An-Nisaa 4:23
النساءحُرِّمَتْ عَلَيْكُمْ أُمَّهَـٰتُكُمْ وَبَنَاتُكُمْ وَأَخَوَٰتُكُمْ وَعَمَّـٰتُكُمْ وَخَـٰلَـٰتُكُمْ وَبَنَاتُ ٱلْأَخِ وَبَنَاتُ ٱلْأُخْتِ وَأُمَّهَـٰتُكُمُ ٱلَّـٰتِىٓ أَرْضَعْنَكُمْ وَأَخَوَٰتُكُم مِّنَ ٱلرَّضَـٰعَةِ وَأُمَّهَـٰتُ نِسَآئِكُمْ وَرَبَـٰٓئِبُكُمُ ٱلَّـٰتِى فِى حُجُورِكُم مِّن نِّسَآئِكُمُ ٱلَّـٰتِى دَخَلْتُم بِهِنَّ فَإِن لَّمْ تَكُونُوا۟ دَخَلْتُم بِهِنَّ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ وَحَلَـٰٓئِلُ أَبْنَآئِكُمُ ٱلَّذِينَ مِنْ أَصْلَـٰبِكُمْ وَأَن تَجْمَعُوا۟ بَيْنَ ٱلْأُخْتَيْنِ إِلَّا مَا قَدْ سَلَفَ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ غَفُورًا رَّحِيمًا
Mmeharamishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na khaalati zenu, na binti wa kaka, na binti wa dada, na mama zenu waliowanyonyesha, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wa wake zenu, na watoto wenu wa kambo walio katika ulinzi wenu waliozaliwa na wake zenu mliowaingilia. Ikiwa hamkuwaingilia, basi hakuna ubaya juu yenu. (Pia mmeharamishiwa) wake wa watoto wenu waliotoka katika migongo yenu. Na kuwaoa kwa pamoja dada wawili isipokuwa yale yaliyokwishapita. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Mmeharimishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na khaalati zenu, na binti wa ndugu mume, na binti wa dada, na mama zenu walio kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wa wake zenu, na watoto wenu wa kambo walio katika ulinzi wenu walio zaliwa na wake zenu mlio waingilia. Ikiwa hamkuwaingilia basi hapana lawama juu yenu. (Pia mmeharimishwa) wake wa watoto wenu walio toka katika migongo yenu. Na kuwaoa pamoja dada wawili isipo kuwa yale yaliyo kwisha pita. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. [23]
[23] Mwenyezi Mungu amekuharimishieni kuwaoa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu (ndugu wanawake) na shangazi zenu, na khaalati zenu (mama wadogo) na binti wa ndugu, na binti wa dada, na mama walio kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wakwe. Na walio harimishwa bila ya kunasibiana kwa damu ni: mama wa kunyonyesha, dada wa kunyonya, mama mkwe, binti za wake kwa waume wengine ikiwa hao wake wameingiliwa, na wake wa watoto mlio wazaa, na kuwaoa pamoja ndugu wawili. Yaliyo pita katika siku za ujahili yamesamehewa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe kwa yaliyo pita kabla ya mpango huu, na Mwenye kuwarehemu katika aliyo kuwekeeni sharia. Ni Sharia ya Kiislamu pekee iliyo harimisha kwa sababu ya kunyonyesha. Anaye nyonya anakula kutokana na mwili wa mnyonyeshaji kama anavyo kula kutokana na mama yake ndani ya tumbo lake. Wote hao wawili wanakuwa ni sehemu yake huyo mtoto. Hapana khitilafu baina ya kukua ndani ya chumba na ndani ya tumbo. Na katika kuharimisha kwa kunyonyesha ni kumtukuza mnyonyeshaji, kwani anakuwa kama mama. Na haya ni kuzidi kushajiisha kunyonyesha kimaumbile, sio kwa chupa, kwa watoto wachanga.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Allah Mtukufu Amewaharamishia kuwaoa mama zenu, wanaingia kwenye uharamu huu mabibi wa upande wa baba na upande wa mama, na mabinti zenu, wanaingia kwenye uharamu huu mabinti wa watoto wa kiume au wa kike na kwenda chini, na dada zenu kwa baba na mama au kwa baba au kwa mama, na mashangazi zenu, nao ni ndugu wa kike wa baba zenu na babu zenu, na makhalati zenu, nao ni dada za mama zenu na bibi zenu, na mabinti wa ndugu wa kiume na mabinti wa ndugu wa kike; na waingia humo watoto wao, na mama zenu waliowanyonyesha, na dada zenu mlionyonya nao; na Mtume, rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie, ameharamisha kwa ajili ya kunyonya kila aliyeharamishwa kwa ajili ya ukaribu wa nasaba. Pia ni haramu kuwaoa mama za wake zenu, muwe mumewaingilia hao wake zenu au hamukuwaingilia, na mabinti wa wake zenu wa mababa wengine ambao kawaida wanalelewa majumbani mwenu na chini ya uangalizi wenu, wao ni haramu kuwaoa hata kama hawamo majumbani mwenu, lakini kwa sharti ya kuwaingilia mama zao. Na iwapo hamkuwaingilia mama zao, na mkawataliki au wakafa kabla ya kuwaingilia, hapo hapana makosa kuwaoa mabinti wao. Pia amewaharamishia Allah Mtukufu kuwaoa waliokuwa wake wa watoto wenu watokao migongoni mwenu, na wale walioshikanishwa na wao ambao ni watoto wenu wa kiume kwa kunyonya. Kuharamishwa huku kunakuwa kwa kufunga ndoa, awe yule mtoto wa kiume amemuingilia mkewe au hakumuingilia. Pia Amewaharamishia kuwakusanya pamoja, kwenye ndoa, dada wawili wa nasaba au wa kunyonya, isipokuwa yale yaliopita mlioyafanya katika zama za kabla ya Uislamu. Kadhalika, haifai kuwakusanya, kindoa, mwanamke na shangazi yake au khalati yake, kama ilivyokuja katika Sunnah. Allah Mtukufu daima ni Mwenye kuwasamehe watenda madhambi pindi wanapotubia. Ni Mwenye huruma nao, Hawakalifishi wasiloliweza.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net