Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 22 · Aya ya 40

Al-Hajj 22:40

الحج

ٱلَّذِينَ أُخْرِجُوا۟ مِن دِيَـٰرِهِم بِغَيْرِ حَقٍّ إِلَّآ أَن يَقُولُوا۟ رَبُّنَا ٱللَّهُ ۗ وَلَوْلَا دَفْعُ ٱللَّهِ ٱلنَّاسَ بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لَّهُدِّمَتْ صَوَٰمِعُ وَبِيَعٌ وَصَلَوَٰتٌ وَمَسَـٰجِدُ يُذْكَرُ فِيهَا ٱسْمُ ٱللَّهِ كَثِيرًا ۗ وَلَيَنصُرَنَّ ٱللَّهُ مَن يَنصُرُهُۥٓ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَقَوِىٌّ عَزِيزٌ

Maana

Wale ambao walitolewa majumbani mwao pasina haki, ila kwa kuwa wanasema: "Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu!" Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawakingi watu kwa watu, basi hapana shaka zingelivunjwa nyumba za watawa, na makanisa, na masinagogi, na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayemsaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mtukufu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawakingi watu kwa watu, basi hapana shaka zingeli vunjwa nymba za wat'awa, na makanisa, na masinagogi, na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anaye msaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu. [40]

[40] Hao ambao makafiri wamewadhulumu na wakawalazimisha waache mji wao wa Makka wauhame. Na wao hawakuwa na kosa lolote ila ni kuwa walimjua Mwenyezi Mungu na wakamuabudu Yeye pekee. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakuwatumilia kwa ajili ya Haki wasaidizi wa kumnusuru Yeye na wakamtetea kupinga jeuri za madhaalimu, basi hapana shaka upotovu ungeli enea, na majeuri wangeli endelea katika jeuri zao, na sauti ya haki wangeli inyamazisha. Wala wasingeli achiliwa Wakristo makanisa yao, wala mamonaki (wat'awa wa Kikristo) wasinge baki na monastari zao (nyumba zao za ibada), wala Mayahudi wansinge kuwa na masinagogi yao, wala Waislamu wasinge kuwa na misikiti yao, ambamo mote humo hutajwa kwa wingi jina la Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu amechukua juu ya nafsi yake ahadi ya nguvu ya kwamba atamsaidia na kumnusuru kila anaye isaidia Dini yake, na atamtukuza kila mwenye kulitukuza Neno la Haki katika ulimwengu. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu haiendi kinyume. Kwani Yeye ni Mwenye nguvu wa kutimiza alitakalo, Mtukufu hashindwi na yeyote.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Wale ambao walilazimishwa kutoka majumbani mwao, si kwa lolote isipokuwa ni kwa kuwa wamesilimu na wamesema, «Mola wetu ni Allah Mtukufu Peke Yake.» Na lau si mpango Aliouweka Allah Mtukufu wa kuondoa maonevu ambayo kwayo wananufaika watu wa dini zote zilizoteremshwa na kuurudisha ubatilifu kwa kuruhusu kupigana, haki ingeshindwa katika kila ummah, ardhi ingeharibiwa, sehemu za ibada zingevunjwa, kama masinagogi ya watawa, makanisa ya Wanaswara, majumba ya ibada ya Mayahudi na misikiti ya Waislamu ambayo Wanaswali ndani yake, na wanamtaja Allah Mtukufu humo kwa wingi. Na mwenye kufanya bidii kuitetea Dini ya Allah Mtukufu, basi Allah Mtukufu Atamnusuru juu ya adui yake. Hakika Allah Mtukufu ni Mwenye nguvu Asiyeshindwa, ni Mshindi Asiyefikiwa, Amewatendesha nguvu viumbe na Amezishika paa za nyuso zao.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Hajj

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net