Al-A'raaf 7:146
الأعرافسَأَصْرِفُ عَنْ ءَايَـٰتِىَ ٱلَّذِينَ يَتَكَبَّرُونَ فِى ٱلْأَرْضِ بِغَيْرِ ٱلْحَقِّ وَإِن يَرَوْا۟ كُلَّ ءَايَةٍ لَّا يُؤْمِنُوا۟ بِهَا وَإِن يَرَوْا۟ سَبِيلَ ٱلرُّشْدِ لَا يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا وَإِن يَرَوْا۟ سَبِيلَ ٱلْغَىِّ يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُوا۟ بِـَٔايَـٰتِنَا وَكَانُوا۟ عَنْهَا غَـٰفِلِينَ
Nitawaepusha na Ishara zangu wale wanaotakabari katika ardhi bila ya haki. Na wao wakiona kila Ishara, hawaiamini. Wakiiona njia ya uwongofu, hawaichukui kuwa ndiyo njia. Lakini wakiiona njia ya ukengeufu, wanaichukua kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu walizikadhibisha Ishara zetu, na walikuwa wakighafilika mbali nazo.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Nitawatenga na Ishara zangu wale wanao fanya kiburi katika nchi bila ya haki. Na wao wakiona kila Ishara hawaiamini. Wakiiona njia ya uwongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wamezikanusha Ishara zetu, na wameghafilika nazo. [146]
[146] Hao walio majeuri na wakapanda kiburi katika ardhi wakakataa kukubali yaliyo sawa bila ya haki, nitawazuia wasiweze kuzizingatia dalili za uwezo wangu ziliomo katika nafsi za watu na jiha zote. Watu hawa hata wakiona kila Ishara inayo thibitisha ukweli wa Mitume wetu hawaisadiki. Na wakiiona njia ya uwongofu hawaipiti, na wakiiona njia ya upotofu ndio wanaipita! Hayo yanatokea kwao kwa sababu wamezikanusha Ishara zetu zilio teremshwa, na wameghafilika na kuongoka kwazo.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Nitazipotoa nyoyo za wenye kufanya kiburi wakaacha kunitii na wenye kuwafanyia watu kiburi pasi na haki zisizielewe hoja na dalili zinazoonesha ukubwa wangu, sheria yangu na hukumu zangu, wawe hawamsikilizi Mtume yoyote kwa kiburi chao. Na wakiona, hawa wenye kuifanyia Imani kiburi, kila alama hawaiyamini, kwa sababu ya kupa mgongo kwao na kupingana kwao na Allah Mtukufu na Mtume Wake. Wakiiona njia ya uongofu hawaifanyi ni njia, na wakiiona njia ya upotevu wanaifanya kuwa ni njia na ni dini. Hayo ni kwa sababu ya kukanusha kwao aya za Allah Mtukufu na kughafilika kwao kuziangalia na kuyatia akilini maana yake.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net