Al-Baqara
Hii ni tarjama ya tafsiri ya as-Saʿdī kama IslamHouse.com inavyoichapisha katika saadi.islamenc.com, iliyosomwa kutoka kurasa za tovuti hiyo. Tovuti haisemi ni nani aliyeitafsiri kwa lugha nyingine wala inafuata toleo gani lililochapishwa, na haitaji masharti ya kuchukua matini yake, kwa hiyo haki ya kuionyesha haijathibitishwa. Hakuna aliyeilinganisha na kitabu kilichochapishwa, na hakuna mwanazuoni aliyeihakiki. Kila kifungu kipo kando ya aya inazozifafanua, ambazo ni matini ya Qur’ani ya Tanzil, inavyoonekana huko; aya ambayo tovuti haitoi ufafanuzi wake yenyewe inakaa pamoja na kifungu kilichotangulia, na faharasa inataja kila aya ya aina hiyo. Sabīl haikuandika wala kutafsiri kwa lugha nyingine chochote kati yake.
Maandishi kutokasaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)ilichukuliwa 2026-10-22
فِى قُلُوبِهِم مَّرَضٌ فَزَادَهُمُ ٱللَّهُ مَرَضًا ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌۢ بِمَا كَانُوا۟ يَكْذِبُونَ 10
(10) Na kauli yake: “Nyoyoni mwao mna maradhi” kilichokusudiwa na maradhi hapa ni maradhi ya shaka, dhana potovu na unafiki. Kwa sababu, moyo hupatwa na maradhi mawili ambayo yanautoa katika afya yake na wastani wake: Maradhi ya dhana potovu, na maradhi ya matamanio mabaya. Kwa hivyo, ukafiri, unafiki, shaka na uzushi, vyote ni katika maradhi ya dhana potovu. Nao uzinzi, na kupenda machafu na maasia na kuyafanya ni katika maradhi ya matamanio, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake” nayo ni matamanio ya zinaa. Naye aliyeepushwa ni yule aliyeepushwa na haya maradhi mawili, kwa hivyo akapata yakini na imani, na subira kutokana na kila maasia, kwa hivyo akajifahiri katika nguo ndefu za usalama. Na katika kauli yake kuhusu wanafiki: “Nyoyoni mwao mna maradhi, na Mwenyezi Mungu amewazidishia maradhi." Inabainisha hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kuwaandikia waasi maasia, na kwamba kwa sababu ya madhambi yao yaliyotangulia; anawapa mtihani wa maasia yajayo ambayo yanalazimu adhabu zake. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Nasi twazigeuza nyoyo zao na macho yao kama walivyokuwa hawakuamini kwayo mara ya kwanza.” Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Walipopotoka, Mwenyezi Mungu aliziachia nyoyo zao zipotoke.” Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: “Na ama wale wenye maradhi katika nyoyo zao, basi yanawazidishia uovu juu ya uovu wao.” Kwa hivyo, adhabu ya maasia ni maasia baada yake, kama vile malipo ya wema ni wema baada yake. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Na Mwenyezi Mungu huwazidishia uwongofu wale walioongoka.”