Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 7 · Aya ya 38

Al-A'raaf 7:38

الأعراف

قَالَ ٱدْخُلُوا۟ فِىٓ أُمَمٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِكُم مِّنَ ٱلْجِنِّ وَٱلْإِنسِ فِى ٱلنَّارِ ۖ كُلَّمَا دَخَلَتْ أُمَّةٌ لَّعَنَتْ أُخْتَهَا ۖ حَتَّىٰٓ إِذَا ٱدَّارَكُوا۟ فِيهَا جَمِيعًا قَالَتْ أُخْرَىٰهُمْ لِأُولَىٰهُمْ رَبَّنَا هَـٰٓؤُلَآءِ أَضَلُّونَا فَـَٔاتِهِمْ عَذَابًا ضِعْفًا مِّنَ ٱلنَّارِ ۖ قَالَ لِكُلٍّ ضِعْفٌ وَلَـٰكِن لَّا تَعْلَمُونَ

Maana

Mwenyezi Mungu atasema: Ingieni (Motoni) pamoja na umma zilizopita kabla yenu miongoni mwa majini na watu. Kila utakapoingia umma, utalaani dada yake. Mpaka watakapokusanyika wote humo, wa mwisho wao atasema juu ya wa mwanzo wao: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio waliotupoteza. Basi wape adhabu ya Motoni maradufu. Atasema: Kila mmoja ana maradufu, lakini nyinyi hamjui tu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Mwenyezi Mungu atasema: Ingieni Motoni pamoja na umma zilizo pita kabla yenu za majini na watu. Kila utakapo ingia umma utawalaani wenzake. Mpaka watakapo kusanyika wote humo, wa mwisho wao watawasema wa mwanzo wao: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio walio tupoteza; basi wape adhabu ya Motoni marudufu. Atasema: Itakuwa kwenu nyote marudufu, lakini nyinyi hamjui tu. [38]

[38] Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atawaambia hawa makafiri: Ingieni Motoni pamoja na kaumu nyengine za kikafiri miongoni mwa watu na majini, walio kwisha kutangulieni. Kila umma ukiingia Motoni huwalaani umma mwingine ulio kufuru mfano wao, na ambao waliwafanya ndio wa kuwafuata. Mpaka wakisha ingia kwa kufuatana wote wakakusanyika, wale walio fuata watawashutumu wale walio kuwa waongozi kwa kusema: Ewe Mola wetu Mlezi! Hao walitupoteza tulipo wafuata, kwa kuwa walitutangulia au kwa kuwa walikuwa ndio wakitutawala. Basi wakatugeuza kwenye Njia ya Haki tusiifuate. Basi wao wape adhabu mara mbili, wabebe malipo ya uasi wao na uasi wetu! Mwenyezi Mungu atawajibu: Kila mmoja wenu atapata adhabu mara mbili ambayo hapana ataye iepuka katika makundi yenu mawili. Wanao fuata watapata adhabu marudufu kwa ukafiri wao na upotovu wao, na kufuata kwao bila ya kuzingatia na kufikiri. Na wale walio fuatwa watapata adhabu marudufu kwa ukafiri wao na upotovu, na pia kwa kuwakufurisha na kuwapotoa wengineo. Lakini nyinyi hamjui kiasi gani itakuwa adhabu ya kila mmoja wenu.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Hapo Allah Mtukufu, Aliyetukuka, Atasema kuwaambia washirikina hawa wazushi, Ingieni Motoni mkiwa pamoja na makundi ya walio mfano wenu katika ukafiri, waliotangulia kabla yenu, kati ya majini na wanadamu. Kila kundi la mila moja likiingia Motoni litalaani watu wa kundi lingine linalofanana nalo, waliokuwa ni sababu ya kupotea kwake kwa kuwafuata. Mpaka watakapokutana ndani ya Moto wote pamoja: wa mwanzo, miongoni mwa wafuasi wa mila za kikafiri, na wa mwisho miongoni mwao; hapo watasema wa mwisho, waliokuwa ni watu wa kuandama ulimwenguni, kuwaambia viongozi wao, «Mola wetu, hawa ndio waliotupoteza wakatupotosha na haki, basi wape adhabu nyongeza ya Moto.» Allah Mtukufu, Aliyetukuka, Atasema, «Kila mmoja atapata nyongeza.» Yaani, kila mmoja kati yenu na wao atapata adhabu nyongeza ya Moto, «lakini nyinyi wafuasi hamuijui ile sehemu ya adhabu na machungu ambayo kila kundi miongoni mwenu ataipata».

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-A'raaf

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net