasomi wala haandiki, naye ni Muhammad, (rehema za Allah Mtukufu na amani imshukie,) ambaye wanazipata sifa zake na mambo yake yaandikwa huko kwao katika Taurati na Injili; anawaamrisha kumpwekesha Allah Mtukufu na kumtii na kila lijulikanalo kuwa ni lema, na anawakataza ushirikina na maasia na kila lijulikanalo kuwa ni baya, na anawahalalishia vizuri vya vyakula na vinywaji na kuoana, na anawaharamishia vichafu vya hivyo kama nyama ya nguruwe na vile ambavyo walikuwa wakijihalalishia miongoni mwa vyakula na vinywaji ambavyo aliviharamisha Allah Mtukufu, na anawaondolea wao mambo magumu waliokalifishwa nayo kama kukata mahali pa najisi nguoni, kuzichoma moto ngawira, ulazimu wa kisasi juu ya aliyeua kwa kukusudia au kwa kukosea. Basi wale ambao walimuamini Nabii asiyejua kuandika wala kusoma kilichoandikwa, Muhammad, (rehema za Allah Mtukufu na amani imshukie, na wakaukubali unabii wake,) wakamheshimu, wakamtukuza na wakamuhami na wakaifuata Qur’ani aliyoteremshiwa, wakaufuata mwendo wake kivitendo, hao ni wenye kufaulu kwa kupata yale ambayo Allah Mtukufu Aliwaahidi waja wake Waumini.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net