Al-Baqara 2:102
البقرةوَٱتَّبَعُوا۟ مَا تَتْلُوا۟ ٱلشَّيَـٰطِينُ عَلَىٰ مُلْكِ سُلَيْمَـٰنَ ۖ وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَـٰنُ وَلَـٰكِنَّ ٱلشَّيَـٰطِينَ كَفَرُوا۟ يُعَلِّمُونَ ٱلنَّاسَ ٱلسِّحْرَ وَمَآ أُنزِلَ عَلَى ٱلْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَـٰرُوتَ وَمَـٰرُوتَ ۚ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَآ إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ ۖ فَيَتَعَلَّمُونَ مِنْهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِۦ بَيْنَ ٱلْمَرْءِ وَزَوْجِهِۦ ۚ وَمَا هُم بِضَآرِّينَ بِهِۦ مِنْ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذْنِ ٱللَّهِ ۚ وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ ۚ وَلَقَدْ عَلِمُوا۟ لَمَنِ ٱشْتَرَىٰهُ مَا لَهُۥ فِى ٱلْـَٔاخِرَةِ مِنْ خَلَـٰقٍ ۚ وَلَبِئْسَ مَا شَرَوْا۟ بِهِۦٓ أَنفُسَهُمْ ۚ لَوْ كَانُوا۟ يَعْلَمُونَ
Na wakafuata yale waliyosoma mashetani katika ufalme wa Suleiman. Na wala Suleiman hakukufuru, bali mashetani ndio waliokufuru, wakiwafundisha watu uchawi, na yaliyoteremshwa kwa wale Malaika wawili, Haarut na Maarut huko Baabil. Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie: 'Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru.' Wakajifunza kwa hao wawili yale ya kumtenganisha mtu na mkewe. Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa kutaka kwa Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza yenye kuwadhuru wala hayawanufaishi. Na hakika, walikwishajua kwamba mwenye kuununua (uchawi), hatakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na hakika ni kiovu mno walichouza kwacho nafsi zao, laiti wangelikuwa wanajua.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na wakafuata yale waliyo zua mashet'ani kuuzulia ufalme wa Su leiman. Na wala Suleiman hakukufuru, bali mashet'ani ndio walio kufuru, wakiwafundisha watu uchawi, na yaliyo teremshwa kwa Malaika wawili, Haaruta na Maaruta katika Baabil. Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie: Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru. Wakajifunza kwa hao wawili yale ya kumfarikisha mtu na mkewe. Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa kutaka Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza yatayo wadhuru wala hayawanufaishi. Na hakika wanajua kwamba aliye khiari haya hatakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na hakika ni kiovu mno walicho jiuzia nafsi zao laiti wangelijua. [102]
[102] Na wao hakika waliyasadiki waliyo yazua mashetani wao na wapotovu wao juu ya ufalme wa Suleiman, walipo dai kuwa Suleiman hakuwa Nabii wala si Mtume aliye teremshiwa ufunuo (Wahyi) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bali alikuwa ni mchawi tu anaye tegemea msaada wa uchawi wake. Na kwamba ni uchawi wake huu ndio ulio mjengea ufalme wake na ukamwezesha aweze kuwatawala majini, na ndege, na upepo. Kwa hivyo walimsingizia ukafiri Suleiman, na hali Suleiman hakukufuru, lakini hao mashetani waovu ndio walio kufuru. Wao ndio walio zua uzushi huu, wakaingia kuwafunza watu uchawi wao na walio pokea katika mabaki yaliyo teremka katika Baabil (Babilonia) kwa Malaika wawili, Haaruta na Maaruta. Na hawa Malaika wawili hawakuwa wakimfundisha mtu yeyote mpaka wamwambie: Sisi ni mtihani uwe ni majaribio kwenu, tunakufundisha mafunzo ambayo yanaweza kuleta fitna na ukafiri, basi jifunze lakini tahadhari usiitumie ilimu hii. Na lakini watu hawakunasihika kwa nasiha hii, na wakatumia hayo waliyo jifunza kwa hao Malaika wawili ya kumgombanisha mtu na mkewe. Naam, hawa mashetani waovu wamekufuru walipo zua katika uzushi wao na hadithi zao za uwongo wakafanya hayo ndio wasila na udhuru wa kuwafundishia Mayahudi uchawi. Na wao hao wachawi hawawezi kumdhuru yeyote, lakini Mwenyezi Mungu ndiye Yeye anayeweza kumletea mtu madhara pindi akipenda. Na hayo ya uchawi wao yanawadhuru hao wanao jifunza katika dini yao na dunia yao, na wala hawapati faida yoyote. Na wao wanajua kweli ya kujua ya kwamba anaye elekea upande huu hana sehemu yoyote katika neema za Akhera. Na kama wamebakia na ujuzi wowote yafaa wajue kuwa haya waliyo yakhiari kwa ajili ya nafsi zao ni hadi ya kuwa maovu.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na Mayahudi walifuata yale ambayo mashetani walikuwa wanawasimulia wachawi katika kipindi cha ufalme wa Sulaimān mwana wa Dāwūd. Na Sulaymān hakukufuru na wala hakujifundisha uchawi. Lakini mashetani ndio walimkanusha Allah Mtukufu kwa kuwafundisha watu uchawi, kwa kuwaharibia dini yao. Mayahudi pia waliufuata uchawi ulioshushwa kwa malaika wawili: Hãrũt na Mãrũt, katika ardhi ya Bābil ilyoko Iraq, ukiwa ni mtihani na majaribio kutoka kwa Allah Mtukufu kwa waja Wake. Na hao Malaika wawili hawakuwa wakimfunza yoyote mpaka wamnasihi na kumuonya asijifunze uchawi na kumwambia, “Usikufuru kwa kujifunza uchawi na kuwatii mashetani.” Basi watu walikuwa wakijifunza kutoka kwa Malaika wawili vitu vinavyozusha chuki baina ya mume na mke mpaka wakafarikana. Na wachawi hawana uwezo wa kumdhuru, kwa uchawi wao, yoyote isipokuwa kwa idhini ya Allah Mtukufu na hukumu Yake. Na wachawi hawajifunzi ila shari yenye kuwadhuru na kutowapa nafuu. Mashetani waliupeleka uchawi kwa Mayahudi, ukaenea kwao mpaka wakaufadhilisha juu ya Kitabu cha Allah Mtukufu. Na Mayahudi walijua kwamba mwenye kuchagua uchawi na kuacha haki, hatakuwa na fungu lolote la kheri huko Akhera. Ni ubaya ulioje uchawi na ukafiri waliojichagulia nafsi zao kuwa ni badala ya Imani na kumfuata Mtume, lau wangekuwa na elimu yenye kuzalisha vitendo vya kufuata mawaidha wapewayo!
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net