Ruka hadi kwenye maudhui
Tafsir As-Saadi - Swahili · An-Nisaa
Sura ya 4

An-Nisaa

Hii ni tarjama ya tafsiri ya as-Saʿdī kama IslamHouse.com inavyoichapisha katika saadi.islamenc.com, iliyosomwa kutoka kurasa za tovuti hiyo. Tovuti haisemi ni nani aliyeitafsiri kwa lugha nyingine wala inafuata toleo gani lililochapishwa, na haitaji masharti ya kuchukua matini yake, kwa hiyo haki ya kuionyesha haijathibitishwa. Hakuna aliyeilinganisha na kitabu kilichochapishwa, na hakuna mwanazuoni aliyeihakiki. Kila kifungu kipo kando ya aya inazozifafanua, ambazo ni matini ya Qur’ani ya Tanzil, inavyoonekana huko; aya ambayo tovuti haitoi ufafanuzi wake yenyewe inakaa pamoja na kifungu kilichotangulia, na faharasa inataja kila aya ya aina hiyo. Sabīl haikuandika wala kutafsiri kwa lugha nyingine chochote kati yake.

Maandishi kutokasaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)ilichukuliwa 2026-10-22

Aya ya 82

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ ٱلْقُرْءَانَ ۚ وَلَوْ كَانَ مِنْ عِندِ غَيْرِ ٱللَّهِ لَوَجَدُوا۟ فِيهِ ٱخْتِلَـٰفًا كَثِيرًا 82

{82} Yeye Mtukufu anaamrisha kukizingatia Kitabu chake. Nako ni kutafakari juu ya maana zake na kutazama kwa fikira ya ndani yake na katika misingi yake, na matokeo yake, na yanayofungamana na hayo. Kwani katika kukizingatia Kitabu cha Mwenyezi Mungu kuna ufunguo wa elimu na maarifa, na kwacho inatolewa kila heri, na zinatolewa ndani yake kila elimu, na kwayo imani inaongezeka moyoni, na mti wake unaimarika. Kwani kinamjulisha Mola Mlezi, na yale aliyo nayo miongoni mwa sifa za ukamilifu, na yale anayotakaswa kutokana nayo miongoni mwa sifa za upungufu. Na kinajulisha njia inayofikia kwake, na sifa za watu wake, na yale ambayo wanayo wakati watakapofika kwake. Na kinajulisha kuhusu adui ambaye ndiye adui wa hakika, na njia inayofikisha kwenye adhabu, na sifa za watu wake, na yale waliyo nayo wakati wa kuwepo kwa sababu za adhabu. Na kila mja anapozidisha kukitafakari, anaongezeka elimu, na matendo, na utambuzi. Ndiyo maana, Mwenyezi Mungu akaamuru hivyo, na akamhimiza juu yake, na akajulisha kuwa hicho ndicho kilichokusudiwa katika kuiteremsha Qur-ani. Kama alivyosema Yeye Mtukufu, “Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, ni chenye baraka, ili wazizingatie Aya zake, na wawe wa kukumbuka wenye akili.” Na akasema Yeye Mtukufu, “Je, hawaizingatii hii Qur-ani? Au kwenye nyoyo (zao) yako makufuli yake?” Na katika faida za kukizingatia Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni kwamba kwa kufanya hivyo mja hufikia daraja ya yakini na kujua kwamba ni maneno ya Mwenyezi Mungu. Kwa sababu, anaona kikisadikishana chenyewe kwa chenyewe, na kinaafikiana chenyewe kwa chenyewe. Basi utaona hekima, na visa, na habari zikirudiwa katika Qur-ani katika sehemu kadhaa, zote zinaafikiana na kusadikishana, na haikinzani yenyewe kwa yenyewe. Na kwa hilo, unajulikana ukamilifu wa Qur-ani, na kwamba inatoka kwa Yule ambaye elimu yake imezunguka kila kitu. Na ndiyo maana Yeye Mtukufu akasema, “Na lau kuwa ingetoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, bila ya shaka wangelikuta ndani yake hitilafu nyingi.” Yani kwa kuwa ilitoka kwa Mwenyezi Mungu, hapakuwa na hitilafu yoyote ndani yake hata kidogo.