Al-Baqara 2:85
البقرةثُمَّ أَنتُمْ هَـٰٓؤُلَآءِ تَقْتُلُونَ أَنفُسَكُمْ وَتُخْرِجُونَ فَرِيقًا مِّنكُم مِّن دِيَـٰرِهِمْ تَظَـٰهَرُونَ عَلَيْهِم بِٱلْإِثْمِ وَٱلْعُدْوَٰنِ وَإِن يَأْتُوكُمْ أُسَـٰرَىٰ تُفَـٰدُوهُمْ وَهُوَ مُحَرَّمٌ عَلَيْكُمْ إِخْرَاجُهُمْ ۚ أَفَتُؤْمِنُونَ بِبَعْضِ ٱلْكِتَـٰبِ وَتَكْفُرُونَ بِبَعْضٍ ۚ فَمَا جَزَآءُ مَن يَفْعَلُ ذَٰلِكَ مِنكُمْ إِلَّا خِزْىٌ فِى ٱلْحَيَوٰةِ ٱلدُّنْيَا ۖ وَيَوْمَ ٱلْقِيَـٰمَةِ يُرَدُّونَ إِلَىٰٓ أَشَدِّ ٱلْعَذَابِ ۗ وَمَا ٱللَّهُ بِغَـٰفِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ
Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauwana, na mnawatoa baadhi yenu majumbani mwao, mkisaidiana (na adui zao) dhidi yao kwa dhambi na uadui. Na wakikujieni wakiwa mateka, mnawakomboa, na hali mlikatazwa kuwatoa. Je, mnaamini baadhi ya Kitabu na mnamkufuru baadhi yake? Basi ni yapi malipo ya mwenye kutenda hayo miongoni mwenu ila aibu katika maisha ya duniani, na Siku ya Kiyama watapelekwa kwenye adhabu kali kabisa. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika mbali na yale mnayoyatenda.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauwana, na mnawatoa baadhi yenu majumbani kwao, mkisaidiana kwa dhambi na uadui. Na wakikujieni mateka mnawakomboa, na hali kuwatoa mmekatazwa. Je! Mnaamini baadhi ya Kitabu na mnakataa baadhi yake? Basi hana malipo mwenye kutenda hayo miongoni mwenu ila hizaya katika maisha ya duniani, na Siku ya Kiyama watapelekwa kwenye adhabu kali kabisa. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale mnayo yatenda. [85]
[85] Nanyi wenyewe kwa wenyewe mnauwana, na mnatoana majumbani, nyinyi kwa nyinyi: hawa wanawauwa hawa na hawa wanawauwa hawa; hawa wanawafukuza hawa majumbani mwao na hawa wanawafukuza hawa. Na huku mkisaidiana katika vitendo vya dhambi na uadui. Baada ya hayo wakitokea baadhi yenu wakatekwa na hao mnao shirikiana nao mnajishughulisha kwenda kuwakomboa hao mateka. Mkiulizwa nini kilicho kupelekeeni kuwakomboa, mnajibu kuwa vitabu vyenu vinakuamrisheni kukomboa mateka wa Kiyahudi. Jee, vitabu hivyo havikukuamrisheni msimwage damu ya ndugu zenu? Havikukuamrisheni msiwatoe watu majumbani mwao? Hivyo nyinyi mnat'ii sehemu ya yaliyo kujieni katika Kitabu na mnayakataa mengineyo? Basi jaza ya mwenye kutenda hayo katika nyinyi si lolote ila kupata hizaya katika maisha ya duniani, na Siku ya Kiyama. Mwenyezi Mungu, anaye vijua vyema vitendo vyao na siri zao, atawapeleka kwenye adhabu iliyo kali kabisa. Kabla ya Uislamu zilikuwapo katika mji wa Madina kabila mbili za Kiarabu ambazo zilikuwa na uadui baina yao, nazo ni Aus na Khazraj. Na pia zilikuwako kabila za Kiyahudi nazo ni Banu Quraidha na Banu Nnadhir. Banu Quraidha walifungamana na Aus, na Banu Nnadhir walifungamana na Khazraj. Ilikuwa kabila mbili za Kiarabu zikipigana, zile kabila za Kiyahudi nazo huingia vitani, kila kabila upande wa rafiki zake, na zikiuwana na wenzao wa dini moja nao, na wakifukuzana makwao. Lakini kila moja katika kabila mbili hizo za Kiyahudi zikishughulika baadaye kuwakomboa mateka walio tekwa na rafiki zao wa Kiarabu. Wakiulizwa kwa nini mnawakomboa na hao walikuwa wakipigana nanyi upande wa maadui zenu? Wao wakisema: Mwenyezi Mungu ametuamrisha katika Taurati tuwakomboe mateka wa Kiyahudi. Na wanajifanya hawajui kama Mwenyezi Mungu amewaamrisha vile vile wasiuwane wala wasitoane majumbani mwao. Kwa hivyo ndio wanaamini sehemu ya Kitabu na wanaikataa nyengine.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauana, baadhi yenu wanawaua wengine, na baadhi yenu wanawatoa wengine majumbani mwao; na kila kundi kati yenu linajitafutia nguvu kwa maadui dhidi ya ndugu zake kwa njia ya udhalimu na uonevu. Na mkijiwa nao, hao ndugu zenu, ni mateka kwenye mikono ya maadui, mnafanya haraka kuwakomboa kwa kulipa fidia, pamoja na kuwa imeharamishwa kwenu kuwatoa majumbani mwao. Ni ubaya ulioje mnaoufanya wa kuziamini baadhi ya hukumu za Taurati na kuzikanusha nyingine! Basi Malipo ya wanaoyafanya hayo si mengine ila ni unyonge na fedheha ulimwenguni, na Siku ya Kiyama watapelekwa kwenye adhabu kali sana ndani ya Moto. Na Allah Mtukufu si Mwenye kughafilika kwa mnayoyafanya.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net