Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 58 · Aya ya 1

Al-Mujaadila 58:1

المجادلة

قَدْ سَمِعَ ٱللَّهُ قَوْلَ ٱلَّتِى تُجَـٰدِلُكَ فِى زَوْجِهَا وَتَشْتَكِىٓ إِلَى ٱللَّهِ وَٱللَّهُ يَسْمَعُ تَحَاوُرَكُمَآ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ سَمِيعٌۢ بَصِيرٌ

Maana

Hakika Mwenyezi Mungu amekwishasikia usemi wa mwanamke anayejadiliana nawe juu ya mumewe, na anamlalamikia Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anayasikia majibizano yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia mno, Mwenye kuona zaidi.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

MWENYEZI MUNGU amekwisha sikia usemi wa mwanamke anaye jadiliana nawe juu ya mumewe, na anamshitakia Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anayasikia majibizano yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona. [1]

[1] Mwenyezi Mungu amekwisha sikia kauli ya huyo mwanamke anaye kurejea wewe kwa shauri ya mumewe aliye jitenga naye kwa kudai ati anamwona kama mgongo wa mama yake, na akamlalamikia Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anayasikia hayo maneno mnayo jibizana. Hakika Mwenyezi Mungu anayasikia vyema yote ya kusikiwa, anayaona vyema yote ya kuonekana. Imepokelewa kuwa Sahaba mmoja, aitwaye Aus bin Ass'amit, aliudhika na mkewe aitwaye, Khola bint Tha'labah, akamwambia: "Wewe kwangu mimi kama mgongo wa mama yangu." Na katika siku za Ujahiliya ilikuwa ndio mwanamke kesha harimika kwa mumewe. Mwanamke akenda kumpa khabari Nabii s.a.w., na Mtume akamwambia: "Sijaamrishwa kitu katika kesi yako. Na sioni ila ni kuwa kweli umekwisha harimika kwake." Mwanamke akajadiliana na Mtume s.a.w. na akamrejea tena, na akawa anamshitakia Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kukhofu kufarikiana na mume na kupotea mwanawe. Haukupita muda ila ikateremka Aya hii na tatu zilizo baada yake.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Ashasikia Allah Mtukufu neno (la Khawalah binti ya Tha’labah) anayekurudiarudia kuhusu mumewe (Aws mtoto wa al-Ṣāmit) na kuhusu kile kilichotokea upande wake cha kufanya ẓihār nako ni kule kutamka mumewe kumwambia yeye, «wewe kwangu ni kama mgongo wa mama yangu», yaani katika uharamu wa kumuingilia, na huku anamnyenyekea Allah Mtukufu Aliyetukuka Amtatulie shida yake, na Allah Mtukufu Anayasikia maneno yenu. Hakika Allah Mtukufu ni Msikizi wa kila neno, ni Muoni wa kila kitu, hakifichiki Kwake chochote chenye kufichika.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Mujaadila

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net