Ruka hadi kwenye maudhui
Tafsir As-Saadi - Swahili · Al-Ghaafir
Sura ya 40

Al-Ghaafir

Hii ni tarjama ya tafsiri ya as-Saʿdī kama IslamHouse.com inavyoichapisha katika saadi.islamenc.com, iliyosomwa kutoka kurasa za tovuti hiyo. Tovuti haisemi ni nani aliyeitafsiri kwa lugha nyingine wala inafuata toleo gani lililochapishwa, na haitaji masharti ya kuchukua matini yake, kwa hiyo haki ya kuionyesha haijathibitishwa. Hakuna aliyeilinganisha na kitabu kilichochapishwa, na hakuna mwanazuoni aliyeihakiki. Kila kifungu kipo kando ya aya inazozifafanua, ambazo ni matini ya Qur’ani ya Tanzil, inavyoonekana huko; aya ambayo tovuti haitoi ufafanuzi wake yenyewe inakaa pamoja na kifungu kilichotangulia, na faharasa inataja kila aya ya aina hiyo. Sabīl haikuandika wala kutafsiri kwa lugha nyingine chochote kati yake.

Maandishi kutokasaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)ilichukuliwa 2026-10-22

Aya ya 9

وَقِهِمُ ٱلسَّيِّـَٔاتِ ۚ وَمَن تَقِ ٱلسَّيِّـَٔاتِ يَوْمَئِذٍ فَقَدْ رَحِمْتَهُۥ ۚ وَذَٰلِكَ هُوَ ٱلْفَوْزُ ٱلْعَظِيمُ 9

{9} "Na waepushe na maovu;" yaani, matendo maovu na adhabu yake. "Kwani umwepushaye maovu siku hiyo" ya Kiyama "hakika umemrehemu," kwa sababu rehema yako haijaacha kuwafikia waja na hakuna kinachozizuia rehema zako isipokuwa madhambi ya waja na mabaya yao. Na yule ambaye utamwepusha maovu, basi utakuwa umemuwezesha kufikia mazuri na malipo yake mazuri. "Na huko" kuondokewa na yanayotaadhariwa kwa kumlinda mja kutokana na maovu na kuweza kupata anachopenda kwa kupata rehema "ndiko kufuzu kukubwa," ambako hakuna kufaulu mfano wake, wala washindani hawashindani kwa ajili ya kizuri zaidi yake. Dua hii kutoka kwa Malaika inajumuisha: Kumjua kwao Mola wao Mlezi kikamilifu na kumtegemea Mwenyezi Mungu kwa majina yake mazuri zaidi, ambayo anapenda kwamba waja wake wafike kwake kupitia hayo na kuomba dua kwa kutumia majina yanayofailia kitu ambacho wanakiomba kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hapa, walijifikisha kwa Mwenyezi Mungu kupitia majina yake mawili ambayo ni Mwingi wa rehema na Mwingi wa kurehemu. Hii ni kwa kuwa waliomba dua kwamba wapewe rehema na waondolewe athari za yale ambayo nafsi za wanadamu zilihitaji, ambazo Mwenyezi Mungu alijua kwamba zilikuwa na upungufu kwa kufanya maasia na mambo mengineyo ambayo Mwenyezi Mungu alishayadhibiti kwa elimu yake. Pia inajumuisha ukamilifu wa adabu zao mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kukiri umola wake wa jumla na wa mahususi juu yao. Na kwamba hawana jambo lao katika suala hilo, bali dua yao waliyomuomba Mola wao Mlezi ilitoka kwa yule ambaye ni masikini katika dhati yake kwa namna yoyote ile na hawezi kujisimamia mbali na Mola wake Mlezi kwa hali yoyote ile. Hii sio isipokuwa fadhila ya Mwenyezi Mungu, ukarimu wake na wema wake. Pia inajumuisha kuafikiana kwao kikamilifu na Mola wao Mlezi kwa kupenda matendo anayoyapenda, ambayo ni ibada wanazozifanya na wanajitahidi sana kama wanavyojitahidi wapenzi, na wakaafikiana naye kuhusiana na wanayoyatenda matendo hayo ambao ni waumini, ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu anawapenda kati ya viumbe wake wote. Kwani Mwenyezi Mungu anawachukia viumbe wote wanaojukumishwa kisheria isipokuwa Waumini miongoni mwao. Na kwa sababu ya upendo wa malaika kwao, walimwomba Mwenyezi Mungu na wakajitahidi kuboresha hali zao. Kumwombea mtu dua ni katika ishara za wazi kabisa za upendo wake juu yake. Kwa sababu mtu hamuombei isipokuwa yule ambaye anampenda. Yale ambayo Mwenyezi Mungu alibainisha na kueleza kwa kina kuhusiana na dua yao - baada ya kauli yake: "wanawaombea msamaha wale walioamini" - yanajumuisha tanabahisho nzuri sana juu ya jinsi ya kukitafakari Kitabu chake.Na kwamba mwenye kukitafakari kitabu hiki hafai kusimamia tu kwa lafudhi ya neno peke yake, bali anapaswa kutafakari maana ya lafudhi pia. Ikiwa ataifahamu kwa usahihi namna ilivyo,atalitazama jambo hilo kwa akili yake na atatazama njia zinazolifikia, na yale ambayo hayatimii bila ya hilo, na yale ambayo linategemea juu yake, na awe na hakika kwamba Mwenyezi Mungu alilitaka; kama anao uhakika kwamba alitaka maana yake mahususi inayoashiriwa na neno na lafudhi hiyo. Na yale yanayolazimu kuwa na yakini juu yake kwamba Mwenyezi Mungu alilitaka ni mambo mawili: moja yake ni kwamba ajue na awe na uhakika kwamba ni moja ya mambo yanayotokana na maana yake na ambayo inategemea juu yake. Ya pili ni ajue kwamba Mwenyezi Mungu anajua vyema kila kitu, na kwamba Mwenyezi Mungu amewaamrisha waja wake kukizingatia na kukitafakari Kitabu chake. Mwenyezi Mungu Mtukufu alijua kinachohitajika katika maana hizo, na Yeye ndiye aliyetufahamisha kwamba Kitabu chake ni uwongofu, nuru na ufafanuzi wa kila kitu, na kwamba ndicho chenye maneno yenye ufasaha zaidi na yenye kubainisha kwa kina zaidi. Kwa kupitia hayo, mja anapata elimu kubwa na heri nyingi kulingana na yale ambayo Mwenyezi Mungu amemuwezesha. Katika tafsiri yetu kulikuwa na mengi katika haya ambayo Mwenyezi Mungu ametuneemesha kwayo, na katika baadhi ya aya maana yake inaweza kufichikana kwa yule ambaye hafikirii kwa njia sahihi. Na tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atufungulie katika hazina za rehema zake mambo ambayo yatakuwa ni sababu ya kutengenea kwa hali zetu na hali za Waislamu, kwani hatuna ila kushikamana na ukarimu wake na kumfikia kupitia wema wake ambao bado tunaendelea kuupata katika wakati wote. Pia tunamuomba kutokana na fadhila zake kwamba atulinde kutokana na uovu wa nafsi zetu ambao unazuia kuifikia rehema yake. Hakika, Yeye ndiye Mkarimu zaidi, Mpaji zaidi, ambaye alitupa fadhila zake na visababu vya kuzifikia. Aya hii pia inajumuisha kwamba watu wanaokuwa pamoja kama vile mume, mke, mtoto na rafiki wanafaidika kutoka kwa wenzake na unakuwa uhusiano wao huo ndiyo sababu ya kufikia heri ambayo yeye mwenyewe hakuifanya; kama vile Malaika wanavyowaombea Waumini na wale waliofanya mema miongoni mwa wazee wao, wake zao na dhuriya zao. Lakini, pia inaweza kusemwa kwamba ni lazima wao wenyewe wawe wema, kulingana na kauli yake: "na wale waliofanya mema." Ikiwa ni hivyo, basi inakuwa kwamba hayo yote ni matokeo ya matendo yao. Na Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye zaidi.