Muhammad 47:4
محمدفَإِذَا لَقِيتُمُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ فَضَرْبَ ٱلرِّقَابِ حَتَّىٰٓ إِذَآ أَثْخَنتُمُوهُمْ فَشُدُّوا۟ ٱلْوَثَاقَ فَإِمَّا مَنًّۢا بَعْدُ وَإِمَّا فِدَآءً حَتَّىٰ تَضَعَ ٱلْحَرْبُ أَوْزَارَهَا ۚ ذَٰلِكَ وَلَوْ يَشَآءُ ٱللَّهُ لَٱنتَصَرَ مِنْهُمْ وَلَـٰكِن لِّيَبْلُوَا۟ بَعْضَكُم بِبَعْضٍ ۗ وَٱلَّذِينَ قُتِلُوا۟ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ فَلَن يُضِلَّ أَعْمَـٰلَهُمْ
Basi mnapowakuta wale waliokufuru, wapigeni shingoni mwao, mpaka mkiwadhoofisha, wafungeni pingu. Tena waachilieni kwa hisani au wajikomboe, mpaka vita vipoe. Ndivyo hivyo. Na lau angelitaka Mwenyezi Mungu, angeliwashinda mwenyewe, lakini haya ni kwa sababu awatie mitihani nyinyi kwa nyinyi. Na wale waliouliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu, hatayapoteza matendo yao.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Basi mnapo wakuta walio kufuru wapigeni shingoni mwao, mpaka mkiwadhoofisha wafungeni pingu. Tena waachilieni kwa hisani au wajikomboe, mpaka vita vipoe. Ndio hivyo. Na lau angeli taka Mwenyezi Mungu angeli washinda mwenyewe, lakini haya ni kwa sababu akutieni mitihani nyinyi kwa nyinyi. Na walio uliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu hatazipoteza a'mali zao. [4]
[4] Mtapo kutana na walio kufuru katika vita basi wapigeni kwenye shingo zao, mpaka mtakapo wadhoofisha kwa wingi wa kuwauwa, basi tena wafungeni mateka. Tena ama waachilieni wende zao kwa wema na ihsani, baada ya kwisha vita, kwa kuwaachia bila ya fidia, au kwa fidia ya kutoa mali au kubadilishana kwa mateka wa Kiislamu. Inakuwa mmewaachilia kwa badali. Huu ndio uwe mwendo wenu na makafiri mpaka vita vimalizike kabisa. Mwenyezi Mungu anawahukumieni hivyo. Na lau angeli taka bila ya shaka angeli washinda bila ya vita, lakini haya ni ili awajaribu Waumini kwa makafiri kama mtihani ndio ameamrisha Jihadi. Na walio uwawa katika njia ya Mwenyezi Mungu kabisa hatoacha vitendo vyao vipotee. Atawahidi, na azitengeneze nyoyo zao, na awatie katika Pepo aliyo kwisha wajuulisha. Katika Aya hii tukufu zimetajwa "shingo" khasa, kwa sababu kuzipiga hizo ndio njia inayo faa mno kummaliza upesi mwenye kupigwa bila ya kumuadhibu na kumtesa. Kwani imethibiti kwa ilimu kuwa shingo ndiyo kiungo baina ya kichwa na kiwiliwili kizima. Basi ukikatika mshipa wa uti wa mgongo wenye kupeleka hisiya zote, basi viungo vyote muhimu vinapooza. Na ikikatika mishipa ya damu, damu inasita kufika kwenye ubongo. Na zikikatika njia za kupitisha hewa, basi pumzi husita. Na katika hali hizi zote uhai unakatika mara moja.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Basi mkipambana, enyi Waumini, na wale waliokufuru katika viwanja vya vita, piganeni nao kidhati na mzipige shingo zao. Hata mtakapowadhoofisha kwa kuwaua kwa wingi na mkazivunja nguvu zao, wafungeni kisawasawa wale mnaowateka. Kisha basi ima muwasamehe kwa kuwafungua na kuwaacha bila kutoa fidia badala yake, au wajikomboe kwa kutoa fidia, au watiwe utumwani au wauawe. Na endeleeni kufanya hivyo mpaka vita vimalizike. Hiyo ndiyo hukumu iliyotajwa ya kuwatahini Waumini kwa makafiri na ushindi kuzunguka baina yao. Na lau Allah Mtukufu angetaka wangepata ushindi Waumini bila ya vita, lakini Allah Mtukufu Amejaalia mateso yao yawe mikononi mwenu, ndipo Akaweka sheria ya jihadi ili Awajaribu nyinyi kwa wao, na Ainusuru kupitia kwenu Dini Yake. Na wale Waumini waliouwawa katika njia ya Allah Mtukufu, hatayaporomosha Allah Mtukufu malipo mema ya matendo yao.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net