Ruka hadi kwenye maudhui
Tafsir As-Saadi - Swahili · An-Nisaa
Sura ya 4

An-Nisaa

Hii ni tarjama ya tafsiri ya as-Saʿdī kama IslamHouse.com inavyoichapisha katika saadi.islamenc.com, iliyosomwa kutoka kurasa za tovuti hiyo. Tovuti haisemi ni nani aliyeitafsiri kwa lugha nyingine wala inafuata toleo gani lililochapishwa, na haitaji masharti ya kuchukua matini yake, kwa hiyo haki ya kuionyesha haijathibitishwa. Hakuna aliyeilinganisha na kitabu kilichochapishwa, na hakuna mwanazuoni aliyeihakiki. Kila kifungu kipo kando ya aya inazozifafanua, ambazo ni matini ya Qur’ani ya Tanzil, inavyoonekana huko; aya ambayo tovuti haitoi ufafanuzi wake yenyewe inakaa pamoja na kifungu kilichotangulia, na faharasa inataja kila aya ya aina hiyo. Sabīl haikuandika wala kutafsiri kwa lugha nyingine chochote kati yake.

Maandishi kutokasaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)ilichukuliwa 2026-10-22

Aya ya 113

وَلَوْلَا فَضْلُ ٱللَّهِ عَلَيْكَ وَرَحْمَتُهُۥ لَهَمَّت طَّآئِفَةٌ مِّنْهُمْ أَن يُضِلُّوكَ وَمَا يُضِلُّونَ إِلَّآ أَنفُسَهُمْ ۖ وَمَا يَضُرُّونَكَ مِن شَىْءٍ ۚ وَأَنزَلَ ٱللَّهُ عَلَيْكَ ٱلْكِتَـٰبَ وَٱلْحِكْمَةَ وَعَلَّمَكَ مَا لَمْ تَكُن تَعْلَمُ ۚ وَكَانَ فَضْلُ ٱللَّهِ عَلَيْكَ عَظِيمًا 113

{113} Kisha akataja neema yake kwa Mtume wake kwa kumhifadhi na kumlinda kutokana na aliyetaka kumpoteza, na akasema: “Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako na rehema yake, kundi moja kati yao lingedhamiria kukupoteza.“ Hakika, Aya hizi tukufu wametaja wafasiri kwamba sababu ya kuteremshwa kwake ni kuwa watu wa nyumba fulani waliiba huko Madina. Na walipojulikana kile walichoiba, wakahofia kufedheheshwa, na wakachukua vitu vyao vya wizi na wakavitupa ndani ya nyumba ya mtu ambaye hakuwa na hatia ya hilo. Na mwizi huyo akaomba msaada kwa watu wake ili waje kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu – rehema na amani ziwe juu yake - na wamuombe amwondolee rafiki yao hatia mbele ya watu. Wakasema: “Hakika, hakuiba, bali aliyeiba ni yule ambaye kile alichoiba kitapatikana ndani ya nyumba yake.” Naye ndiye yule ambaye hakuwa na hatia.” Kwa hivyo, Mtume wa Mwenyezi Mungu – rehema na amani ziwe juu yake – akaazimia kumtolea hatia mwenzao huyo. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu akateremsha aya hizi ili ziwe ukumbusho na ubainisho wa tukio hilo, na kumtahadharisha Mtume - rehema na amani zimshukie - dhidi ya kuwabishania wahaini. Kwa maana, kumbishania mwenye batili ni katika upotovu. Kwa kuwa, upotovu ni aina mbili: upotovu katika elimu, nao ni kutoijua haki, na upotovu katika vitendo, ambao ni kufanya kitu kisichokuwa kinachohitajika. Basi Mwenyezi Mungu akamhifadhi Mtume wake kutokana na aina hii ya upotofu kama vile alivyomhifadhi kutokana na upotovu katika vitendo. Na akajulisha kwamba vitimbi vyao na njama zao vinawarudia wao wenyewe, kama ilivyo hali ya kila mpanga njama, akasema: "Na hawapotezi isipokuwa nafsi zao;" wa sababu vitimbi hivyo na hila hiyo haikuwafanya kufikia lengo lao lililokusudiwa, na hawakupata isipokuwa kuambulia patupu na kunyimwa, na dhambi na hasara. Na hii ni neema kubwa juu ya Mtume wake – rehema na amani ziwe juu yake - ambayo inajumuisha neema ya matendo, nayo ni kuwezesha kufanya yaliyo ya faradhi na kumkinga dhidi ya kila jambo lililoharamishwa. Kisha akatajia neema yake ya elimu juu yake. Akasema, "Na Mwenyezi Mungu amekuteremshia Kitabu na hekima;" yani amekuteremshia Qur-ani hii tukufu na ukumbusho wenye hekima, ambao ndani yake kuna ubainisho wa kila kitu, elimu ya kwanza na ya mwisho. Na hekima ima ni Sunna ambayo baadhi ya watu wema waliotangulia walisema: Sunnah inateremshwa kwake kama inavyoteremshwa Qur-ani. Au ni kujua siri za Sheria zinazozidi kujua hukumu zake, na kuweka mambo mahali pake, na kupanga kila kitu kulingana nacho. "Na akakufundisha yale uliyokuwa huyajui." Na hili linajumuisha yote aliyoyafundisha Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwani yeye - Swalah na salamu zimshukie - kama vile Mwenyezi Mungu alivyomueleza kabla ya unabii wake, kwa kauli yake. "Hukuwa unajua ni nini Kitabu, wala Imani." "Na akakukuta umepotea akakuongoa?" Kisha Mwenyezi Mungu hakuacha kuendelea kumfunulia wahyi, na kumfundisha, na kumkamilisha mpaka akapanda daraja la elimu ambalo haliwezekani kwa watu wa kwanza na wa mwisho kulifikia. Kwa hivyo akawa ndiye mwenye elimu zaidi wa viumbe vyote, na mwenye kujumuisha zaidi yao wa sifa za ukamilifu, na mkamilifu wao zaidi. Na ndiyo maana akasema: "Na fadhila za Mwenyezi Mungu zilizo juu yako ni kubwa." Basi neema yake juu ya Mtume Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake - ni kubwa zaidi kuliko neema yake juu ya viumbe vyote, na aina za fadhila ambazo Mwenyezi Mungu amemfadhilisha kwazo hawezi kuzifuatilia zote, wala kuzihesabu kwa urahisi.