الإسراء
هذه ترجمة لتفسير السعدي كما ينشرها IslamHouse.com في saadi.islamenc.com، مقروءةً من صفحات ذلك الموقع. لا يذكر الموقع من ترجمها ولا أي طبعة مطبوعة تتبعها، ولا يذكر شروطًا لأخذ نصّها، ولذلك لم يُتحقق من حق عرضها. لم يقارنها أحد بكتاب مطبوع، ولم يراجعها أحد من العلماء. يقف كل مقطع بجانب الآيات التي يعلّق عليها، وهي نص القرآن من Tanzil كما هو عنده؛ والآية التي لا يعطيها الموقع شرحًا خاصًّا بها تقف مع المقطع الذي قبلها، ويسمّي الفهرس كل آية من هذا النوع. لم يكتب سبيل شيئًا منها ولم يترجمه.
النص منsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)أُخذ في 2026-10-22
قُل لَّوْ كَانَ مَعَهُۥٓ ءَالِهَةٌ كَمَا يَقُولُونَ إِذًا لَّٱبْتَغَوْا۟ إِلَىٰ ذِى ٱلْعَرْشِ سَبِيلًا ٤٢
{42} Na miongoni mwa mambo makubwa ambayo aliyawekea ishara na hoja anuwai ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu ambako ndiyo msingi wa misingi yote. Kwa hivyo akaliamrisha hilo na akakataza kinyume chake, na akalisimamishia hilo hoja za kiakili na za kimaandiko nyingi sana kiasi kwamba mwenye kusikiliza baadhi yake, haziachi moyoni mwake shaka yoyote wala kusitasita. Na katika ushahidi wa hilo ni ushahidi huu wa kiakili ambao alitaja hapa, akasema, "Sema" uwaambie washirikina hawa ambao wanamfanya mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu. "Lau kuwa wangelikuwa pamoja naye miungu mingine kama wasemavyo." Yaani, kulingana na madai yao na uzushi wao wa uongo, "basi wangelitafuta njia ya kumfikia Mwenye Kiti cha Enzi." Yaani, wangetafuta njia ya kumfikia Mwenyezi Mungu kwa kumwabudu, kurudi kwake, kumkaribia, na kutafuta njia ya kumfikia. Basi vipi atamchukua mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu mja maskini ambaye anaona ukubwa wa uhitaji wake kumuabudu Mola wake Mlezi? Je, haya si isipokuwa ni katika dhuluma kubwa zaidi na upumbavu mkubwa zaidi? Na kwa maana hii, aya hii inakuwa na maana kama kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, "Hao wanaowaomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kwendea kwa Mola wao Mlezi - hata miongoni mwao walio karibu mno" na ni kama kauli yake yeye Mtukufu, "Na siku atakapowakusanya wao na hao wanaowaabudu. Na akasema: Je, ni nyinyi mliowapoteza waja wangu hawa, au wao wenyewe walipotea njia? Watasema: Subhanak (Umetakasika na upungufu)! Haikutufailia sisi kujifanyia walinzi wowote badala yako." Na inawezekana kwamba maana ya kauli yake, "Sema: Lau kuwa wangelikuwa pamoja naye miungu mingine kama wasemavyo, basi wangelitafuta njia ya kumfikia Mwenye Kiti cha Enzi." Yaani, wangetafuta njia na wakafanya bidii ya kumshinda Mwenyezi Mungu Mtukufu. Basi ikiwa wao watashinda atakuwa yeye aliye juu na aliye mshidi ndiye Mola Mlezi, Muabudiwa. Lakini kwa kuwa wao wenyewe wanakiri kwamba miungu yao ambayo wanaiomba badala ya Mwenyezi Mungu wameshindwa na hawana chochote katika jambo hilo, basi ni kwa nini waliwafanya kuwa miungu wao ilhali hii ndiyo hali yao? Basi maana hii inakuwa kama kauli yake, "Mwenyezi Mungu hana mwana yeyote, wala hakuna mungu yeyote pamoja naye. Ingekuwa hivyo, basi kila mungu angelichukua alivyoumba, na baadhi yao wangeliwashinda wengine."