Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 5 · Aya ya 6

Al-Maaida 5:6

المائدة

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓا۟ إِذَا قُمْتُمْ إِلَى ٱلصَّلَوٰةِ فَٱغْسِلُوا۟ وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى ٱلْمَرَافِقِ وَٱمْسَحُوا۟ بِرُءُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى ٱلْكَعْبَيْنِ ۚ وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَٱطَّهَّرُوا۟ ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰٓ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَآءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ ٱلْغَآئِطِ أَوْ لَـٰمَسْتُمُ ٱلنِّسَآءَ فَلَمْ تَجِدُوا۟ مَآءً فَتَيَمَّمُوا۟ صَعِيدًا طَيِّبًا فَٱمْسَحُوا۟ بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ ۚ مَا يُرِيدُ ٱللَّهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُم مِّنْ حَرَجٍ وَلَـٰكِن يُرِيدُ لِيُطَهِّرَكُمْ وَلِيُتِمَّ نِعْمَتَهُۥ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

Maana

Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Sala, basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake katika vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba, basi jisafisheni. Na mkiwa wagonjwa au katika safari, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi likusudieni vumbi lililo nzuri, na pakeni nyuso zenu na mikono yenu katika hilo. Hapendi Mwenyezi Mungu kuwatia katika uzito, bali anataka kuwatakasa na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Enyi mlio amini! Mnapo simama kwa ajili ya Swala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu; bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru. [6]

[6] Enyi Waumini! Mkitaka kuswali nanyi hamna udhu, tawadhini kwa kukosha nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake maji kichwa kizima au baadhi yake. Na mkoshe miguu yenu mpaka vifundoni. Mnapo taka kuswali nanyi mna janaba kwa kuingiliana na wake zenu, basi kogeni mwili mzima. Ikiwa mna maradhi ambayo hayakufaliini kutumia maji, au mpo safarini na ipo taabu ya maji, au mmetoka chooni kukidhi haja, au mmeingiliana (kwa lugha ya Qur'ani "kugusana") na wanawake na msipate maji, basi inakupaseni kutayamamu, yaani kujipaka vumbi lilio safi. Na hayo ni kwa kupangusa kwa hilo vumbi nyuso zenu na mikono yenu. Na Mwenyezi Mungu hataki kukudhikini katika hayo anayo kuamrisheni, bali anakupeni sharia za kukusafisheni ndani na nje, ili atimize neema zake juu yenu kwa uwongofu, na kubainisha na kusahilisha, mpate kumshukuru kwa uwongofu wake na kutimilia neema yake kwa kudumisha ut'iifu kwake. T'ahara (Usafi) wa Kiislamu una maana mbili: Moja ni kumwelekea Mwenyezi Mungu Mtukufu moyoni kwa kujiweka tayari kwa hayo, na kufunga azimio kusimama mbele yake na hali ni mwenye nafsi iliyo t'aahiri, na moyo ulio safi kabisa kwake Yeye tu. Pili ni unadhifu wa dhaahiri kwa udhu. Na katika hayo ni kuvikosha viungo vyote vinavyo weza kuchafuka. Na udhu ni jambo la kufanywa mara kwa mara, na huweza kufika hata kutwa mara tano. Pia kuna kukoga unapo ingiliana na mke, na wakati wa damu ya mwezi na uzazi. Udhu na kukoga ni kuondoa takataka zenye vijidudu vya maradhi, na pia huleta uchangamfu kwa kusisimua damu ya kwenye ngozi, na kupoza mishipa. Na kwa hivyo Mtume s.a.w. aliusia: "Ukihamaki tawadha".

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Enyi mlioamini! Mkitaka kuinuka ili kuswali, hali ya kuwa hamuna udhu, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka kwenye visukusuku (Kisukusuku ni kiungo kilichoko kati ya mkono na nyoka mkono). Na pakeni maji kwenye vichwa vyenu na muoshe miguu yenu pamoja na macho mawili ya miguu ( nayo ni mifupa miwili iliyojitokeza katika makutano ya muundi na nyayo). Na mtakapopatikana na tukiyo la hadathi kubwa ya kuondoa utohara, basi jitwahirisheni kwa kuoga kabla ya kuswali. Na mkiwa ni wagonjwa au muko safarini katika hali ya afya, au iwapo mmoja wenu amemaliza haja yake, au amemuingilia mke wake, na mkawa hamkupata maji, basi ipigeni ardhi kwa mikono yenu na mupanguse nyuso zenu na mikono yenu kwayo. Allah Mtukufu Hataki kuwadhiki katika jambo la kujitoharisha, ndipo Akawatolea nafasi na kuwahurumia kwa kuwaruhusu kutayamamu (kutumia mchanga) badala ya kutumia maji katika kujitoharisha. Ruhusa ya kutayamamu ilikuwa ni katika kuzikamilisha neema ambazo zinapelekea kumshukuru Mneemeshaji kwa kumtii katika yale Aliyoyamrisha na kuyakataza.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Maaida

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net