Al-Kahf
Kani waa tarjumaad tafsiirka as-Saʿdī sida IslamHouse.com ugu daabacdo saadi.islamenc.com, oo laga akhriyay bogagga goobtaas. Goobtu ma sheegayso cidda tarjuntay ama daabacaadda la daabacay ee ay raacayso, mana sheegayso shuruudo qaadashada qoraalkeeda ah, sidaas darteed xaqa muujinteeda lama xaqiijin. Qofna ma barbardhigin buug la daabacay, aqoonyahanna ma dib u eegin. Qayb kasta waxay ag taagan tahay aayadaha ay ka hadlayso, kuwaas oo ah qoraalka Quraanka ee Tanzil, sida uu ugu yaal halkaas; aayad goobtu aanay faallo u gaar ah ka bixin waxay la taagan tahay qaybta ka horraysa, tusmaduna waxay magacaabaysaa aayad kasta oo caynkaas ah. Sabīl wax ka mid ah ma qorin, mana tarjumin.
Qoraalka waxaa laga helaysaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)la qaaday 2026-10-22
وَأَمَّا ٱلْجِدَارُ فَكَانَ لِغُلَـٰمَيْنِ يَتِيمَيْنِ فِى ٱلْمَدِينَةِ وَكَانَ تَحْتَهُۥ كَنزٌ لَّهُمَا وَكَانَ أَبُوهُمَا صَـٰلِحًا فَأَرَادَ رَبُّكَ أَن يَبْلُغَآ أَشُدَّهُمَا وَيَسْتَخْرِجَا كَنزَهُمَا رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ ۚ وَمَا فَعَلْتُهُۥ عَنْ أَمْرِى ۚ ذَٰلِكَ تَأْوِيلُ مَا لَمْ تَسْطِع عَّلَيْهِ صَبْرًا 82
{82}. ''Na ama ukuta ule" ambao niliusimamisha, ''huo ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini. Na chini yake ilikuwako hazina yao; na baba yao alikuwa ni mtu mwema." Yaani, hali yao inahitaji wafanyiwe upole na kuwarehemu, kwa sababu wao ni wachanga ambao walimpoteza baba yao, na Mwenyezi Mungu pia aliwahifadhi kwa sababu ya wema wa wazazi wao. ''Basi Mola wako Mlezi alitaka wafikie utu uzima wao na wajitolee hazina yao wenyewe." Na ndiyo maana niliubomoa ukuta huo, nikatoa hazina iliyokuwa chini yake, na nikaujenga tena, kisha nikairudisha hazina yao bure bila malipo. "Hii ikiwa ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi" ambayo Mwenyezi Mungu alimpa mja wake Al-Khidhr. "Wala mimi sikuyatenda hayo kwa amri yangu'' na kwa kutaka kwangu tu. Lakini hayo yalikuwa kutokana na rehema ya Mwenyezi Mungu na amri yake. ''Hiyo'' ambayo nimekufasiri "ndiyo tafsiri ya hayo ambayo wewe hukuweza kuyasubiria." Na katika kisa hiki cha ajabu na kitukufu, kunazo faida, hukumu, na misingi mingi ambayo tutaonyesha baadhi yake kwa msaada wa Mwenyezi Mungu: Miongoni mwake ni ubora wa elimu na kusafiri kwa ajili ya kuitafuta, na kwamba hayo ndiyo mambo muhimu zaidi. Kwa maana, Musa, amani iwe juu yake, alisafiri kwenda umbali mrefu, na akapata uchovu katika kuitafuta, na akaacha kukaa pamoja na Wana wa Israili ili awafundishe na kuwaelekeza, na akachagua kusafiri ili kuongeza elimu kuliko hayo. Na miongoni mwake ni kuanza na kilicho muhimu zaidi kisha kinachokifuata kwa umuhimu. Kwa maana, kuzidisha elimu na elimu ya mwanadamu ni muhimu zaidi kuliko kuliacha hilo, na kushughulika na kufundisha pasi na kujiongezea elimu, na kuyachanganya mambo mawili haya ndio ukamilifu zaidi. Miongoni mwake ni kwamba inaruhusika kuwa na mtumishi nyumbani na safarini, ili atosheleze kazi mbalimbali na ili akupumzishe, kama alivyofanya Musa. Miongoni mwake ni kwamba mwenye kusafiri kwa ajili ya kutafuta elimu, au kushiriki katika jihadi au mengineyo ikiwa masilahi yatahitaji kujulisha anachotafuta na anakokwenda, basi hilo ni kamilizi zaidi kuliko kulificha. Kwa maana, katika kulidhihirisha kuna faida kama vile kujiandaa kwa ajili ya hili maandalizi mazuri, na ili kulifanya jambo kwa ufahamu, na kuonyesha hamu kubwa juu ya ibada hii tukufu. Kama Musa alivyosema, ''Sitaacha kuendelea mpaka nifike zinapokutana bahari mbili, au nitaendelea kwa muda mrefu.'' Na kama Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, - alivyowajulisha maswahaba zake wakati alipotaka kwenda katika vita vya Tabuk kuhusu anakokwenda, pamoja na kwamba kawaida yake nikujulisha kuhusu jambo kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja, na hilo linafuatana na masilahi. Na miongoni mwake ni kufungamanisha uovu na sababu zake na Shetani kwa njia ya kushawishi na kupamba maovu. Hata kama yote hayo ni kutika hukumu na majaliwa ya Mwenyezi Mungu, kwa kauli ya kijana wa Musa, ''Na hakuna aliyenisahaulisha kulikumbuka isipokuwa Shetani tu." Na miongoni mwake ni kwamba inaruhusika kumjulisha mtu yale ambayo ni katika mambo ya kimaumbile kama vile uchovu, njaa, au kiu, ikiwa sio kwa njia ya hasira na yakawa ni ukweli. Kwa kauli ya Musa, "Kwa hakika tumepata machovu kweli kwa hii safari yetu." Na miongoni mwake ni kuwa inapendekezwa kwamba mtumishi wa mtu awe mwerevu, mwenye uelewa wa haraka, mwenye busara ili aweze kufikia kile anachotaka. Na miongoni mwake ni kwamba inapendekezwa kwa mtu kumlisha mtumishi wake kutoka katika chakula chake na kwamba wakile pamoja. Kwa sababu maana ya dhahiri ya kauli yake ''Tupe chakula chetu cha mchana'' inawafungamanisha wote nacho, na kwamba yeye Musa na kijana wake wote walikula kwacho. Miongoni mwake ni kwamba msaada unamshukia mja kulingana na kufanya kwake aliyoamrishwa, na kwamba mwenye kuafiki amri ya Mwenyezi Mungu husaidiwa kwa namna asiyosaidiwa asiyekuwa yeye. Kwa kauli yake, ''Hakika tumepata uchovu katika safari yetu hii.'' Na sehemu ya safari inayoashiriwa hapa ni ile sehemu yake waliyokuwa tayari wameshapita makutano ya bahari zile mbili. Na ama sehemu yake ya kwanza, hakulalamika kwa sababu yake uchovu wowote pamoja na urefu wake, kwa sababu ndiyo ilikuwa safari kwa uhakika. Na ama ya mwisho, basi la dhahiri ni kwamba ilikuwa baadhi ya siku, kwa sababu walimpoteza samaki wao walipokimbilia kwenye mwamba. Na la dhahiri ni kwamba walilala hapo, kisha wakaendelea kutembea kesho yake mpaka ilipokuwa ni wakati wa chakula cha mchana, Musa akamwambia kijana wake: Tupe chakula chetu cha mchana. Basi hapo, ndipo akakumbuka kwamba alikisahau pale mahali ambapo palikuwa amepakusudia hasa. Na miongoni mwake ni kwamba mja huyo ambaye Musa alikutana naye hakuwa nabii, bali alikuwa mja mwema tu. Kwa sababu alimuelezea kwa sifa ya uja tu, na akataja neema ya Mwenyezi Mungu juu yake kwa rehema na elimu. Lakini hakutaja utume wake wala unabii wake. Na kama angekuwa nabii, basi angetaja hilo kama alivyowataja wengineo. Na ama kauli yake mwishoni mwa kisa hiki, ''Wala mimi sikutenda hayo kwa amri yangu,'' hiyo haionyeshi kuwa yeye ni nabii, lakini inaonyesha tu kwamba alifahamishwa na kuonyeshwa hayo na Mwenyezi Mungu, na wanavyofanyiwa hivyo wasiokuwa manabii pia. Kama alivyosema Yeye Mtukufu, ''Na tulimfunulia mama yake Musa kwa kumwambia: Mnyonyeshe." Na kauli yake, "Na Mola wako Mlezi amemfunulia nyuki: Jitengenezee majumba yako." Na miongoni mwake ni kwamba elimu ambayo Mwenyezi Mungu anawafundisha waja wake ni ya aina mbili: elimu ya kujifundisha ambayo mja huipata kwa bidii yake na kujitahidi kwake, na aina nyingine ni elimu ya kupewa na Mwenyezi Mungu ambayo Mwenyezi Mungu humtunuku anayemneemesha kwayo katika waja wake. Kwa kauli yake, ''na tukamfunza mafunzo yaliyotoka kwetu." Na miongoni mwake ni kuwa na adabu mbele ya mwalimu na mwanafunzi kuzungumza naye kwa maneno ya upole zaidi, kama alivyosema Musa, amani iwe juu yake, "Je, nikufuate ili unifundishe kile ulichofundishwa cha uwongofu?" Akawa ameyatoa maneno kwa njia ya upole na kutafuta ushauri, na kwamba unaniruhusu kufanya hivyo au la? Na kukubali kwake kwamba ajifunze kutoka kwake. Haya ni tofauti na yale wayafanyayo wale ambao hawana adabu na wenye kiburi, ambao hawamuonyeshi mwalimu kwamba wanahitaji elimu yake. Lakini wanadai kwamba atashirikiana naye na hata anaweza kufikiria kuwa anamfundisha mwalimu wake ilhali yeye ni mjinga sana. Kwa hivyo, kujidhalilisha mbele ya mwalimu na kuonyesha kwamba anahitaji amfundishe ni katika mambo yenye manufaa zaidi kwa mwanafunzi. Na miongoni mwake ni kunyenyekea kwa yule alieye bora mbele ya yule aliye chini yake. Kwa maana, Musa bila shaka ni bora kuliko Al-Khidhr. Na miongoni mwake ni kwamba mwanachuoni bora anaweza kujifunza elimu ambayo hakuijua vilivyo kutoka kwa yule ambaye ni stadi ndani yake, hata kama atakuwa chini yake katika elimu kwa daraja nyingi. Kwa maana Musa, amani iwe juu yake, alikuwa katika Mitume wenye stahamala kubwa sana ambao Mwenyezi Mungu aliwapa elimu ambayo hakuwapa wengineo, lakini elimu hii maalumu, mja mwema Al-Khidhr alikuwa na kile ambacho Musa hawakuwa nacho. Basi ndiyo maana akafanya bidii ili ajifunze kutoka kwake. Na haipaswi kwa mwanachuoni katika elimu ya Fiqhi na hadithi akiwa na upungufu na kasoro katika elimu ya nahwu au swarf, au mfano wake miongoni mwa elimu tofautitofauti, asijifundishe kutoka kwa yule ambaye ni stadi katika hilo hata kama si mwanachuoni wa hadithi wala elimu ya Fiqhi. Na miongoni mwake ni kufungamanisha elimu na mengineyo miongoni mwa fadhila nyinginezo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kukubali hilo, na kumshukuru Mwenyezi Mungu juu yake, kauli yake, ''unifunze katika ule uwongofu uliofunzwa wewe?'' Yaani, katika yale ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu alikufundisha. Na katika hayo ni kwamba elimu yenye manufaa ni elimu inayoelekeza mtu katika mambo ya heri. Kwa hivyo, kila elimu yenye kuelekeleza sawasawa na yenye kuongoza kwenye heri na kutahadharisha na njia ya uovu njia ya kufanya hivyo, basi hiyo ni katika elimu yenye manufaa. Na chochote kisichokuwa hivyo, basi ima ni yenye madhara au haina faida, kwa kauli yake, "ili unifunze katika ule uwongofu uliofunzwa wewe?" Na miongoni mwake ni kwamba yeyote asiyekuwa na nguvu ya kusubiri juu ya kumpa usuhuba mwanachuoni na kusubiri juu ya elimu na kuwa imara sawasawa katika hilo, basi [atakosa elimu nyingi kulingana na kutoweza kusubiri kwake katika hilo]. Kwa hivyo, yeyote asiyeweza kusubiri, hawezi kuipata elimu. Na yeyote mwenye kusubiri na akashikamana nayo, basi atapata kwayo kila kitu anachokifanyia bidii. Kama alivyosema Al-Khidhr huku akitaka Musa kumkubalia udhuru, kwa kutaja kizuizi kilichomzuia Musa kujifunza elimu kutoka kwake: kwamba hakuweza kusubiri kuwa pamoja naye. Na miongoni mwake ni kwamba sababu kubwa ya kuweza kusubiri ni mtu kulijua sawasawa jambo hilo na kuwa na uzoefu na jambo hilo ambalo aliamrishwa alivumilie. Vinginevyo, yeyote asiyelijua au asiyejua kusudi lake, matokeo yake, wala faida yake na matunda yake, basi hatakuwa na sababu ya kusubiri juu yake. Kama alivyosema, ''Na utawezaje kusubiri yale usiyoyajua vilivyo undani wake?" Kwa hivyo akafanya sababu ya kutosubiri kwake kuwa ni kutojua kwake vyema jambo hilo. Na miongoni mwake ni amri ya kutoharakisha, kuthibitisha mambo, na kutoharakisha kutoa hukumu ya jambo mpaka mtu ajue linalotakikana na ni lipi hasa linalokusudiwa. Miongoni mwake ni kufungamanisha mambo ya baadaye ambayo ni katika matendo ya waja na mapenzi yake Mwenyezi Mungu, na kwamba mtu asiseme chochote: Hakika mimi nitafanya hilo katika siku zijazo isipokuwa na aseme pia: Mwenyezi Mungu akipenda. Na miongoni mwake ni kwamba kuazimia kufanya kitu siyo sawa na kukifanya hasa. Kwa maana, Musa alisema, ''Inshaallah (Mwenyezi Mungu) akipenda, utanipata ni mwenye kusubiri." Basi akaanza kuizoesha nafasi yake juu ya kusubiri lakini hakufanya hivyo. Na miongoni mwake ni kwamba ikiwa mwalimu ataona kwamba kuna masilahi katika kumzuia mwanafunzi kuuliza maswali mwanzoni juu ya baadhi ya vitu mpaka mwalimu mwenyewe awe ndiye anayemjulisha juu yake, basi inapaswa kufuata masilahi hayo, kama vile ikiwa uelewa wake ni mdogo, au akamkataza kuuliza mambo madogo ambayo mengineyo ni muhimu zaidi kuliko hayo au kwamba akili yake haiyafikii, au kuuliza swali ambalo halihusiani na jambo hilo. Na miongoni mwake, ni kuruhusiwa kusafiri baharini katika hali isipokuwa ile ambayo kuna hofu katika hilo. Na miongoni mwake ni kwamba mwenye kusahau halaumiwi kwa kusahau kwake, si kwa haki ya Mwenyezi Mungu, wala katika haki za waja wake, kwa kauli yake, "Usinichukulie kwa niliyosahau.'' Na miongoni mwake ni kwamba mtu anapaswa kuchukua katika tabia za watu na miamala yao kile cha chini zaidi na kile ambacho nafsi zao ziliweza kufanya, na wala haifai kuwatwika kile ambacho hawakiwezi au kuwafanyia ugumu na kuwachosha. Kwa maana, hili litasababisha wajitenge naye na kuchoka naye, lakini na achukue chepesi ili jambo hilo limuwiye jepesi. Na miongoni mwake ni kwamba hukumu za mambo zinahukumiwa kulingana na dhahiri zake, na zinafungamanishwa hivyo na hukumu za kidunia zinazohusiana na mali, damu, na mengineyo. Kwa maana, Musa, amani iwe juu yake, alimkataza Al-Khidhr kulitoboa lile jahazi na kumuua kijana yule, na kwamba mambo haya kwa dhahiri yake ni kwamba ni maovu, na Musa, amani iwe juu yake, hakuweza kukaa kimya juu yake katika hali isiyokuwa hii ya kuandamana kwake na Al-Khidhr. Kwa hivyo yeye, amani iwe juu yake, akaharakisha na kukimbilia kuyahukumu kulingana na hali yake ya ujumla, na wala hakuzingatia mambo hayo yaliyofungamana nayo ambayo yalimhitaji kusubiri na kutoharakisha kukataza. Miongoni mwake ni ile kanuni kubwa tukufu ambayo ni kwamba uovu mkubwa unaweza kuzuiwa kwa kutenda uovu mdogo, na yanazingatiwa masilahi makubwa zaidi kati ya masilahi mawili hayo kwa kukosa masilahi yaliyo chini kati ya hayo. Kwa maana, kumuua mvulana ni uovu, lakini kuishi kwake hadi awatie majaribio wazazi ili waiache dini yao ni uovu mkubwa kuliko huo. Na kuishi kwa mvulana huyo bila ya kumua na kuuhifadhi uhai wake, hata kama inafikiriwa kuwa ni heri, lakini heri katika kubakia dini ya wazazi wake na imani yao ni bora kuliko hiyo. Na ndiyo kwa sababu hiyo Al-Khidhr akamuua. Na chini ya kanuni hii, kuna matawi na faida mbazo hazihesabiwi. Kwa maana, suala la kushindana kwa masilahi na uharibifu yote yanaingia katika hili. Na miongoni mwake ni kwamba ni kanuni hii kuu pia ambayo ni kwamba matendo ya mtu ya katika mali ya wengine, ikiwa ni kwa masilahi bora na kuondoa uharibifu, basi hilo linaruhusiwa, hata kama ni bila ya ruhusa. Hata kama kazi yake hiyo itasababisha kuharibika kwa baadhi ya mali hiyo ya wengine, kama mja Al-Khidhr alivyolitoboa lile jahazi ili liwe na dosari ili lisalimike kutokana na kupokonywa na mfalme yule dhalimu. Kwa hivyo, lau lingechomeka, au kuzama, au mambo kama hayo katika nyumba ya mtu yoyote au mali zake, na ikawa katika kuharibu baadhi ya mali hiyo au kubomoa baadhi ya nyumba hiyo kuna usalama kwa sehemu iliyobakia, basi mtu anaruhusiwa kufanya hivyo, bali sheria imemruhusu kufanya hivyo ili kuhifadhi mali za wengine. Vivyo hivyo, ikiwa mtu dhalimu atataka kuchukua mali za wengine, na mtu akampa mali kiasi fulani ili kukomboa zilizobaki, basi hilo linaruhusiwa, hata kama ni bila ya ruhusa. Na miongoni mwake ni kwamba inaruhusiwa kufanya kazi baharini kama inavyoruhusiwa katika nchi kavu. Kwa kauli yake, "wafanyao kazi baharini,'' na hakuwakataza kazi yao hiyo. Na miongoni mwake ni kwamba masikini anaweza kuwa na mali ambazo hazimtoshelezi na wala hatoki kwa hilo nje ya jina la umasikini, kwa sababu Mwenyezi Mungu alijusha kwamba masikini hawa wana jahazi. Na miongoni mwake ni kwamba mauaji ni katika madhambi makubwa zaidi. Kwa kauli yake kuhusiana na kuuawa kwa kijana yule, "Ama hakika umefanya jambo baya kabisa!" Na miongoni mwake ni kwamba kuua kwa kisasi si jambo linalokatazwa. Kwa sababu ya kauli yake, ''wala hakuuwa." Na miongoni mwake ni kwamba mja mwema analindwa na Mwenyezi Mungu katika nafsi yake na katika kizazi chake. Na miongoni mwake ni kwamba kuwatumikia watu wema au wale wanaohusiana nao ni bora kuliko kufanya mengineyo, kwa sababu alitoa sababu ya kutoa hazina yao hiyo na kuusimamisha ukuta wao huo tena kwamba ni kwa kuwa baba yao alikuwa ni mwema. Na miongoni mwake ni kuwa na adabu mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika maneno. Kwa maana, Al-Khidr alifungamanisha kuitia kasoro jahazi ile na yeye mwenyewe, kwa kauli yake, "nilitaka kuitia dosari." Na ama heri, hiyo aliifungamanisha na Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kauli yake, ''Basi Mola wako Mlezi alitaka wafikie utu uzima wao na wajitolee hazina yao wenyewe, hii ikiwa ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi." Kama alivyosema Ibrahim, amani iwe juu yake, "Na ninapougua, ni Yeye ndiye anayeniponesha." Nao majini walisema, "Nasi hatujui kama wanatakiwa uovu wale wanaokaa kwenye ardhi au Mola wao Mlezi anawatakia uwongofu." Pamoja na kwamba yote hayo ni kwa majaliwa ya Mwenyezi Mungu na hatima yake. Na miongoni mwake ni kwamba rafiki asimwache mwenzake kwa hali yoyote ile na kuacha urafiki wake hadi atakapomlaumu na kumtaka mwenzake huyo amkubalie udhuru wake, kama vile alivyofanya Al-Khidhr alipokuwa pamoja na Musa. Na miongoni mwake ni kwamba kuafikiana kwa rafiki na mwenzake katika mambo yasiyokuwa ya haramu inachangia na ni sababu ya kubakia urafiki huo na kuusisitiza, kama vile kutoafikiana naye ni sababu ya kukatika kwa urafiki huo. [Na miongoni mwake ni kwamba mambo haya ambayo Al-Khidhr aliyafanya ni hatima tupu, ambayo Mwenyezi Mungu aliyapitisha na akayaweka mikononi mwa mja huyu mwema ili waja waweze kuchukua hayo kama ushahidi juu ya hukumu zake. Na kwamba anaweza kumwandikia mja mambo ambayo anayachukia sana, lakini hayo ndiyo yenye kumtengenezea dini yake. Kama ilivyo katika suala la kijana yule. Na hayo ndiyo yenye kuutengeneza vyema dunia yake, kama ilivyo katika suala la jahazi lile. Kwa hivyo aliwaonyesha mfano wa upole wake na ukarimu wake ili wapate kuujua, na waridhie kabisa na hukumu zake zinazochukiza].