Az-Zumar 39:6
الزمرخَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَٰحِدَةٍ ثُمَّ جَعَلَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَأَنزَلَ لَكُم مِّنَ ٱلْأَنْعَـٰمِ ثَمَـٰنِيَةَ أَزْوَٰجٍ ۚ يَخْلُقُكُمْ فِى بُطُونِ أُمَّهَـٰتِكُمْ خَلْقًا مِّنۢ بَعْدِ خَلْقٍ فِى ظُلُمَـٰتٍ ثَلَـٰثٍ ۚ ذَٰلِكُمُ ٱللَّهُ رَبُّكُمْ لَهُ ٱلْمُلْكُ ۖ لَآ إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُصْرَفُونَ
Amewaumba kutokana na nafsi moja. Kisha akamfanya mwenziwe katika nafsi ile ile. Na akawaletea wanyama wa mifugo jozi nane. Anawaumba katika matumbo ya mama zenu, umbo baada ya umbo, katika viza vitatu. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Hapana mungu isipokuwa Yeye. Basi nyinyi mnageuzwa wapi?
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Amekuumbeni kutokana na nafsi moja. Kisha akamfanya mwenziwe katika nafsi ile ile. Na akakuleteeni wanyama wa mifugo jozi nane. Anakuumbeni katika matumbo ya mama zenu, umbo baada ya umbo, katika viza vitatu. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Basi nyinyi mnageuzwa wapi? [6]
[6] Enyi watu! Mwenyezi Mungu amekuumbeni kutokana na nafsi moja, naye ni Adam, baba wa watu wote. Na amemuumba kutokana na nafsi hiyo mkewe, Hawa. Na amekuteremshieni kwa ajili ya maslaha yenu namna nane za nyama hoa, wanyama wa mifugo, madume na majike. Nao ni ngamia, na ng'ombe, na kondoo, na mbuzi. Naye anakuumbeni matumboni mwa mama zenu kwa kukua na kugeuka geuka, katika viza vitatu, navyo ni kiza cha tumbo, na tumbo la uzazi, na zalio. Huyo aliye kuneemesheni kwa neema hizi ndiye Mwenyezi Mungu, Mlezi wenu, Mwenye kumiliki mambo yenu yote. Ni Yeye tu, si mwenginewe, ndiye Mwenye utawala wa pekee. Hapana wa kuabudiwa kwa Haki ila Yeye. Basi yawaje hata wanaacha kumuabudu Yeye wakenda kuwaabudu wenginewe? Huzuka yai katika mwahala pa kufanyika mayai kwa mwanamke, hata likisha kuwa tayari hutumbukia katika mojapo ya paipu za Filopia likapita humo mpaka kufikia kwenye tumbo la uzazi Rahimi (Womb). Halifiki huko ila kupita siku kidogo, na huenda kijidudu cha manii (Sperm) ya mwanamume kikaliingia hilo yai, na hapo huanza viwango vya kugeuka na kukua kwa mwanzo. Na katika tumbo la uzazi hubaki mtoto muda wa mimba, na hujifanyia vifuniko viwili, na sehemu ya funiko moja hufanyika zalio, placenta. Na funiko jingine ndio humfunika yule mtoto khasa. Yapo maoni mbali mbali juu ya hivyo "viza vitatu" kama ilivyo tajwa katika Aya hii tukufu. Katika hayo ni Tumbo, na tumbo la uzazi, na zalio, yaani mfuko unao mfunika mtoto. (2)Tumbo la uzazi, na ile mifuniko miwili. (3) Tumbo na mgongo na tumbo la uzazi. (4) Panapo toka mayai (Mabiidh, au Ovaries), na paipu ya kupitia mayai, Fillopian tube, na tumbo la uzazi (Rahimi au Womb). Na dhaahiri ni kuwa hii ya mwisho ndiyo rai yenye nguvu zaidi, kwa sababu ni mahala patatu mbali mbali. Ama zile rai nyengine zinaonyesha kwa hakika kiza kimoja katika pahala pamoja palipo zungukwa na t'abaka kadhaa. Na Muumbaji Mtukufu ameashiria katika Kitabu chake ukweli huu wa kisayansi katika zama walipo kuwa watu hawajavumbua hayo mayai ya mwanamke na mwendo wake katika mwili ulio kuwa hauwezi kuonekana kwa macho.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Amewaumba nyinyi Mola wenu, enyi watu, kutokana na Ᾱdam, na Akamuumba kutokana naye mke wake, na Akawaumbia, katika wanyama hoa, aina nane za kiume na kike, miongoni mwa ngamia, ng’ombe, kondoo na mbuzi. Anawaumba nyinyi matumboni mwa mama zenu, umbile baada ya umbile ndani ya giza la tumbo, kizazi na kifuko.Huyo Ndiye Allah Mtukufu Aliyeumba vitu hivi, Mola wenu Aliyepwekeka kwa ufalme na Aliye Mmoja katika uungu, Anayestahiki kuabudiwa PekeYake. Basi ni vipi mnaacha kumuabudu Yeye na mnaelekea kumuabudu asiyekuwa Yeye miongoni mwa viumbe Vyake?
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net