At-Tawba
Ini ialah terjemahan Tafsir as-Saʿdī seperti yang diterbitkan oleh IslamHouse.com di saadi.islamenc.com, dibaca daripada halaman-halaman laman itu. Laman itu tidak menyatakan siapa yang menterjemahkannya atau edisi cetakan mana yang diikutinya, dan tidak menyatakan syarat untuk mengambil teksnya, maka hak untuk memaparkannya belum disahkan. Belum ada sesiapa yang membandingkannya dengan buku bercetak, dan tiada ulama yang menyemaknya. Setiap bahagian berada di sisi ayat-ayat yang diulasnya, iaitu teks Al-Quran daripada Tanzil, dipaparkan seperti yang ada di sana; ayat yang tidak diberi ulasan tersendiri oleh laman itu berada bersama bahagian sebelumnya, dan indeks menamakan setiap ayat sedemikian. Sabīl tidak menulis atau menterjemahkan satu pun daripadanya.
Teks daripadasaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)diambil pada 2026-10-22
إِلَّا تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ ٱللَّهُ إِذْ أَخْرَجَهُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ ثَانِىَ ٱثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِى ٱلْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَـٰحِبِهِۦ لَا تَحْزَنْ إِنَّ ٱللَّهَ مَعَنَا ۖ فَأَنزَلَ ٱللَّهُ سَكِينَتَهُۥ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُۥ بِجُنُودٍ لَّمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ ٱلسُّفْلَىٰ ۗ وَكَلِمَةُ ٱللَّهِ هِىَ ٱلْعُلْيَا ۗ وَٱللَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ 40
{40} Yaani, ikiwa hamtamnusuru Mtume wake Muhammad - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, - basi Mwenyezi Mungu hawahitaji, hakuna kitu kinachoweza kumdhuru. Kwa maana kwa hakika, alimnusuru katika uchache zaidi unaowezekana, na udhalilifu zaidi "walipomtoa wale waliokufuru" kutoka Makka walipoazimia kumuua, na wakafanya juhudi katika hilo na wakawania mno kwa hivyo wakamshinikiza mpaka akatoka "akiwa ni wa pili wa wawili." Yaani, yeye na Abu Bakr As-Siddiq, mwenyezi Mungu amwiye radhi; "walipokuwa katika pango." Yaani, walipokimbia kutoka Makka, walikimbilia kwenye pango la Thawr katika upande wa chini wa Makka, na wakakaa ili kuwatuliza watafutaji wao. Walipokuwa katika hali hiyo ngumu na kali, yenye mashaka wakati maadui walipoenea katika kila upande wakiwatafuta ili wawaue, kwa hivyo Mwenyezi Mungu akawateremshia katika nusura yake jambo ambalo haliwezi kufikiriwa. Nabii "alipomwambia sahibu wake" Abu Bakr, alipohuzunika na wasiwasi wake ukawa mkubwa, "usihuzunike. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi" kwa msaada wake, na nusura, na kumuunga kwake mkono. "Basi Mwenyezi Mungu akauteremsha utulivu wake juu yake;" yaani, uthabiti, na kutua, na utulivu unaoimarisha moyo. Na ndiyo maana sahibu wake alipoingiwa na wasiwasi, akamtuliza na akasema: Usihuzunike, hakika mwenyezi Mungu yu pamoja nasi. "Na akamuunga mkono kwa majeshi ambayo hamkuyaona." Nao ni malaika watukufu, ambao Mwenyezi Mungu aliwaweka kuwa walinzi wake. "Na akalifanya neno la wale waliokufuru kuwa chini." Yaani, kuanguka na kuachiliwa mbali, kwa maana wale waliokufuru katika [hakika] walikuwa wameazimia wakiona kwamba wana uwezo, kulingana na dhana yao kwamba wanaweza kumuua Mtume - rehema na amani ziwe juu yake - na kumtia nguvuni kwa sababu ya hasira dhidi yake. Basi wakafanya kila wawezalo kuhusiana na hilo, lakini Mwenyezi Mungu akawaangusha, wala hakuwatimizia makusudio yao, bali hata wala hawakufikia lolote katika hayo. Na Mwenyezi Mungu akamnusuru Mtume wake kwa kumzuilia hilo. Na huku ndiko kunusuru kulikotajwa pahali hapa kwa maana nusura ni aina mbili: Kuwanusuru Waislamu wanapotaka kwamba Mwenyezi Mungu awatimizie kile wanachotaka na kukusudia, na ili wawe na mamlaka juu ya adui yao na kuwashinda. Ya pili ni kumnusuru aliyedhoofishwa, ambaye adui wake anamtakia shari. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu akamnusuru kwa kumuondolea adui yake na kumlinda. Na huenda nusura hii ndio yenye manufaa zaidi kati ya nusura hizi mbili. Na nusura ya Mwenyezi Mungu juu ya Mtume wake pale wale waliokufuru walipomtoa alipokuwa wa pili wa wawili ni katika aina hii. Na kauli yake: "Na Neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu." Yaani, Maneno yake ya kimajaaliwa na Maneno yake ya kidini ndiyo ya juu zaidi kuliko maneno ya wengineo, ambayo miongoni mwake ni kauli yake: "Na ilikuwa ni haki juu yetu kuwanusuru Waumini;" "hakika sisi tunawanusuru Mitume wetu wetu na wale walioamini katika uhai wa dunia hii na siku watakaposimama Mashahidi;" "Na Hakika jeshi letu ndio washindi." Kwa hivyo Dini ya Mwenyezi Mungu ndiyo iliyo ya juu zaidi kuliko dini nyingine zote, kwa hoja zilizo wazi, na aya zenye kung'aa, na mamlaka yenye ushindi. "Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu" hawezi kumshinda mwenye kushinda yeyote, wala hamkimbii mwenye kukimbia. "Mwenye hekima;" anaweka vitu pahali pake, na huchelewesha kulinusuru kundi lake mpaka wakati mwingine unaohitajika kwa hekima ya Mwenyezi Mungu. Na katika aya hii tukufu kuna ubora wa Abu Bakr as-Siddiq kwa sifa ambayo hakuna mtu mwingine yeyote katika umma huu aliyekuwa nayo, ambayo ni kufikia cheo hiki cha heshima na usuhuba mzuri. Na Waislamu wamekubaliana kwa kauli moja kwamba yeye ndiye aliyekusudiwa katika Aya hii tukufu. Na ndiyo maana wanaona kuwa yeyote yule anayekanusha kwamba Abu Bakr hakuandamana pamoja na Nabii – Rehema na Amani zimshukie – ni kafiri. Kwa sababu anaikanusha Qur’an ambayo ililisema hilo wazi wazi. Na ndani yake kuna ubora wa utulivu, na kwamba huo ni katika utimilifu wa neema ya Mwenyezi Mungu juu ya mja nyakati za shida na hofu ambazo nyoyo hupotea kwazo, na kwamba hilo huwa kulingana na elimu ya mja juu ya Mola wake Mlezi, imani yake katika ahadi yake ya kweli, na kulingana na imani yake na ujasiri wake. Na ndani yake kuna kwamba huzuni unaweza kuwapata waja wakweli wateule wa Mwenyezi Mungu, pamoja na kwamba lifaalo zaidi ikiwa huzuni huu unampata mja ajitahidi kujiondolea. Kwa maana huo unadhoofisha moyo na unapunguza azimio.