Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 10 · Aya ya 22

Yunus 10:22

يونس

هُوَ ٱلَّذِى يُسَيِّرُكُمْ فِى ٱلْبَرِّ وَٱلْبَحْرِ ۖ حَتَّىٰٓ إِذَا كُنتُمْ فِى ٱلْفُلْكِ وَجَرَيْنَ بِهِم بِرِيحٍ طَيِّبَةٍ وَفَرِحُوا۟ بِهَا جَآءَتْهَا رِيحٌ عَاصِفٌ وَجَآءَهُمُ ٱلْمَوْجُ مِن كُلِّ مَكَانٍ وَظَنُّوٓا۟ أَنَّهُمْ أُحِيطَ بِهِمْ ۙ دَعَوُا۟ ٱللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ ٱلدِّينَ لَئِنْ أَنجَيْتَنَا مِنْ هَـٰذِهِۦ لَنَكُونَنَّ مِنَ ٱلشَّـٰكِرِينَ

Maana

Yeye ndiye anayewaendesha katika nchi kavu na baharini. Mpaka mnapokuwa katika majahazi na yakawa yanakwenda nao kwa upepo mzuri na wakaufurahia, upepo mkali ukayajia, na yakawajia mawimbi kutokea kila mahali, na wakaona kwamba wameshazingirwa, basi hapo wanamwomba Mwenyezi Mungu kwa kumpwekeshea yeye tu dini, “Ukituokoa kutokana na haya, bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.”

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Yeye ndiye anaye kuendesheni bara na baharini. Hata mnapo kuwa majahazini na yakawa yanakwenda nao kwa upepo mzuri wakaufurahia, upepo mkali ukawazukia, na yakawajia mawimbi kutoka kila upande, na wakaona wameshazongwa, basi hapo humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia niya: Ukituokoa na haya bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa wanao shukuru. [22]

[22] Mwenyezi Mungu mnaye ikufuru neema yake, na mnakanusha Ishara zake, ndiye Yeye anaye kuezesheni kwenda na kutembea nchi kavu kwa miguu au kwa vipando, na baharini kwa vyombo alivyo fanya vikutumikieni, vinavyo kwenda juu ya maji, kama anavyo visahilishia Mwenyezi Mungu kwa upepo mzuri unao puliza kwa amani mpaka kufikilia huko vyendako. Hata mkisha tumaini na mkafurahia huvuma tena upepo mkali ukatibua mawimbi kutoka kila upande, na mkayakinika kuwa hapana ila kuhiliki tu! Katika shida kama hii hamna tegemeo ila Mwenyezi Mungu. Hapo basi mnamwomba madua kwa usafi wa niya, kwa kuyakinika kuwa hapana mwokozi isipo kuwa Yeye, na mnampa ahadi kuwa pindi akikuvueni na balaa hiyo mtamuamini, na mtakuwa wenye kushukuru.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Yeye Ndiye Anayewaendesha nyinyi, enyi watu, juu ya wanyama na vinginevyo barani, na ndani ya majahazi baharini, hata mnapokuwa humo na yakatembea kwa upepo mzuri na abiria wa hayo majahazi wakafurahi kwa huo upepo mzuri, ghafla majahazi hayo yanajiwa na upepo mkali, na mawimbi yakawajia abiria kutoka kila mahali, na wakawa na hakika kuwa maangamivu yamewazunguka, hapo wanamtakasia dua Allah Mtukufu Peke Yake, na wakaviacha vile ambavyo walikuwa wakiviabudu na wanasema, «Ukituokoa kutoka kwenye shida hii ambayo tuko nayo, kwa kweli tutakuwa ni miongoni mwa wale wenye kukushukuru kwa neema yako».

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Yunus

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net