Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 53 · Aya ya 32

An-Najm 53:32

النجم

ٱلَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَـٰٓئِرَ ٱلْإِثْمِ وَٱلْفَوَٰحِشَ إِلَّا ٱللَّمَمَ ۚ إِنَّ رَبَّكَ وَٰسِعُ ٱلْمَغْفِرَةِ ۚ هُوَ أَعْلَمُ بِكُمْ إِذْ أَنشَأَكُم مِّنَ ٱلْأَرْضِ وَإِذْ أَنتُمْ أَجِنَّةٌ فِى بُطُونِ أُمَّهَـٰتِكُمْ ۖ فَلَا تُزَكُّوٓا۟ أَنفُسَكُمْ ۖ هُوَ أَعْلَمُ بِمَنِ ٱتَّقَىٰٓ

Maana

Ambao wanajiweka mbali na madhambi makuu na vitendo vichafu, isipokuwa makosa hafifu. Hakika Mola wako Mlezi ni Mkunjufu wa maghfira, naye anakujueni sana tangu alipokuumbeni kutoka kwenye ardhi, na mlipokuwa mimba matumboni mwa mama zenu. Basi msijione watakatifu. Yeye anamjua sana mwenye kujikinga akawa mbali na maovu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Ambao wanajiepusha na madhambi makuu na vitendo vichafu, isipo kuwa makosa khafifu. Hakika Mola wako Mlezi ni Mkunjufu wa maghfira, naye anakujueni sana tangu alipo kuumbeni kutoka kwenye ardhi, na mlipo kuwa mimba matumboni mwa mama zenu. Basi msijisifu usafi. Yeye anamjua sana mwenye kujikinga na maovu. [32]

[32] Wema hao ndio wale wanao jitenga na madhambi yenye adhabu kubwa kubwa, na yanayo chukiza mno. Lakini Mwenyezi Mungu husamehe dhambi ndogo ndogo. Hakika Mola wako Mlezi ni Mkuu wa kughufiria, naye anajua vyema hali zenu. Kwani Yeye ndiye aliye kuumbeni kutokana na ardhi, na mlipo kuwa mimba matumboni mwa mama zenu katika hali zenu mbali mbali za kukua na kugeuka. Basi msikae mkijisifu nafsi zenu kuwa mmesafika kwa kujigamba na kujifakhari. Na Yeye ndiye Mjuzi mkubwa kabisa wa kila mwenye kumcha na akajisafisha nafsi yake kweli kweli kwa uchamngu wake.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Nao ni wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu isipokuwa dhambi ndogondogo nazo ni dhambi ndogo ambazo haendelei nazo mwenye kuzifanya, au zile ambazo mja amezifanya kwa nadra. Kwani hizo pamoja na kufanya mambo ya wajibu na kujiepusha na mambo ya haramu, Atayasamehe Allah Mtukufu na Atawasitiria. Hakika Mola wako ni Mkunjufu wa msamaha. Yeye Anazijua zaidi hali zenu Alipomuumba baba yenu Ãdam kwa mchanga, na mlipokuwa bado hamjazaliwa, mko ndani ya matumbo ya mama zenu. Basi msizitakase nafsi zenu, mkazipamba na mkazipa sifa za uchamungu. Yeye Anamjua zaidi anayeogopa mateso Yake miongoni mwa waja Wake na akajiepusha na kufanya mambo ya kumuasi.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

An-Najm

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net