Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 282

Al-Baqara 2:282

البقرة

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓا۟ إِذَا تَدَايَنتُم بِدَيْنٍ إِلَىٰٓ أَجَلٍ مُّسَمًّى فَٱكْتُبُوهُ ۚ وَلْيَكْتُب بَّيْنَكُمْ كَاتِبٌۢ بِٱلْعَدْلِ ۚ وَلَا يَأْبَ كَاتِبٌ أَن يَكْتُبَ كَمَا عَلَّمَهُ ٱللَّهُ ۚ فَلْيَكْتُبْ وَلْيُمْلِلِ ٱلَّذِى عَلَيْهِ ٱلْحَقُّ وَلْيَتَّقِ ٱللَّهَ رَبَّهُۥ وَلَا يَبْخَسْ مِنْهُ شَيْـًٔا ۚ فَإِن كَانَ ٱلَّذِى عَلَيْهِ ٱلْحَقُّ سَفِيهًا أَوْ ضَعِيفًا أَوْ لَا يَسْتَطِيعُ أَن يُمِلَّ هُوَ فَلْيُمْلِلْ وَلِيُّهُۥ بِٱلْعَدْلِ ۚ وَٱسْتَشْهِدُوا۟ شَهِيدَيْنِ مِن رِّجَالِكُمْ ۖ فَإِن لَّمْ يَكُونَا رَجُلَيْنِ فَرَجُلٌ وَٱمْرَأَتَانِ مِمَّن تَرْضَوْنَ مِنَ ٱلشُّهَدَآءِ أَن تَضِلَّ إِحْدَىٰهُمَا فَتُذَكِّرَ إِحْدَىٰهُمَا ٱلْأُخْرَىٰ ۚ وَلَا يَأْبَ ٱلشُّهَدَآءُ إِذَا مَا دُعُوا۟ ۚ وَلَا تَسْـَٔمُوٓا۟ أَن تَكْتُبُوهُ صَغِيرًا أَوْ كَبِيرًا إِلَىٰٓ أَجَلِهِۦ ۚ ذَٰلِكُمْ أَقْسَطُ عِندَ ٱللَّهِ وَأَقْوَمُ لِلشَّهَـٰدَةِ وَأَدْنَىٰٓ أَلَّا تَرْتَابُوٓا۟ ۖ إِلَّآ أَن تَكُونَ تِجَـٰرَةً حَاضِرَةً تُدِيرُونَهَا بَيْنَكُمْ فَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَلَّا تَكْتُبُوهَا ۗ وَأَشْهِدُوٓا۟ إِذَا تَبَايَعْتُمْ ۚ وَلَا يُضَآرَّ كَاتِبٌ وَلَا شَهِيدٌ ۚ وَإِن تَفْعَلُوا۟ فَإِنَّهُۥ فُسُوقٌۢ بِكُمْ ۗ وَٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ ۖ وَيُعَلِّمُكُمُ ٱللَّهُ ۗ وَٱللَّهُ بِكُلِّ شَىْءٍ عَلِيمٌ

Maana

Enyi mlioamini! Mnapodaiana deni hadi muda maalumu, basi liandikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala mwandishi asikatae kuandika kama alivyomfunza Mwenyezi Mungu. Basi na aandike, na mwenye deni juu yake aandikishe; na amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi, wala asipunguze chochote ndani yake. Na ikiwa mwenye kudaiwa ni mtu aliye pumbaa au mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe mlinzi wake kwa uadilifu. Na washuhudisheni mashahidi wawili katika wanaume wenu. Na ikiwa wanaume wawili hawapo, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili katika wale mnaowaridhia miongoni mwa mashahidi. Ili ikiwa mmoja wao (wanawake hao) atapotea, basi mmoja wao amkumbushe huyo mwengine. Na mashahidi wasikatae pindi wanapoitwa. Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyo ya uadilifu zaidi kwa Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa zaidi kwa ushahidi, na ya chini zaidi ili msiwe na shaka. Isipokuwa ikiwa ni biashara ya mkono kwa mkono mnayoifanya baina yenu, basi hapo hakuna ubaya juu yenu msipoiandika. Lakini wekeni mashahidi mnapouziana. Wala asitiwe matatani mwandishi wala shahidi. Na mkifanya hivyo, basi hakika huko ni kupita mipaka mliko nako. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kila kitu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Enyi mlio amini! Mnapo kopeshana deni kwa muda ulio wekwa, basi andikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala mwandishi asikatae kuandika. Aandike kama alivyo mfunza Mwenyezi Mungu. Na mwenye deni juu yake aandikishe; naye amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala asipunguze chochote ndani yake. Na akiwa mwenye kudaiwa ni mtu aliye pumbaa au mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe mlinzi wake kwa uadilifu. Na mshuhudishe mashahidi wawili katika wanaume wenu. Ikiwa hapana wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili katika mnao waridhia kuwa mashahidi. Ili ikiwa mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwengine. Na mashahidi wasikatae waitwapo. Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyo haki zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa zaidi kwa ushahidi, na vyema zaidi ili msiwe na shaka. Ila ikiwa ni biashara ya mkono-kwa-mkono baina yenu, basi hapo si vibaya kwenu msipo iandika. Lakini mnapo uziana wekeni mashahidi. Wala asitiwe matatani mwandishi wala shahidi. Na mkifanya hivyo basi hakika hilo ni kosa kwenu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. [282]

[282] Enyi mlio amini! Mkikopeshana deni kwa muda, inatakikana huo muda ujuulikane. Nanyi muandikiane ili kuhifadhi haki na usitokee mzozo. Na lazima mwenye kuandika awe mtu muadilifu katika uandishi wake. Wala muandishi asikatae kuandika, kwani hivyo ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya ilimu aliyo mfunza naye alikuwa haijui. Basi aandike lile deni kwa mujibu anavyo kubali yule mwenye kukopa. Naye huyo mwenye kukopa amwogope Mola wake Mlezi, asipunguze hata chembe katika deni lilio juu yake. Pindi akiwa mwenye kukopa hawezi kujiendesha, wala hayawezi mambo vilivyo, au ni mnyonge kwa udogo au ugonjwa au ukongwe, au akawa hawezi kuandikisha kwa ajili ya ububu au uzito wa ulimi au kutojua lugha inayo andikiwa huo waraka, basi mlinzi wake wa kisharia au hakimu au aliye mkhiari yeye, awe ndiye naibu wake wa kutoa imla ya kuliandika hilo deni kwa uadilifu ulio timia. Na washuhudisheni deni hilo wanaume wawili miongoni mwenu. Ikiwa hawakupatikana wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili, washuhudie ili pindi mtu akirusha waweze kutoa ushahidi wao, na akisahau mmoja mwengine aweze kumkumbusha. Wala haijuzu kujizuia kutoa ushahidi pindi unapo takikana. Wala msipuuze kuandika kidogo na kikubwa maadamu ni deni la kulipwa baadae. Hivyo ndio uadilifu wa sharia ya Mwenyezi Mungu, na ndio kuwa na nguvu zaidi kuwa ni dalili ya ukweli wa ushahidi, na ndio vyema zaidi kuondoa shaka shaka baina yenu. Ila ikiwa jambo lenyewe ni biashara ya mkono-kwa-mkono mnayo uzuiana baina yenu, hapo si lazima kuandikiana, kwani hapana dharura ya hayo. Na inatakikana lakini katika kuuziana pawepo mashahidi ili kuepusha ugomvi. Na tahadharini asipate madhara yoyote mwenye kuandika au mwenye kushuhudia. Hayo itakuwa ni kutokana na ut'iifu wa Mwenyezi Mungu. Na mkhofuni Mwenyezi Mungu, na ogopeni heba yake katika anayo amrisha na anayo yakataza. Hivyo ndio nyoyo zenu zitalazimika kufuata insafu na uadilifu. Na Mwenyezi Mungu anakubainishieni haki zenu na waajibu ulio juu yenu. Naye ni Mjuzi wa kila kitu - vitendo vyenu na vinginevyo. Aya hii inahakikisha misingi ya kuthibitisha. Inahakikisha msingi wa kuandikiana. Hukumu haiwi kwa chini kuliko mashahidi wawili walio wanaume waadilifu, au mwanamume mmoja na wanawake wawili. Na imelazimika mwandishi awe muadilifu, na wawepo mashahidi panapo kuwapo mafungamano. Lakini hapana lazima ya mashahidi ikiwa mua'mala wenyewe wa papo kwa papo, nipe nikupe, mkono kwa mkono. Pia aya inahakikisha kuwa mtu aliye pumbaa, au hawezi kujiendeshea mambo yake mtu mwenyewe, au mnyonge dhaifu, basi lazima awe na mtu kuwa ni wakili wake wa kumtendea badala yake. Na pindi ikiwa ni safarini na hapana mtu wa kuandika, basi yatosha kutoa kitu kiwe rahani akamate mwenye kukopesha

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Enyi mliomuamini Allah Mtukufu na mkamfuata Mtume Wake Muhammad, rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie, mkiamiliana kwa mkopo mpaka muda maalumu, usajilini kwa maandishi ili kuhifadhi mali na kuondoa ugomvi. Na asimame kuandika mtu muaminifu mwenye kudhibiti. Na asilikatae hilo yule mtu aliyetunukiwa na Allah Mtukufu ujuzi wa uandishi. Na asimame mdaiwa kufanya imla ya deni iliyo juu yake. Na amuogope Mola wake na asipunguze chochote katika deni iliyo juu yake. Iwapo mdaiwa amezuiwa matumizi kwa ubadhirifu wake na utumiaji wake unaopita kiasi, au akawa ni mdogo au ni mwendawazimu, au hawezi kusema kwa ububu au kwa ulemavu wa kutoweza kusema kabisa, basi na asimamie shughuli ya kufanya imla msimamizi wa mdaiwa kwa niaba yake. Na takeni ushahidi wa Waislamu wawili wanaume, waliobaleghe, wenye akili na waadilifu. Iwapo hawatopatikana wanaume wawili, takeni ushahidi wa mwanamume mmoja na wanawake wawili mnaoridhika na ushahidi wao, ili akisahau mmoja wao (hao wanawake wawili) yule mwengine amkumbushe. Na ni juu ya mashahidi kukubali mwito wa mwenye kuwaita kutoa ushahidi. Na ni juu yao kutoa ushahidi wao wakitakiwa kufanya hivyo. Na msichoke kuisajili deni, iwe ni kubwa au ni ndogo, mpaka wakati wake maalumu wa kulipa. Kwani hilo ni la usawa zaidi katika Sheria ya Allah Mtukufu na uongofu Wake, na linasaidia sana kabisa katika kusimamisha ushahidi na kuutekeleza, na liko karibu zaidi na kuondoa shaka kuhusu deni yenyewe, kiasi chake na muda wake. Lakini, iwapo ni jambo la kuuza na kununua, kwa kuchukua bidhaa na kutoa thamani yake papo hapo, basi hakuna haja ya kusajili, na inapendekezwa kushuhudisha hilo ili kuepusha ugomvi na utesi. Na katika mambo ya lazima kwa shahidi na mwandishi ni kutekeleza ushahidi kwa njia zake na usajili kama Alivyoamrisha Allah Mtukufu. Na hafai kwa mwenye haki na kwa yule ambaye haki iko juu ya shingo yake kuwadhuru waandishi na mashahidi. Pia, haifai kwa waandishi na mashahidi kuwadhuru wanaohitajia uandishi wao na ushahidi wao. Na mkifanya mliyokatazwa, huko ni kutoka nje ya twaa ya Allah Mtukufu; na mwisho mbaya wa kitendo hiko utawafikia. Na muogopeni Allah Mtukufu katika maamrisho Yake yote aliyowaamrisha nayo na akawakataza nayo. Na Allah Mtukufu Anawajulisha yote yanayotengeneza ulimwengu wenu na Akhera yenu. Na Allah Mtukufu kwa kila jambo ni Mjuzi. Hakuna kitu chochote kinachofichika Kwake kuhusu mambo yenu, na Atawalipa kwa hayo.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net