Al-Baqara 2:184
البقرةأَيَّامًا مَّعْدُودَٰتٍ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ وَعَلَى ٱلَّذِينَ يُطِيقُونَهُۥ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ ۖ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُۥ ۚ وَأَن تَصُومُوا۟ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ
(Mfunge) siku zenye kuhesabika. Na atakayekuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini, basi atimize hesabu katika siku nyingine. Na wale wasioweza, watoe fidia kwa kumlisha masikini. Na atakayefanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga saumu, ndiyo bora kwenu, ikiwa mnajua.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
(Mfunge) siku maalumu za kuhisabika. Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine. Na wale wasio weza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. Na atakaye fanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu, kama mnajua. [184]
[184] Mmeamrishwa mfunge siku chache za kuhisabika, na lau Mwenyezi Mungu angependa angeli kufanyieni muda mrefu. Wala hatukulazimisheni katika Saumu jambo msilo liweza. Aliye mgonjwa wa maradhi yanayo dhuriana na kufunga, au aliomo safarini, basi anaweza kula na alipe akisha pona au akirejea safarini. Ama asiyekuwa mgonjwa wala si msafiri, lakini hawezi kufunga ila kwa taabu kwa sababu ya udhuru kama ukongwe, na maradhi yasiyo tarajiwa kupona, yeye pia anaweza kula, na juu yake amlishe masikini ambaye hamiliki hata chakula cha siku moja yake. Na mwenye kujitolea kwa ridha yake kufunga zaidi kuliko faradhi itakuwa ni bora zaidi kwake. Kwani Saumu daima ni bora kwa mwenye kujua ukweli wa ibada.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Amewafaradhia Allah Mtukufu kufunga siku zinazojulikana idadi yake, nazo ni siku za mwezi wa Ramadhani. Basi yule kati yenu atakuwa mgonjwa, ikawa ni uzito kwake kufunga, au akawa ni msafiri, basi aweza kufungua. Na itamlazimu kufunga idadi ya siku nyengine zinazolingana na idadi ya siku alizokula. Na ni juu ya wale ambao kwao ni vigumu kufunga na ikawa inawaelemea maelemeo yasiyochukulika, kama mzee mkongwe na mngonjwa asiyetarajiwa kupoa, watoe fidia ya kila siku ambayo watafungua, nayo ni kulisha masikini. Na yule atakayezidisha katika kiwango cha fidia, kwa hiyari yake, basi hilo ni bora kwake. Na kufunga kwenu ni bora kwenu, pamoja na kuhimili shida, kuliko kutoa fidia, iwapo mnazijua fadhila kubwa zipatikanazo kwenye kufunga mbele ya Allah Mtukufu.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net