Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 229

Al-Baqara 2:229

البقرة

ٱلطَّلَـٰقُ مَرَّتَانِ ۖ فَإِمْسَاكٌۢ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌۢ بِإِحْسَـٰنٍ ۗ وَلَا يَحِلُّ لَكُمْ أَن تَأْخُذُوا۟ مِمَّآ ءَاتَيْتُمُوهُنَّ شَيْـًٔا إِلَّآ أَن يَخَافَآ أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ ٱللَّهِ ۖ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ ٱللَّهِ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا فِيمَا ٱفْتَدَتْ بِهِۦ ۗ تِلْكَ حُدُودُ ٱللَّهِ فَلَا تَعْتَدُوهَا ۚ وَمَن يَتَعَدَّ حُدُودَ ٱللَّهِ فَأُو۟لَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلظَّـٰلِمُونَ

Maana

Talaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa uzuri. Wala si halali kwenu kuchukua chochote katika kile mlichowapa wake zenu, isipokuwa ikiwa wote wawili watahofia ya kwamba hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkihofia kuwa hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu, hapo hakuna ubaya juu yao katika kile ambacho mke atajikomboa kwacho. Hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi msiikiuke. Na mwenye kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

T'alaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa vizuri. Wala si halali kwenu kuchukua chochote mlicho wapa wake zenu, ila ikiwa wote wawili wakiogopa ya kwamba hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkiogopa kuwa hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu hapo itakuwa hapana lawama ikiwa mwanamke atajikomboa. Hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu; basi msiikiuke. Na watakao ikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, hao ndio madhaalimu. [229]

[229] T'alaka ni mara mbili. Baada ya kila t'alaka ana haki mume kukaa naye kwa kumrejea kabla ya kwisha siku za eda, au kumrejesha katika dhamana yake kwa kumwoa upya. Na katika hali hiyo inapasa makusudio yake ni kukaa naye kwa uadilifu na kumtendea wema, au kuachana kwa ihsani na heshima bila ya kukhasimiana. Wala si halali kwenu, enyi waume, kuchukua chochote mlicho wapa wanawake ila mkikhofu kuwa hamtoweza kufuata haki za uke na ume alizo kubainishieni Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, na akaku lazimisheni mzifuate. Mkikhofu, enyi Waislamu, kutofuata haki za mume na mke vilivyo kama alivyo eleza Mwenyezi Mungu basi ameamrisha mke atoe mali kwa ajili ya kutokana na mumewe. Na hizi ni hukumu zilizo pitishwa, msiende kinyume nazo, mkazipindukia. Mwenye kufanya hivyo amejidhulumu nafsi yake na amedhulumu jamii anayo ishi kati yake. Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la ameifanyia sharia T'alaka, na akampa mwanamume kwanza uwezo wa kuacha. Baadhi ya watu wanadhani kuwa haya huleta madhara katika maisha na kusahilisha kuvunjika nyumba za watu. (a) Ama kupewa haki ya kuacha mwanamume kwa hakika hakupewa haki hiyo bila ya masharti yoyote. Katika masharti hayo aliyo wekewa ni: KWANZA hana ruhusa kuacha ila t'alaka moja ya kuweza kurejea, yaani anakuwa na haki ya kumrejea mke kabla ya kwisha eda. Ama amrejee naye yu ndani ya eda au amwache, na hivyo tena ni dalili ya hadi ya kuchukiana, na hapana maisha ya mume na mke tena kuchukiana kumefika hadi hiyo. PILI asimwache wakati wa hedhi, kwani wakati huo mwanamke huwa na hamaki, kwa hivyo huwa hapana utulivu. Na huenda hiyo hedhi ndiyo sababu ya hizo chuki zilizo zidi. Basi asiache mpaka mambo yawe yametua. TATU asimwache naye yumo katika t'ahara aliyo kwisha muingilia, kwani hiyo yaweza kuonekana huko kuchukiana kunatokana na kutokuwa na raghba na mkewe. Basi mambo yakiwa hivi t'alaka inakuwa katika hali ya chuki iliyo na nguvu, na kukatika mapenzi ya daima.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Talaka ambayo mtu anaweza kumrejea mke wake ni mara mbili, moja baada ya nyegine. Basi hukumu ya Allah Mtukufu, baada ya kila talaka, ni kumshikilia mwanamke kwa wema na tangamano zuri baada ya kumrejea au kumpa nafasi ya kwenda kwao pamoja na maelewano mema kwa kumtekelezea haki zake, na asimtaje mtalaka wake kwa uovu. Wala si halali kwenu, enyi Waumini, kuwapokonya chochote miongoni mwa vile mlivyowapa, kama mahari na vinginevyo. Isipokuwa wakiogopa waliooana kuwa hawataweza kutekeleza haki za unyumba, hapo mambo yao yatawekwa mbele ya mawalii. Na watakapochelea hao mawalii kuwa wanyumba wao hawataweza kutekeleza haki na mipaka ya Allah Mtukufu, hakuna kosa kwa waliooana katika kile atakacho kukitoa mwanamke kumpa mume kama ridhaa ya kupata talaka. Hukumu hizo ndiyo mipaka ya Allah Mtukufu, inayopambanua kati ya halali na haramu, basi msiikiuke. Na wenye kusubutu kuikeuka mipaka ya Allah Mtukufu, hao ndio madhalimu wa nafsi zao kwa kuzihatarisha adhabu ya Allah Mtukufu.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net