Al-Hajj 22:65
الحجأَلَمْ تَرَ أَنَّ ٱللَّهَ سَخَّرَ لَكُم مَّا فِى ٱلْأَرْضِ وَٱلْفُلْكَ تَجْرِى فِى ٱلْبَحْرِ بِأَمْرِهِۦ وَيُمْسِكُ ٱلسَّمَآءَ أَن تَقَعَ عَلَى ٱلْأَرْضِ إِلَّا بِإِذْنِهِۦٓ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ بِٱلنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ
Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu vilivyo katika ardhi, na merikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi, ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa watu, Mwenye kurehemu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu viliomo katika ardhi, na marikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu. [65]
[65] Ewe mwenye akili! Huyaangalii yaonekanayo kwa macho ya uwezo wa Mwenyezi Mungu, ukaona anavyo wasahilishia watu wote kunafiika na ardhi na viliomo ndani yake? Na akawatengenezea bahari za kwendea ndani yake marikebu kwa mujibu apendavyo Yeye? Na akazishika sayari zote ziliomo angani kwa kudra yake hata zisikosee mpango wake, au zikaangukia kwenye ardhi, isipo kuwa akitaka kwa mapenzi yake. Hakika Mwenyezi Mungu Aliye takasika ni Mwingi wa huruma na rehema kwa waja wake. Kwa hivyo amewatengenezea kila njia za maisha mema. Huwaje basi baada ya haya yote hamumsafii niya Yeye kwa kumshukuru na kumuabudu? "Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu viliomo katika ardhi, na marikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu." Aya hii tukufu inakusanya maana za kisayansi za ndani. Mbingu, nayo ni kila kilicho juu yetu, inaanza kwa kuifunika ardhi kwa hewa, tena kwa anga, tena kwa vyombo vya mbinguni vinavyo toa mwanga kama nyota n.k. na visio toa mwanga wake mwenyewe kama mwezi, na sayari nyengine, na nyota mkia, na vumbi la ulimwengu, n.k. Vyote hivi vinakuwa vilivyo na vinashikana kwa athari ya nguvu mbali mbali. Muhimu wa hizo ni mvuto na nguvu inayo tokana na kule kuzunguka kwao. Yamedhihiri mapenzi ya Mwenyezi Mungu na huruma zake kwa waja wake kuwa katengeneza kifuniko cha angani kina namna za gasi mbali mbali ambazo ni dharura kwa uhai. Kama pia anawalinda wakaazi wa duniani na mianga na vimondo n.k. vinavyo zunguka angani na ambavyo vinapo karibia kwenye ardhi huungua kabla havijafika chini. Na katika mapenzi yake na rehema yake Mwenyezi Mungu ni kuwa hivyo vimondo vinavyo anguka kwenye ardhi ni nadra sana kutokea, na hutokea mwahala wasipo kaa watu. Jambo hili la dhaahiri laonyesha huruma na rehema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Na haya yanatilia nguvu na kusadikisha kauli yake Mwenyezi Mungu: " na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu."
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Je, huoni kwamba Allah Mtukufu, Aliyetukuka, Amewadhalilishia vilivyoko ardhini miongoni mwa vitu vitambaavyo na wanyama na nafaka na matunda na vitu visivyo na roho, kwa ajili ya kipando chenu, chakula chenu na manufaa yenu, kama Alivyowadhalilishia mashua zinazotembea baharini kwa uwezo Wake na amri Yake, ziwabebe nyinyi na vyombo vyenu ziwafikishe kwenye miji na sehemu mzitakazo, na kwamba Yeye Ndiye Anayeizuia mbingu na kuitunza, ili isianguke juu ya ardhi ikawaangamiza walioko juu yake isipokuwa kwa idhini Yake, Aliyetakasika na kila sifa za upungufu, kuwa hilo lifanyike, ili Awarehemu watu rehema kunjufu katika mambo yao ya hivi sasa hapa duniani na ya baadaye kesho Akhera? Na miongoni mwa rehema Zake ni vitu hivi Alivyowadhalilishia na vinginevyo kwa fadhila Zake juu yao.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net