At-Tawba 9:117
التوبةلَّقَد تَّابَ ٱللَّهُ عَلَى ٱلنَّبِىِّ وَٱلْمُهَـٰجِرِينَ وَٱلْأَنصَارِ ٱلَّذِينَ ٱتَّبَعُوهُ فِى سَاعَةِ ٱلْعُسْرَةِ مِنۢ بَعْدِ مَا كَادَ يَزِيغُ قُلُوبُ فَرِيقٍ مِّنْهُمْ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّهُۥ بِهِمْ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ
Mwenyezi Mungu alikwishakubali toba ya Nabii na Wahajiri na Ansari waliomfuata katika saa ya ugumu, baada ya kwamba nyoyo za kundi miongoni mwao zilikuwa zimekaribia kukengeuka. Basi akakubali toba yao. Hakika Yeye kwao ni Mpole, Mwenye kurehemu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Mwenyezi Mungu amekwisha pokea toba ya Nabii na Wahajiri na Ansari walio mfuata katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia nyoyo za baadhi yao kugeuka. Basi akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao ni Mpole na ni Mwenye kuwarehemu. [117]
[117] Mwenyezi Mungu Subhanahu amemfadhili Nabii wake na Masahaba wake wenye kuamini, walio wakweli, miongoni mwa Wahajiri na Ansari, walio toka pamoja naye kwenda pigana Jihadi wakati wa shida. (katika vita vya Tabuk) . Aliwaweka imara na akawalinda wasikhitalifiane, baada ya shida ya dhiki ya kuwafarikisha baina yao, hata zikakaribia nyoyo zao kuelekea kutaka kubaki nyuma wasitoke kwenda kwenye Jihadi. Tena Mwenyezi Mungu aliwasamehe kwa ile raghba yao iliyo wapitia ndani ya nafsi zao. Hakika Yeye Subhanahu ni Mwenye upole mwingi, na Mwenye rehema kubwa. Vita hivi vilikuwa mwezi wa Rajab mwaka wa 9 wa Hijra, baina ya Waislamu na Warumi. Na huitwa "Vita vya Dhiki", Ghazwatu U'sr, kwa sababu ya dhiki ya Waislamu waliyo kuwa nayo kwa ukosefu wa mali na zana. Katika vita hivi alijitolea Othman kulizatiti jeshi zima.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Allah Mtukufu Alimuelekeza Nabii Wake Muhammad, (rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie), kurudi Kwake na kumtii, na Aliwakubalia toba Muhãjirûn, waliogura nyumba zao na jamaa zao wakaenda kwenye Nyumba ya Uislamu, na pia Aliwakubalia toba waliomuhami Mtume wa Allah Mtukufu, (rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie), waliotoka pamoja na yeye kupambana na maadui katika vita vya Tabûk katika kipindi cha joto kali na shida ya chakula na vipando. Allah Mtukufu Aliwakubalia toba yao baada ya hali kufikia kiwango kwamba nyoyo za baadhi yao zilikaribia kuiepuka haki na kupendelea ulegevu na utulivu. Lakini Allah Mtukufu Aliwathibitisha na Akawapa nguvu na Akawakubalia toba. Hakika Yeye kwao ni Mwingi wa upole ni mwenye huruma. Na miongoni mwa huruma Yake kwao ni kwamba Aliwapa neema ya kutubia, Akaikubali toba yao na Akawathibitisha juu yake.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net