An-Nisaa
Hii ni tarjama ya tafsiri ya as-Saʿdī kama IslamHouse.com inavyoichapisha katika saadi.islamenc.com, iliyosomwa kutoka kurasa za tovuti hiyo. Tovuti haisemi ni nani aliyeitafsiri kwa lugha nyingine wala inafuata toleo gani lililochapishwa, na haitaji masharti ya kuchukua matini yake, kwa hiyo haki ya kuionyesha haijathibitishwa. Hakuna aliyeilinganisha na kitabu kilichochapishwa, na hakuna mwanazuoni aliyeihakiki. Kila kifungu kipo kando ya aya inazozifafanua, ambazo ni matini ya Qur’ani ya Tanzil, inavyoonekana huko; aya ambayo tovuti haitoi ufafanuzi wake yenyewe inakaa pamoja na kifungu kilichotangulia, na faharasa inataja kila aya ya aina hiyo. Sabīl haikuandika wala kutafsiri kwa lugha nyingine chochote kati yake.
Maandishi kutokasaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)ilichukuliwa 2026-10-22
وَمَن يُهَاجِرْ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ يَجِدْ فِى ٱلْأَرْضِ مُرَٰغَمًا كَثِيرًا وَسَعَةً ۚ وَمَن يَخْرُجْ مِنۢ بَيْتِهِۦ مُهَاجِرًا إِلَى ٱللَّهِ وَرَسُولِهِۦ ثُمَّ يُدْرِكْهُ ٱلْمَوْتُ فَقَدْ وَقَعَ أَجْرُهُۥ عَلَى ٱللَّهِ ۗ وَكَانَ ٱللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا 100
{100} Haya ni katika kueleza kuhimiza na kutia moyo juu ya kuhama na kueleza yale yaliyo ndani yake ya masilahi. Basi Mkweli aliahidi katika ahadi yake kwamba, mwenye kuhama katika njia yake kwa kutafuta radhi zake kwamba atapata pengi pa kukimbilia katika ardhi na wasaa. Basi ‘mahali pengi pa kukimbilia’ linajumuisha masilahi ya kidini, na ‘wasaa’ linajumuisha masilahi ya kidunia. Na hili ni kwa sababu wengi katika watu hufikiri kwamba katika kuhama kuna kutengana baada ya kuwa pamoja, na umaskini baada ya kuwa na mali, na unyonge baada ya kuwa na utukufu, na ugumu baada ya kuwa na wepesi, lakini hilo sivyo hivyo. Kwa maana, Muumini maadamu yuko katika washirikina, basi Dini yake ina upungufu mkubwa; si katika ibada zinazomhusu yeye tu, kama vile swala na mfano wake, wala katika ibada zinazovuka mipaka, kama vile jihadi kwa kauli na vitendo na yanayofuatana na hayo. Kwa sababu hawezi kufanya hivyo, na anakaribia kufitiniwa kutoka katika dini yake, hasa akiwa amedhoofishwa. Basi akihama katika njia ya Mwenyezi Mungu, ataweza kusimamisha dini ya Mwenyezi Mungu na kupigana jihadi na maadui wa Mwenyezi Mungu na kuwashambulia. Kwa sababu Al-Muraaghama ni neno lenye kujumuisha kila kitu kinachosababisha hasira kwa maadui wa Mwenyezi Mungu kwa maneno na vitendo, na pia atapata wasaa katika riziki yake, na tayari hilo lilitokea kama alivyojulisha Yeye Mtukufu. Basi zingatia hilo kwa maswahaba, Mwenyezi Mungu awe radhi nao. Wao walipohama katika njia ya Mwenyezi Mungu na wakaacha makazi yao, na watoto wao, na mali zao kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, imani yao ikakamilika kwa hilo. Na wakapata imani timilifu, na jihadi kubwa, na nusura kwa Dini ya Mwenyezi Mungu, hata wakawa kwa sababu ya hilo maimamu wa waliokuja baada yao. Na vile vile walipata yale yanayotokana na hilo kama vile ushindi, na ngawira na wakawa kwayo matajiri zaidi ya watu wote. Na vivyo hivyo, kila mwenye kufanya yale waliyoyafanya, basi atapata yale waliyoyapata mpaka Siku ya Qiyama. Kisha akasema, “Na mwenye kutoka katika nyumba yake akihamia kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.” Yani akimkusudia Mola wake Mlezi, na radhi zake, na mapenzi yake kwa Mtume wake, na kuinusuru Dini ya Mwenyezi Mungu, na si kwa makusudio mengine. “Kisha yakamfika mauti” kwa kuuawa au kinginecho, “basi hakika umekwisha wajibika ujira kwa Mwenyezi Mungu.” Yani ameshapata ujira wa mhamiaji aliyefikia lengo lake kwa dhamana ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hilo ni kwa sababu alikusudia na akaazimia, na akaanzisha na kulitenda hilo. Na katika rehema ya Mwenyezi Mungu juu yake na wengine mfano wake ni kwamba aliwapa ujira wao kamili, hata kama hawakumaliza matendo, na akawafutia yale waliyoyafanya ya mapungufu katika kuhama na mengineyo. Na ndiyo maana akahitimisha Aya hii kwa majina haya mawili matukufu. Akasema, “Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.” Anawafutia Waumini yale makosa waliyoyafanya, hasa wale waliotubia na wakarejea kwa Mola wao Mlezi. Ni Mwenye kurehemu viumbe vyote kwa rehema ya kuwaumba, na kuwaweka salama, na kuwaruzuku mali, na watoto, na nguvu na mengineyo. Ni Mwenye kuwarehemu Waumini, ambapo aliwawezesha kuamini, na akawafunza katika elimu ambayo kwayo wanapata yakini, na akawarahisishia njia za furaha na kufaulu, na ambayo kwayo wanapata faida kubwa zaidi, na wataona katika rehema yake na ukarimu wake yale ambayo jicho halijawahi kuona, wala sikio halijawahi kusikia, wala halijawahi kupita katika moyo wa mwanadamu yeyote. Kwa hivyo, tunamuomba Mwenyezi Mungu kwamba asitunyime heri yake kwa uovu kile tulicho nacho.