Al-Baqara
این ترجمهٔ تفسیر سعدی است، همانگونه که IslamHouse.com آن را در saadi.islamenc.com منتشر میکند و از صفحههای آن سایت گرفته شده است. سایت نمیگوید چه کسی آن را ترجمه کرده و از کدام چاپ پیروی میکند، و برای برداشتن متن آن شرطی بیان نمیکند، پس حق نمایش آن تأیید نشده است. کسی آن را با کتاب چاپی مقایسه نکرده و عالمی آن را بررسی نکرده است. هر بخش در کنار آیههایی آمده که دربارهٔ آنها توضیح میدهد و این آیهها متن قرآن از Tanzil است، همانگونه که آنجا هست؛ آیهای که سایت توضیح جداگانهای برایش نمیدهد با بخش پیش از خود میآید، و فهرست هر چنین آیهای را نام میبرد. سبیل چیزی از آن را ننوشته و ترجمه نکرده است.
متن ازsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)برداشتهشده در 2026-10-22
وَبَشِّرِ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَعَمِلُوا۟ ٱلصَّـٰلِحَـٰتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّـٰتٍ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَـٰرُ ۖ كُلَّمَا رُزِقُوا۟ مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقًا ۙ قَالُوا۟ هَـٰذَا ٱلَّذِى رُزِقْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَأُتُوا۟ بِهِۦ مُتَشَـٰبِهًا ۖ وَلَهُمْ فِيهَآ أَزْوَٰجٌ مُّطَهَّرَةٌ ۖ وَهُمْ فِيهَا خَـٰلِدُونَ ۲۵
(25) Alipotaja malipo ya makafiri, akataja malipo ya Waumini, watu wa matendo mema, kama ilivyo njia yake Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Kitabu chake; Yeye hujumuisha kati ya kupeana matumani na kuhofisha; ili mja awe na matumaini (shauku), mwenye kutishika na kuhofu, mwenye matarajio, basi akasema: "Na wabashirie" yani ewe Mtume, na atakayesimama mahali pako "walioamini" kwa nyoyo zao "na wakatenda mema"; kwa viungo vyao. Basi wakawa wamesadikisha imani yao kwa matendo yao mema. Na matendo ya heri yamesifiwa kuwa ni mema; kwa sababu kwayo, hali ya mja hutengenea, na mambo ya dini yake na dunia yake, na maisha yake ya kidunia na ya kiakhera, na kunamwondokea kwayo kuharibikiwa hali. Basi akawa kwa hayo miongoni mwa wema wanaostahiki kuwa karibu na Ar-rahman (Mwingi wa Rehema) katika Pepo yake, basi akawabashiria "kwamba watapata mabustani" yani mabustani yaliyokusanya miti ya ajabu, na matunda ya kifahari, na vivuli virefu, na matawi ya kawaida na matawi yaliyotanda. Na kwa sababu ya hilo, ikawa pepo ambayo ndani yake anasitirika kwayo aingiaye humo, na ananeemeshwa ndani yake mkazi wake "yapitayo mito chini yake." Yani mito ya maji, na maziwa, na asali na pombe, wakivifanya vimiminike kwa wingi wapendavyo, na wanavipeleka popote wapendapo, na miti hiyo hunyweshwa kutoka humo; basi ikaotesha aina mbalimbali za matunda "kila watakapopewa matunda kutoka humo, watasema: Haya ndiyo kama tuliyo pewa mbele." Yani hii ni ya aina yake na yenye sifa zake, yote yanafanana katika uzuri na ladha, hakuna humo matunda mabaya, na hawana wakati usiokuwa na ladha; hivyo basi wao daima wanapata ladha ya matunda yake. Na kauli yake: "Na wataletewa matunda yaliyofanana" ilisemwa kuwa ni yenye kufanana katika jina tu, lakini ni tofauti katika ladha. Na ilisemwa kuwa ni yenye kufanana katika rangi lakini ni tofauti katika majina. Na ilisemwa kuwa yanafanana yenyewe kwa yenyewe katika uzuri na ladha na katika kufurahisha. Na huenda hii ndiyo bora zaidi. Kisha alipoyataja makazi yao, na vyakula vyao, na vinywaji vyao, na matunda yao, akawataja wake zao, na akawaeleza kwa sifa kamilifu zaidi, na fupi zaidi, na bainifu zaidi. Akasema, “na humo watakuwa na wake waliotakasika” na hakusema kuwa ni safi kutokana na dosari fulani, ili ziweze kuingia humo aina zote za usafi. Wao ni safi wa tabia, safi wa mwenendo, safi wa ulimi, safi wa macho. Hivyo, tabia zao ni kwamba wanapendana na waume wao kwa tabia nzuri. Na watiifu kwa waume wao, wenye adabu za usemi na vitendo, waliosafika katika uumbaji wao kutokana na hedhi, na nifasi, na manii, na mkojo, na kinyesi, na kamasi, na mate, na harufu mbaya. Na wamesafika maumbile yao pia kwa ukamilifu wa uzuri, kwa hivyo wao hawana kasoro, wala maumbile mabaya, bali wao ni wema wazuri, waliosafika ndimi na macho, wenye kuwatulizia waume zao macho yao, wenye kuwatulizia waume zao ndimi zao kutokana na kila maneno maovu. Katika hii aya tukufu, amemtaja anayeleta bishara na anayepewa bishara na kinachobashiriwa kupatwa, na sababu inayopelekea hii bishara. Basi anayeleta bishara ni Mtume rehema na amani ziwe juu yake, na anayesimama mahali pake katika umma wake. Naye anayepewa bishara ni Waumini wanaotenda mema. Nacho kinachobashiriwa kupatwa ni Pepo zilizoelezwa kwa sifa hizo. Nayo sababu inayopelekea bishara hii ni kuwa na imani na kutenda mema. Na hakuna njia yenye kufikisha kwenye bishara hii isipokuwa kwa mawili haya. Na hii ndiyo bishara kubwa mno iliyoletwa kwenye mikono ya mbora zaidi wa viumbe wote, kwa sababu bora zaidi. Na ndani yake kuna pendekezo la kuwapa Waumini bishara na kuwafanya wawe wakakamavu juu ya matendo kwa kutaja malipo yake na matunda yake. Kwa sababu, kwa hili (matendo) yanakuwa hafifu na sahali. Na bishara kubwa mno inayopata mtu ni kumwezesha kuamini na kutenda mema. Na hii ndiyo bishara ya kwanza na asili yake, na baada yake ni bishara ile wakati wa kufa, na baada yake ni kuifikia neema hii ya kudumu. Tunamwomba Mwenyezi Mungu katika fadhila zake.