Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 158

Al-Baqara 2:158

البقرة

إِنَّ ٱلصَّفَا وَٱلْمَرْوَةَ مِن شَعَآئِرِ ٱللَّهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ ٱلْبَيْتَ أَوِ ٱعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا ۚ وَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَإِنَّ ٱللَّهَ شَاكِرٌ عَلِيمٌ

Maana

Hakika, vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za Mwenyezi Mungu. Basi, anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akafanya Umra, si kosa kwake kuzunguka kati yake. Na anayejitolea kutenda heri, basi bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye shukrani na Mwenye kujua hilo mno.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Hakika vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za Mwenyezi Mungu. Basi anaye hiji kwenye Nyumba hiyo au akafanya Umra, si kosa kwake kuvizunguka. Na anaye jitendea mwenyewe kheri basi bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye shukrani na Mjuzi. [158]

[158] Na kama alivyo kuwa Mwenyezi Mungu ametukuza hadhi ya Alkaaba akaifanya iwe ndiyo Kibla cha Swala, hali kadhaalika ametukuza shani ya vilima viwili viliopo Makka, navyo ni Safaa na Marwa, akavifanya miongoni mwa mahala pa kufanyia ibada ya Hijja. Basi imewajibikia baada ya kuizunguka Alkaaba kwa kut'ufu, kwenda huku na huku baina ya vilima viwili hivyo mara saba. Kwenda huko kunaitwa Sa'yu. Na baadhi yenu labda walikuwa wakiona vibaya kufanya hivyo kwa kuwa kilikuwa kitendo cha siku za jahiliya kabla ya kuja Uislamu. Lakini kweli iliopo ni kuwa hiyo ni ada ya Kiislamu ya tangu zamani. Basi hapana ubaya wowote kufanya Sa'yu baina ya vilima viwili hivi kwa mwenye kunuwiya Hijja na Umra. Na Muumini na afanye jambo la kheri kama awezavyo, kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa ayatendayo, na Yeye atamlipa kwa a'mali yake.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Hakika Swafa na Marwa, nayo ni majabali mawili madogo karibu ya Alkaba upande wa Mashariki, ni miongoni mwa alama za dini ya Allah Mtukufu zilizo wazi ambazo Allah Mtukufu Amezifanya ni sehemu za ibada kwa waja Wake kusai baina yake. Hivyo basi, yoyote mwenye kuikusudia Alkaba kwa kuhiji au kufanya Umra, si dhambi kwake kusai baina ya hayo majabali mawili, bali ni wajibu kwake kufanya hivyo. Na yule mwenye kufanya mambo ya kutii amri, kwa hiyari yake, hali ya kumtakasia Allah Mtukufu, hakika Allah Mtukufu ni Mwenye kushukuru, Analipa juu ya kichache kwa kingi, ni Mwenye kuzijua amali za waja Wake: Hazipotezi wala Hampunji yoyote chochote hata kama ni uzito wa chungu mdogo.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net