Al-A'raaf 7:143
الأعرافوَلَمَّا جَآءَ مُوسَىٰ لِمِيقَـٰتِنَا وَكَلَّمَهُۥ رَبُّهُۥ قَالَ رَبِّ أَرِنِىٓ أَنظُرْ إِلَيْكَ ۚ قَالَ لَن تَرَىٰنِى وَلَـٰكِنِ ٱنظُرْ إِلَى ٱلْجَبَلِ فَإِنِ ٱسْتَقَرَّ مَكَانَهُۥ فَسَوْفَ تَرَىٰنِى ۚ فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُۥ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُۥ دَكًّا وَخَرَّ مُوسَىٰ صَعِقًا ۚ فَلَمَّآ أَفَاقَ قَالَ سُبْحَـٰنَكَ تُبْتُ إِلَيْكَ وَأَنَا۠ أَوَّلُ ٱلْمُؤْمِنِينَ
Na alipokuja Musa kwenye miadi yetu, na Mola wake Mlezi akamuongelesha, alisema: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe nikutazame. Mwenyezi Mungu akasema: Hutaniona. Lakini utazame huo mlima. Ikiwa utabaki mahali pake, basi utaniona. Basi alipojionyesha Mola wake Mlezi kwa mlima huo, akaufanya upasukepasuke, na Musa akaanguka chini akazimia. Basi alipozindukana, akasema: Subhanaka (Umetakasika)! Nimetubia kwako, na mimi ni wa kwanza wa Waumini.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na alipo kuja Musa kwenye miadi yetu, na Mola wake Mlezi akamsemeza, alisema: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe nikutazame. Mwenyezi Mungu akasema: Hutoniona. Lakini utazame huo mlima. Ukibaki pahala pake basi utaniona. Basi alipo jionyesha Mola Mlezi wake kwa mlima, aliufanya uvurugike, na Musa akaanguka chini amezimia. Alipo zindukana alisema: Subhanaka, Umetakasika! Natubu kwako, na mimi ni wa kwanza wa Waumini. [143]
[143] Na alipo kuja Musa kuzungumza nasi, na Mola Mlezi wake akanena naye kwa maneno ambayo siyo kama kusema kwetu, Musa alisema: Ewe Mola Mlezi wangu! Nionyeshe dhati yako na unidhihirikie, nipate kukutazama nizidi utukufu. Mwenyezi Mungu akasema: Huwezi kuniona. Kisha Subhanahu, Aliye takasika alitaka kumkinaisha kuwa hawezi kumwona, akamwambia: Walakini utazame huo mlima ambao una nguvu kuliko wewe. Ukithibiti pahala ulipo wakati wa kudhihiri kwangu, basi utaniona nikijidhihirisha kwako. Basi Mola wake Mlezi alipo jionyesha kwa huo mlima kwa njia inayo wafikiana naye Mtukufu, mlima ulivurugika ukawa sawa sawa na ardhi. Musa akaanguka, kazimia kwa kitisho alicho kiona. Alipo zindukana kutokana na kuzimia kwake alisema: Nakutakasa mtakaso mkuu na kuonekana kwako duniani! Hakika mimi ninatubu kwako kuja kukutaka kitu bila ya ruhusa yako. Na mimi ni wa mwanzo katika zama zangu wa wanao amini utukufu wako na ubora wako.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na alipokuja Mûsã kwa wakati uliowekwa nao ni muda wa masiku arubaini na Akasema na yeye Mola wake kwa kumpa wahyi wake, maamrisho Yake na makatazo Yake, alifanya hamu ya kumuona Allah Mtukufu akataka amtazame. Allah Mtukufu Akamwambia, «Hutoniona!»Yaani hutaweza kuniona ulimwenguni. «Lakini liangalie jabali, likitulia mahali lilipo nitakapolitokezea, basi utaniona.» Alipojitokeza Mola wake kwa lile jabali alilifanya lipondeke liwe sawa na ardhi. Hapo Mûsã alianguka akiwa amezimia. Alipopata fahamu kutoka kwenye hali ya kuzimia alisema, «Kwa kukutakasa, ewe Mola wangu, na kila sifa isiyolingana na utukufu wako, mimi natubia kwako kutokana na kuomba kwangu kukuona katika uhai huu wa kilimwengu, na mimi ni wa mwanzo wa wenye kukuamini miongoni mwa watu wangu».
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net