Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 5 · Aya ya 2

Al-Maaida 5:2

المائدة

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ لَا تُحِلُّوا۟ شَعَـٰٓئِرَ ٱللَّهِ وَلَا ٱلشَّهْرَ ٱلْحَرَامَ وَلَا ٱلْهَدْىَ وَلَا ٱلْقَلَـٰٓئِدَ وَلَآ ءَآمِّينَ ٱلْبَيْتَ ٱلْحَرَامَ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّن رَّبِّهِمْ وَرِضْوَٰنًا ۚ وَإِذَا حَلَلْتُمْ فَٱصْطَادُوا۟ ۚ وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَـَٔانُ قَوْمٍ أَن صَدُّوكُمْ عَنِ ٱلْمَسْجِدِ ٱلْحَرَامِ أَن تَعْتَدُوا۟ ۘ وَتَعَاوَنُوا۟ عَلَى ٱلْبِرِّ وَٱلتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا۟ عَلَى ٱلْإِثْمِ وَٱلْعُدْوَٰنِ ۚ وَٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ ۖ إِنَّ ٱللَّهَ شَدِيدُ ٱلْعِقَابِ

Maana

Enyi mlioamini! Msivunje alama za Dini, za Mwenyezi Mungu wala mwezi mtakatifu, wala wanyama wanaopelekwa Makka kuchinjwa kama zawadi, wala wale wanaotiwa vigwe, wala wale wanaoelekea kuiendea Nyumba Takatifu, wakitafuta fadhila kutoka kwa Mola wao Mlezi na radhi. Na mkishatoka katika Ihram, basi windeni. Wala kuwachukia watu kwa kuwa waliwazuia kuufikia Msikiti mtakatifu kusiwapelekeeni kuwafanyia uadui. Na saidianeni katika wema na ucha Mungu. Wala msisaidiane katika dhambi na kupita mipaka. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Enyi mlio amini! Msivunje hishima ya alama ya Dini ya Mwenyezi Mungu wala mwezi mtakatifu, wala wanyama wanao pelekwa Makka kuchinjwa, wala vigwe vyao, wala wanao elekea kwendea Nyumba Takatifu, wakitafuta fadhila na radhi za Mola wao Mlezi. Na mkisha toka Hija yenu basi windeni. Wala kuwachukia watu kwa kuwa wali- kuzuilieni kufika Msikiti mtakatifu kusikupelekeeni kuwafanyia uadui. Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu. [2]

[2] Enyi Waumini! Msivunje hishima ya alama ya Dini ya Mwenyezi Mungu, yaani ibada alizo amrisha Mwenyezi Mungu, kama ibada za Hija wakati wa Ihram, na sharia na hukumu nyenginezo. Wala msivunje hishima ya miezi mitakatifu kwa kuzua vita katika miezi hiyo. Wala msipinge wanyama wanao pelekwa Makka, kwa kupokonya au kuzuia wasifike huko, wala msiwavue vigwe walivyo fungwa shingoni mwao kuwa ni alama kuwa wamekusudiwa kupelekwa Nyumba Takatifu, na kuwa watakuwa dhabihu wa Hija. Wala msiwapinge wanao kusudia kwenda Hija nao wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Na mkisha vua Ihram na mkatoka kwenye eneo la Alharam, basi mnaweza kuwinda mtakavyo. Wala msipelekewe na chuki yenu kubwa kwa wale walio kuzuieni kufika kwenye Msikiti wa Makka mkawafanyia uadui. Enyi Waumini! Saidianeni katika kutenda kheri na mambo yote ya ut'iifu, wala msisaidiane katika maasi, na kupindukia mipaka aliyo iweka Mwenyezi Mungu. Na ogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu na nguvu zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuwaadhibu wale wanao mkosa. Mwenye kuhiji akisha "harimiya" (yaani kunuia kuhiji) huwa haramu kwake baadhi ya mambo, kama kuvaa nguo iliyo shonwa, kukata nywele, kuwinda, n.k. mpaka amalize "Ihram" nako ndio kwisha ibada ya Hija.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Enyi mliomuamini Allah Mtukufu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, msivuke mipaka ya Allah Mtukufu na alama Alizoziwekea hiyo mipaka yake. Na msihalalishe vita katika miezi mitukufu, nayo ni Mfungopili, Mfungotatu, Mfungo nne na Rajabu- na hilo lilikuwa katika mwanzo wa Uislamu-. Na msivunje heshima ya wanyama waliokusudiwa kuchinjwa katika ibada ya Hija, wala msivunje heshima ya vitu walivyovishwa navyo. Kwani walikuwa wakiwavalisha kwenye shingo zao miseja ya sufi au ya nyoya, ikiwa ni kitambulisho kwamba mnyama huyo ni wa kuchinjwa katika ibada ya Hija na kwamba mwenye mnyama anaenda Hija. Wala msihalalishe kuwapiga vita wenye kuikusudia Nyumba tukufu, ambao wanazitafuta fadhila za Allah Mtukufu zinazowatengezea maisha yao na kumridhisha Mola wao. Na pindi mnapomaliza ibada yenu ya Hija, mnahalalishiwa kuwinda. Na isiwapelekee nyinyi kuwachukia baadhi ya watu kwa kuwa waliwazuia nyinyi kufika Msikiti mtukufu, kama ilivyotokea katika mwaka wa Hudaibiyah, kuacha kuwafanyia uadilifu. Na saidianeni kati yenu, enyi Waumini, kufanya wema na kumcha Allah Mtukufu wala msisaidiane kwenye mambo ya madhambi, maasia na kuivuka mipaka ya Allah Mtukufu. Na jihadharini kuenda kinyume na amri ya Allah Mtukufu, kwani Yeye ni Mkali wa kutesa.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Maaida

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net