Skip to content
Tafsir As-Saadi - Swahili · Az-Zumar
Sūrah 39

Az-Zumar

This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.

Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22

Verses 45–46

وَإِذَا ذُكِرَ ٱللَّهُ وَحْدَهُ ٱشْمَأَزَّتْ قُلُوبُ ٱلَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِٱلْـَٔاخِرَةِ ۖ وَإِذَا ذُكِرَ ٱلَّذِينَ مِن دُونِهِۦٓ إِذَا هُمْ يَسْتَبْشِرُونَ 45 قُلِ ٱللَّهُمَّ فَاطِرَ ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ عَـٰلِمَ ٱلْغَيْبِ وَٱلشَّهَـٰدَةِ أَنتَ تَحْكُمُ بَيْنَ عِبَادِكَ فِى مَا كَانُوا۟ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ 46

{45 - 46} Mwenyezi Mungu Mtukufu anataja hali ya washirikina na yale uliyoyalazimu ushirikina wao huo, kwamba "anapotajwa Mwenyezi Mungu" kwa kuamrisha kwamba apwekeshwe na kumkusudia Yeye tu katika dini, kuacha vyote vinavyoabudiwa badala yake; wao wanachafuka roho, wanajitenga na wanalichukia hilo kwa chuki kubwa zaidi. "Na wanapotajwa wenginewe wasiokuwa Yeye," kama vile masanamu na wenza, na mwitaji akawaita wayaabudu na kuyahimidi "basi wao hufurahi" kwa sababu wametajiwa hao ambao wanaabudu, na kwa sababu shirki inaafikiana na matamanio yao. Hali hii ndiyo hali ovu na mbaya zaidi, lakini miadi yao ni Siku ya Malipo. Hapo, haki itachukuliwa kutoka kwao na itaangaliwa: Je, miungu yao hiyo waliyokuwa wakiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu itawafaa kitu? Ndiyo maana akasema: "Sema: Ewe Mwenyezi Mungu! Muumba mbingu na ardhi" na mwendeshaji wake, "Mjuzi wa yasiyoonekana," ambayo yamefichikana machoni petu na hata hatuyajui, "na yanayoonekana! Wewe utahukumu baina ya waja wako katika yale waliyokuwa wakihitalifiana." Na hakika katika kuhitilafiana kukubwa zaidi ni kuhitilafiana kati ya wale wanaompwekesha Mwenyezi Mungu kwa kumkusudia Yeye tu,wale wasemao: Waliyo juu yake ndiyo haki na kwamba watapata mazuri zaidi Akhera mbali na wengineo, na washirikina waliokufanyia wenza na vitu vya kuabudu, wakakufanya sawa na wale walio duni,wasiotoshana na chochote, wakakupunguzia hadhi zaidi na wakafurahi wanapotajwa miungu yao, na wakachafuka unapotajwa Wewe, na wakadai pamoja na hayo kwamba wao wako kwenye haki na kwamba wengineo wako katika batili, na kwamba watapata mazuri zaidi. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika wale walioamini na wale ambao ni Mayahudi, Wasabai, Wakristo, Majusi na wale waliomshirikisha Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atawapambanua baina yao Siku ya Kiyama. Hakika Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu." Alitujulisha kwamba atapambanua kati yao baada yake, akasema: "Hawa ni wagomvi wawili waliogombana kwa ajili ya Mola wao Mlezi. Basi wale waliokufuru watakatiwa nguo za moto na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yanayochemka. Kwa maji hayo vitayeyushwa vilivyomo matumboni mwao na ngozi zao pia. Na kwa ajili yao yatakuwepo marungu ya chuma." Mpaka aliposema: "Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza wale walioamini na wakatenda mema katika Bustani zipitiwazo na mito kati yake. Watapambwa humo kwa mapambo ya mikononi ya dhahabu na lulu. Na mavazi yao humo ni hariri." Na amesema Mtukufu: "Wale ambao wameamini na hawakuchanganya imani yao na dhuluma - hao ndio watakaopata amani na wao ndio walioongoka." Na akasema: "Kwani anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharamishia Pepo, na mahala pake ni Motoni." Katika aya hii, kuna maelezo ya ujumla wa kuumba kwa Mwenyezi, ujumla wa elimu yake na ujumla wa hukumu yake kati ya waja wake. Uweza wake ndio ambao viumbe wanatokana nao. Nayo elimu yake inayokizunguka kila kitu inaashiria kwamba atahukumu baina ya waja wake na kuwafufua, na kwamba anajua matendo yao, mema na mabaya, na kiasi cha malipo yao. Nako kuumba kwake kunaonyesha kwamba anajua yote. Kwani hawezi jua aliyeumba?