Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 22 · Aya ya 5

Al-Hajj 22:5

الحج

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ إِن كُنتُمْ فِى رَيْبٍ مِّنَ ٱلْبَعْثِ فَإِنَّا خَلَقْنَـٰكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ مِنْ عَلَقَةٍ ثُمَّ مِن مُّضْغَةٍ مُّخَلَّقَةٍ وَغَيْرِ مُخَلَّقَةٍ لِّنُبَيِّنَ لَكُمْ ۚ وَنُقِرُّ فِى ٱلْأَرْحَامِ مَا نَشَآءُ إِلَىٰٓ أَجَلٍ مُّسَمًّى ثُمَّ نُخْرِجُكُمْ طِفْلًا ثُمَّ لِتَبْلُغُوٓا۟ أَشُدَّكُمْ ۖ وَمِنكُم مَّن يُتَوَفَّىٰ وَمِنكُم مَّن يُرَدُّ إِلَىٰٓ أَرْذَلِ ٱلْعُمُرِ لِكَيْلَا يَعْلَمَ مِنۢ بَعْدِ عِلْمٍ شَيْـًٔا ۚ وَتَرَى ٱلْأَرْضَ هَامِدَةً فَإِذَآ أَنزَلْنَا عَلَيْهَا ٱلْمَآءَ ٱهْتَزَّتْ وَرَبَتْ وَأَنۢبَتَتْ مِن كُلِّ زَوْجٍۭ بَهِيجٍ

Maana

Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka juu ya kufufuliwa, basi kwa hakika Sisi tulikuumbeni kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha kutokana na kipande cha damu iliyogandana, kisha kutokana na kipande cha nyama chenye umbo na kisichokuwa na umbo, ili tuwabainishie. Nasi tunakiweka katika matumbo ya uzazi tunachokitaka mpaka muda uliowekwa. Kisha tunawatoa kwa hali ya mtoto mchanga, kisha mfikie kutimia akili. Na wapo katika nyinyi wanaokufa, na wapo katika nyinyi wanaorudishwa kwenye umri wa unyonge kabisa, hata mtu awe hajui kitu baada ya kuwa anakijua. Na unaiona ardhi imetulia kimya, lakini tunapoyateremsha maji juu yake, husisimka na kututumka, na kumea kila namna ya mimea mizuri.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya kufufuliwa basi kwa hakika Sisi tulikuumbeni kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha kutokana na kipande cha damu ilio gandana, kisha kutokana na kipande cha nyama chenye umbo na kisicho kuwa na umbo, ili tukubainishieni. Nasi tunakiweka katika matumbo ya uzazi tunacho kitaka mpaka muda ulio wekwa. Kisha tunakutoeni kwa hali ya mtoto mchanga, kisha mfikie kutimia akili. Na wapo katika nyinyi wanao kufa, na wapo katika nyinyi wanao rudishwa kwenye umri wa unyonge kabisa, hata mtu awe hajui kitu baada ya kuwa anakijua. Na unaiona ardhi imetulia kimya, lakini tunapo yateremsha maji juu yake husisimka na kututumka, na kumea kila namna ya mimea mizuri. [5]

[5] Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya kukufufueni baada ya kufa, basi katika kuumbwa kwenu ipo dalili ya kuweza kwetu kufufua. Tulikuumbeni asili yenu kutokana na udongo, kisha tukaufanya tone ya manii, kisha baada ya muda tukaigeuza ikawa kipande cha damu iliyo gandana. Kisha tukaifanya kipande cha nyama yenye sura ya kibinaadamu, au isiyo kuwa na sura, ili tukubainishieni uweza wetu wa kuanza uumbaji na kuendeleza kukuza kwa viwango na madaraja, na kugeuza kutoka hali hii na kuingia nyengine. Na katika viliomo katika matumbo ya mzazi vipo tunavyo viharibu tuvitakavyo na tunaviweka imara na madhubuti tuvitakavyo, mpaka utimie muda wa kuzaliwa. Kisha tunakutoeni kwenye matumbo ya mama zenu muwe watoto wachanga. Kisha tunakuleeni mpaka mkamilike akili na nguvu. Na baada ya hayo wapo katika nyinyi ambao Mwenyezi Mungu huwafisha, na wapo ambao umri wao hurefushwa mpaka wakafikia ukongwe wa kupiswa, ujuzi wao na kufahamu kwao mambo kukasita. Na aliye kuumbeni kwa sura hii tangu mwanzo hashindwi kukurudisheni tena. Na jambo jengine la kukuonyesha kudra ya Mwenezi Mungu kufufua ni kuwa wewe unaiona ardhi kavu yabisi; tukiiteremshia maji uhai unaitambalia, na hiyo ardhi hugutuka, na huzidi na hututumka kwa maji na hewa iliyo ingia ndani yake, na hapo tena hutokeza namna mbali mbali za mimea inayo furahisha kuiona, na uzuri wake ukazagaa, na mwenye kuiona roho yake ikakunjuka. (Maurice Bucaille, mtaalamu wa Kifaransa maarufu aliye silimu, amelifasiri neno A'laqa kwa maana ya "kitu kilicho tundikwa". Na hivyo ndivyo inavyo thibitisha Sayansi ya hivi sasa, kuwa mbegu ya uzazi ikisha pandikizwa huja ikaning'inia kama iliyo tundikwa kwenye tumbo la uzazi. Tazama pia 23.14, 40.67, 75.37-38 na kadhaalika Sura ya 5 ya Annisaa Aya 129, inayo eleza kuwa msimwache mke "kama aliye tundikwa")

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Enyi watu, mkiwa mna shaka ya kuwa Allah Mtukufu atawafufua wafu, basi sisi tumemuumba baba yenu Adam kutokana na mchanga kisha kizazi chake kikazaana kutokana na nuṭfah, nayo ni manii ambayo mwanamume anayarusha kwenye kizazi cha mwanamke, yakageuka kwa uwezo wa Allah Mtukufu yakawa ‛alaqah, nalo ni pande la damu nyekundu iliyo nzito, kisha yakawa muḍghah, nacho ni kinofu kidogo cha nyama cha kuweza kutafunika, mara nyingine kikawa kitaumbwa, yaani kiumbike kikamilifu mpaka kifikie hadi ya kutoka kwa mtoto akiwa hai, na mara nyingine kisiumbike kikamilifu kikatoka kabla ya kutimia, ili tuwafafanulie ukamilifu wa uwezo wetu wa kupelekesha miezi ya uumbaji. Na tunakibakisha kwenye kizazi tunachokitaka, nacho ni kile kinachoendelezwa kuumbwa kwake mpaka wakati wa kuzaliwa kwake na itimie ile miezi ya kuzaliwa watoto wakiwa wadogo, wakue mpaka wafikie umri wa kuwa na nguvu, nao ni wakati wa ujana na nguvu na kukamilika akili. Na baadhi ya watoto huenda wakafa kabla ya hapo, na baadhi yao wanakuwa mpaka wanafikisha miaka ya ukongwe na udhaifu wa akili, akawa huyu aliyezeeka hajui kitu alichokuwa akikijua kabla ya hapo. Na utaiona ardhi ni kavu, imekufa haina mimea yoyote, tuyateremshapo maji juu yake, inatikisika kwa mimea ikawa inafunguka, inachepuza, inanyanyuka na kuongezeka kwa kutosheka na maji, na ikaotesha kila aina ya mimea mizuri yenye kuwafurahisha wenye kuangalia.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Hajj

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net