Al-Qasas 28:15
القصصوَدَخَلَ ٱلْمَدِينَةَ عَلَىٰ حِينِ غَفْلَةٍ مِّنْ أَهْلِهَا فَوَجَدَ فِيهَا رَجُلَيْنِ يَقْتَتِلَانِ هَـٰذَا مِن شِيعَتِهِۦ وَهَـٰذَا مِنْ عَدُوِّهِۦ ۖ فَٱسْتَغَـٰثَهُ ٱلَّذِى مِن شِيعَتِهِۦ عَلَى ٱلَّذِى مِنْ عَدُوِّهِۦ فَوَكَزَهُۥ مُوسَىٰ فَقَضَىٰ عَلَيْهِ ۖ قَالَ هَـٰذَا مِنْ عَمَلِ ٱلشَّيْطَـٰنِ ۖ إِنَّهُۥ عَدُوٌّ مُّضِلٌّ مُّبِينٌ
Na akaingia mjini wakati wa kughafilika wenyeji wake, na akakuta humo wanaume wawili wanapigana - mmoja ni katika watu wake, na mwingine katika maadui zake. Kwa hivyo, yule wa kutoka kwa watu wake akamtaka msaada kumpiga adui yake. Kwa hivyo, Musa akampiga ngumi, na akamuua. Akasema, "Hiki ni katika kitendo cha Shetani. Hakika yeye ni adui, mpotezaji dhahiri."
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na akaingia mjini wakati wa kughafilika wenyeji wake, na akakuta humo watu wawili wanapigana - mmoja ni katika wenzake, na mwengine katika maadui zake. Yule mwenzake alimtaka msaada kumpiga adui yake. Musa akampiga ngumi, akamuuwa. Akasema: Hiki ni kitendo cha Shet'ani; hakika yeye ni adui, mpotezaji dhaahiri. [15]
[15] Musa akaingia mjini Misri wakati walipo kuwa watu wake wameghafilika. Akawakuta watu wawili wanapigana. Mmoja ni katika Wana wa Israili, na mwengine katika kaumu ya Firauni. Yule Muisraili akamtaka msaada kumpiga khasimu yake. Naye Musa akamsaidia. Akampiga konde yule khasimu, akamuuwa bila ya kukusudia. Musa akajuta na akasema: Hakika mimi kuja kufanya kitendo hichi ni kazi ya Shetani. Hakika Shetani ni adui aliye wazi kwa uadui na kupoteza.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na Mûsã aliingia mjini kwa kujificha wakati ambapo watu wake walikuwa wako katika hali ya kughafilika, akawapata humo watu wawili wanapigana, mmoja wao ni katika wana wa Isrãîl jamaa wa Mûsã na mwingine ni katika jamaa wa Firáwn. Basi yule aliyekuwa ni katika jamaa wa Mûsã alitaka msaada dhidi ya yule Aliyekuwa katika maadui zake, hapo Mûsã akampiga kofi na akafa. Mûsã akasema alipomuua, «Huu ni katika ushawishi wa Shetani aliyenipandisha hasira zangu mpaka nikampiga huyu akafa. Hakika ya Shetani ni adui ya mwanadamu, ni mwenye kupoteza njia ya uongofu, ni mwenye uadui wa waziwazi.» Kitendo hiki cha Mûsã kilikuwa kabla ya kupewa unabii.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net