An-Nisaa 4:92
النساءوَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ أَن يَقْتُلَ مُؤْمِنًا إِلَّا خَطَـًٔا ۚ وَمَن قَتَلَ مُؤْمِنًا خَطَـًٔا فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ وَدِيَةٌ مُّسَلَّمَةٌ إِلَىٰٓ أَهْلِهِۦٓ إِلَّآ أَن يَصَّدَّقُوا۟ ۚ فَإِن كَانَ مِن قَوْمٍ عَدُوٍّ لَّكُمْ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ ۖ وَإِن كَانَ مِن قَوْمٍۭ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُم مِّيثَـٰقٌ فَدِيَةٌ مُّسَلَّمَةٌ إِلَىٰٓ أَهْلِهِۦ وَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ ۖ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ شَهْرَيْنِ مُتَتَابِعَيْنِ تَوْبَةً مِّنَ ٱللَّهِ ۗ وَكَانَ ٱللَّهُ عَلِيمًا حَكِيمًا
Na haiwi Muumini kumuua Muumini isipokuwa kwa kukosea. Na mwenye kumuua Muumini kwa kukosea, basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya kuwapa jamaa zake maiti, isipokuwa waiache wenyewe kuwa ni sadaka. Na akiwa ni wa kutoka kwa kaumu ambao ni maadui zenu, ilhali yeye ni Muumini, basi ni kwa kumkomboa mtumwa aliye Muumini. Na akiwa ni miongoni wa kaumu ambao kuna agano baina yenu na wao, basi wapewe diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiyepata, basi afunge miezi miwili mfululizo, iwe ni toba kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema, Mwenye hekima kubwa.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na haiwi Muumini kumuuwa Muumini ila kwa kukosea. Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukosea basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya kuwapa jamaa za maiti, isipo kuwa waache wenyewe kuwa ni sadaka. Na akiwa ni jamaa wa maadui zenu, hali yeye ni Muumini, basi ni kumkomboa mtumwa aliye Muumini. Na akiwa ni miongoni wa watu ambao pana ahadi baina yenu na wao basi wapewe diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiye pata, basi afunge miezi miwili mfululizo, kuwa ni toba kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima. [92]
[92] Kuwagawa wanaafiki namna hii ni kwa ajili ya kutoka shakani, ili Muumini asimuuwe Muumini mwenziwe kwa kumdhania kuwa ni mnaafiki. Na haijuzu kumuuwa Muumini ila kwa kukosea, bila ya kukusudia. Na katika hali ya kumuuwa Muumini kwa kukosea akiwa anaishi chini ya utawala wa dola ya Kiislamu, basi atatoa muuwaji diya kuwapa walio fiwa kuwa ni fidia kwa mtu waliye mkosa, na tena amkomboe mtumwa aliye Muumini iwe ni kuwafidia umma wa Kiislamu kwa walicho kosa. Kwani kumkomboa Muumini ni kama kumhuisha mtu kwa kumpatia uhuru. Inakuwa kwa kukomboa shingo ya Muumini ni kuulipa umma wa Kiislamu kwa walicho kosa. Ikiwa aliye uliwa yumo katika watu ambao wana mapatano ya amani na Waislamu, basi yapasa kumpa uhuru mtumwa na kuwalipa watu wa maiti diya, kwani inakuwa hawaichukui hiyo diya kwa kuwaudhi Waislamu kwa sababu ya mapatano yao. Na ikiwa mwenye kuuwa bila ya kukusudia hakupata mtumwa Muumini wa kumkomboa, basi afunge miezi miwili mfululizo, asile mchana hata siku moja. Hayo yawe ni kuitengeza nafsi na kujizoesha kuwa na hadhari zaidi. Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika na Aliye tukuka anazijua sana nafsi za watu na niya zao. Naye ni Mwenye hikima, anajua kuzipanga adhabu zake. "Kuulipa" kwa kuwa utumwa ni amana ya mtu, na kumkomboa mtumwa ni kumhuisha mtu. Akiuliwa Muumini kwa kukosea, na mwenye kuuwa akakomboa shingo ya Muumini basi huyo amehuisha na kuulipa umma.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Si haki kwa yoyote aliyeamini kumfanyia uadui ndugu yake aliyeamini kwa kumuua bila haki labda itokee kuwa limetokea hilo kimakosa kwa kutokusudia. Na yoyote ambaye kosa hilo lilitokea kwake, basi ni juu yake aache huru mtumwa aliyeamini na atoe fidia iliyokadiriwa kiwango chake kuwapa mawalii wa aliyeuawa, isipokuwa iwapo watamuachia kwa njia ya sadaka na watamsamehe. Iwapo muuliwa anamuamini Allah Mtukufu na anaiamini haki aliyoteremshiwa Mtume Wake Muhammad, rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie, na akawa ni katika ukoo wa watu makafiri ambao ni maadui wa Waislamu, basi ni juu ya muuaji aache huru mtumwa aliyeamini. Na iwapo muuliwa ni miongoni mwa watu ambao baina yenu na wao kuna ahadi na mapatano, basi ni juu ya yule aliyemuua, ili Allah Mtukufu Amkubalie toba yake, aache huru mtumwa aliyeamini; asipopata uwezo wa kuacha huru mtumwa aliyeamini, ni juu yake afunge miezi miwili yenye kufuatana. Allah Mtukufu, ni Mjuzi wa hakika ya mambo ya waja Wake, ni Mwenye hekima katika sheria Zake Alizowawekea.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net