Anaeleza bin Abbas -radhi za Allah ziwe juu yake- kuwa yeye alipokuwa kijana mdogo alikuwa kapanda pamoja na Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-, akasema kumwambia -Amani iwe juu yake-: Hakika mimi ninakufundisha vitu na mambo ambayo Mwenyezi Mungu atakunufaisha kwayo: Muhifadhi Mwenyezi Mungu kwa kuhifadhi maamrisho yake na kuepuka makatazo yake, kiasi kwamba akukute katika utiifu na yale yenye kukuweka karibu naye, na asikukute katika maasi na madhambi, ikiwa utafanya hivyo basi malipo yako yatakuwa ni Mwenyezi Mungu kukuhifadhi kutokana na kero za Dunia na Akhera, na atakunusuru katika mambo yako magumu mahala popote utakapoelekea. Na ukitaka kuomba jambo, basi usimuombe ila Mwenyezi Mungu kwani Yeye pekee ndiye mwenye kuwajibu waombaji. Na ukitaka msaada basi usiutake ila kwa Mwenyezi Mungu. Na uwe na yakini kuwa hutopata manufaa yoyote hata kama viumbe wote wa Ardhini watakusanyika ili kutaka kukunufaisha, isipokuwa kwa kile alichokiandika Mwenyezi Mungu kwako, na wala hutopata madhara hata kama viumbe wote wa Ardhini watakusanyika ili kutaka kukudhuru, isipokuwa kwa lile alilolikadiria Mwenyezi Mungu juu yako. Na kuwa jambo hili kashaliandika Mwenyezi Mungu Mtukufu na akalikadiria kulingana na namna hekima na elimu yake zilivyopelekea, na hakuna kubadilishwa yale aliyoyaandika Mwenyezi Mungu. Na kwamba atakayemuhifadhi Mwenyezi Mungu kwa kuhifadhi amri zake na kuyaepuka makatazo yake; basi Mwenyezi Mungu Mtukufu atakuwa mbele ya mja kwa kuyajua matatizo yatakayomfika na atamnusuru na kumpa msaada. Na kwamba mwanadamu atakapomtii Mwenyezi Mungu wakati wa raha basi Mwenyezi Mungu atamletea faraja na njia ya kutokea wakati wa shida, hivyo na aridhie kila mja na kile alichokikadiria Mwenyezi Mungu cha kheri na shari. Na kukiwa na matatizo na mitihani basi mja ashikamane na subira kwani subira ni ufunguo wa faraja, na kwamba mitihani ikizidi kuwa mingi ndio faraja huja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na kwamba uzito unapotokea Mwenyezi Mungu huufuatisha na wepesi.
- Umuhimu wa kuwafundisha vijana na watoto wadogo mambo ya dini kuanzia Tauhidi na adabu na mengineyo.
- Malipo huenda sawa na matendo.
- Amri ya kumtegemea Mwenyezi Mungu, na kutawakali kwake bila kumtegemea asiyekuwa yeye, na yeye ndiye msaidizi bora.
- Kuamini maamuzi na mipango ya Mwenyezi Mungu na kuridhika nayo, nakuwa Mwenyezi Mungu amekwisha kadiria kila kitu.
- Atakayetelekeza amri ya Mwenyezi Mungu basi Mwenyezi Mungu naye humtelekeza na humnyima ulinzi.
- Habari njema kubwa kwa mwanadamu kuwa pale unapompata uzito basi asubiri wepesi.
- Kuliwazwa mja pale inapotokea mitihani, na kuyakosa yale ayapendayo, kwa mujibu wa kauli yake: "Na tambua kuwa yaliyokufika hayakuwa ni yenye kukukosa, na yaliyokukosa hayakuwa ni yenye kukupata" Sentensi ya kwanza ni kuliwazwa wakati wa kufikwa na yenye kuchukiza, na ya pili ni katika kuyakosa yale yenye kupendeka.
سنن الترمذي (4/ 284) (2516). التحفة الربانية في شرح الأربعين حديثًا النووية (ص42). شرح الأربعين النووية، لابن عثيمين (ص200). فتح القوي المتين في شرح الأربعين وتتمة الخمسين، للعباد (ص69).