Al-Maaida
Hii ni tarjama ya tafsiri ya as-Saʿdī kama IslamHouse.com inavyoichapisha katika saadi.islamenc.com, iliyosomwa kutoka kurasa za tovuti hiyo. Tovuti haisemi ni nani aliyeitafsiri kwa lugha nyingine wala inafuata toleo gani lililochapishwa, na haitaji masharti ya kuchukua matini yake, kwa hiyo haki ya kuionyesha haijathibitishwa. Hakuna aliyeilinganisha na kitabu kilichochapishwa, na hakuna mwanazuoni aliyeihakiki. Kila kifungu kipo kando ya aya inazozifafanua, ambazo ni matini ya Qur’ani ya Tanzil, inavyoonekana huko; aya ambayo tovuti haitoi ufafanuzi wake yenyewe inakaa pamoja na kifungu kilichotangulia, na faharasa inataja kila aya ya aina hiyo. Sabīl haikuandika wala kutafsiri kwa lugha nyingine chochote kati yake.
Maandishi kutokasaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)ilichukuliwa 2026-10-22
يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ ٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ وَٱبْتَغُوٓا۟ إِلَيْهِ ٱلْوَسِيلَةَ وَجَـٰهِدُوا۟ فِى سَبِيلِهِۦ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ 35
{35} Hii ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa waja wake Waumini juu ya yale ambayo yanatakiwa na imani miongoni mwa kumcha Mwenyezi Mungu, na kutahadhari dhidi ya hasira yake na ghadhabu yake. Na hilo ni kwamba, mja ajitahidi na ajibidiishe kwa kiasi cha uwezo wake katika kujiepusha na yale ambayo Mwenyezi Mungu huyachukia miongoni mwa dhambi za moyoni, na ulimi, na viungo, za dhahiri na za ndani. Na atafute msaada wa Mwenyezi Mungu katika kuyaacha ili aokoke kwa hilo kutokana na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake. "Na tafuteni njia ya kumfikia," yaani, ukaribu Naye, na cheo Kwake, na kumpenda Yeye. Na hilo ni kwa kutekeleza wajibu zake za kimoyoni, kama vile kumpenda Yeye na kwa sababu yake, na kuhofu, na kutumaini, na kumrudia, na kumtegemea. Na za kimwili kama vile Zaka na Hijja, na zenye kukusanya mawili hayo kama vile Swala na mfano wake miongoni mwa aina nyinginezo za kisomo na ukumbusho. Na katika aina za ihsani kwa viumbe kwa mali, na elimu, na heshima, na mwili, na kuwanasihi waja wa Mwenyezi Mungu. Basi Matendo haya yote humleta mtu karibu na Mwenyezi Mungu mpaka ampende. Na mja haachi kujisongeza karibu na Mwenyezi Mungu kwa hayo hadi ampende. Na akimpenda, anakuwa masikio yake ambayo anasikia kwayo, na macho yake ambayo anatazama kwayo, na mkono wake ambao anakamata kwao, na mguu wake ambao anatembea kwao, na Mwenyezi Mungu anajibu dua yake. Kisha Yeye Mwingi wa baraka, Mtukufu akateua katika ibada zenye kumleta mtu karibu naye kama vile, jihadi katika njia Yake. Nayo ni kufanya juhudi katika kupigana na makafiri kwa mali, na nafsi, na rai na ulimi, na kujitahidi katika kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ambacho mja ana uwezo nacho. Kwa sababu aina hii ni katika utiifu mtukufu zaidi na yale yanye kusongeza karibu na Mwenyezi Mungu yaliyo bora zaidi. Na kwa sababu mwenye kufanya hayo, basi yeye anastahiki zaidi na anafaa zaidi kufanya yasiyokuwa hayo. "Ili mfaulu;" ikiwa mtamcha Mwenyezi Mungu kwa kuacha maasia, na mkatafuta njia ya kumfikia Mwenyezi Mungu kwa kumtii, na mkapigana katika njia yake kwa kutafuta radhi zake. Na kufaulu ni kufikia na kupata kila kitu kinachotafutwa, kinachotakwa, na kuokoka kutokana na kila kitu kinachohofiwa. Basi uhakika wake ni furaha ya milele na neema ya kudumu.