Az-Zumar
Ini adalah terjemahan Tafsir as-Saʿdī sebagaimana diterbitkan IslamHouse.com di saadi.islamenc.com, dibaca dari halaman-halaman situs itu. Situs itu tidak menyebutkan siapa yang menerjemahkannya maupun edisi cetak mana yang diikutinya, dan tidak menyatakan ketentuan untuk mengambil teksnya, sehingga hak untuk menampilkannya belum diverifikasi. Belum ada yang membandingkannya dengan buku cetak, dan belum ada ulama yang meninjaunya. Setiap bagian berdiri di samping ayat-ayat yang diulasnya, yaitu teks Al-Qur’an dari Tanzil, ditampilkan sebagaimana adanya di sana; ayat yang tidak diberi ulasan tersendiri oleh situs itu berdiri bersama bagian sebelumnya, dan indeks menyebutkan setiap ayat semacam itu. Sabīl tidak menulis atau menerjemahkan satu pun darinya.
Teks darisaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)diambil 2026-10-22
أَلَا لِلَّهِ ٱلدِّينُ ٱلْخَالِصُ ۚ وَٱلَّذِينَ ٱتَّخَذُوا۟ مِن دُونِهِۦٓ أَوْلِيَآءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَآ إِلَى ٱللَّهِ زُلْفَىٰٓ إِنَّ ٱللَّهَ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فِى مَا هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَهْدِى مَنْ هُوَ كَـٰذِبٌ كَفَّارٌ 3
{3} "Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu." Huku ni kuthibitisha amri ya kwamba wanapaswa kumkusudia Mwenyezi Mungu peke yake, na kubainisha kwamba Yeye Mtukufu ndiye mkamilifu zaidi na ana fadhila juu ya waja wake kwa namna zote. Basi ni yake dini iliyo safi na isiyo na uchafu wowote. Kwani ndiyo dini aliyoiridhia mwenyewe na akaridhia kwamba iwe ndiyo dini ya viumbe wake wateule, na akawaamrisha kuifuata. Kwa sababu inajumuisha kumfanyia Mwenyezi Mungu tu uungu katika upendo, hofu, matumaini, kutubia kwake, na kurejea kwake katika kutimiza mahitaji ya waja wake. Na hayo ndiyo yanayorekebisha nyoyo na kuzitakasa, pasi na kumshirikisha na chochote katika ibada. Kwani Mwenyezi Mungu yuko mbali mno na kuwa na mshirika yeyote na wala haitajii hilo. Kwani shirki huharibu nyoyo, roho, dunia na akhera, na huzitia nafsi katika mashaka makubwa mno. Ndiyo maana, alipoamrisha waja kumpwekesha na kumkusudia Yeye peke yake, akakataza kumshirikisha, na akajulisha ubaya wa wale wanaomshirikisha akisema: "Na wale wanaowafanya wenginewe kuwa ni walinzi" kwa kuwaabudu na kuwaomba wakijitafutia udhuru wakisema: "'Sisi hatuwaabudu ila wapate kutujongeza tu kumkaribia Mwenyezi Mungu.'" Yaani, ili watufikishie mahitaji yetu kwa Mwenyezi Mungu na kutuombea kwake. Kwa maana sisi tunajua kwamba hivyo vitu haviumbi, haviruzuku, wala havimiliki chochote katika jambo lolote. Watu hawa waliacha yale aliyowaamrisha Mwenyezi Mungu ya kumkusudia Yeye tu, na wakathubutu kufanya jambo kubwa kabisa lililoharamishwa, ambalo ni shirki. Na wakamfananisha yule ambaye hakuna kitu kama mfano wake, Mfalme mkuu, na wafalme wengineo. Na wakadai - kwa akili zao mbovu na maoni ya magonjwa - kwamba wafalme, jinsi hawawezi kufikiwa isipokuwa kwa kupitia watu wa hadhi mbele yake, waombezi, mawaziri ambao wanaweza kumfikishia mahitaji ya raia zao na kuwatafutia huruma mbele yao; kwamba Mwenyezi Mungu yuko hivyo! Ulinganisho huu ni mojawapo ya milinganisho potovu zaidi. Kwani unajumuisha ulinganisho kati ya Muumba na kiumbe, pamoja na kwamba imeshathibiti kuwepo tofauti kubwa kati ya viwili hivyo kiakili, kimaandiko na hata kimaumbile ya asili. Kwa maana wafalme walihitaji wapatanishi kati yao na raia wao kwa sababu hawajui hali zao, basi ndiyo wakahitaji mtu wa kuwajulisha hali zao. Na pengine huenda wasiwe na huruma katika nyoyo zao kwa mwenye haja huyo, kwa hivyo wakahitaji mtu wa kuwatafutia huruma mbele yao. Na wanahitaji waombezi na wasaidizi. Na wanawahofu, kwa hivyo ndiyo wanakidhi mahitaji ya wale wanaowaombea ili kuwatuliza mawazo yao. Nao pia ni wahitaji, na wanaweza kuzuiwa kwa sababu wanaogopa umasikini. Na Mola Mlezi Mtukufu ndiye ambaye elimu yake imezunguka mambo yote ya dhahiri na ya ndani, ambaye hahitaji mtu yeyote kumjulisha hali za raia wake na waja wake. Yeye ndiye Mwingi wa kurehemu, Mkarimu atoaye kwa wingi zaidi ya wote, hamhitaji yeyote katika viumbe vyake ili amfanye kuwa na huruma kwa waja wake. Bali Yeye ni Mwenye huruma zaidi kwao kuliko wao wenyewe kwa nafsi zao na kuliko wazazi wao wanavyowahurumia. Naye ndiye anayewahimiza na kuwaita kwenye visababu vya kuwafanya kufikia rehema zake, na anawatakia masilahi ambayo hata wao wenyewe hawajitakii. Naye ndiye Mkwasi, Mwenye ukwasi kamili kabisa. Ambaye kama viumbe vyote tangu vya mwanzo hadi vya mwisho vingekusanyika mahali pamoja, vikamwomba, naye akakipa kila kimoja kilichoomba na kutamani, havingepunguza ukwasi wake hata kidogo, isipokuwa namna inavyopunguka bahari wakati sindano inaingizwa na kutolewa ndani yake. Na waombezi wote wanamuogopa. Hawezi yeyote miongoni mwao kufanya uombezi ila kwa idhini yake, kwani uombezi wote ni wake. Basi kupitia tofauti hizi, unajulikana ujinga wa wale wanaomshirikisha na upumbavu wao mkubwa, na ukubwa wa ujasiri wanaofanya dhidi yake. Na inajulikana hekima ya ukweli kwamba Mwenyezi Mungu hausamehi ushirikina kwa sababu unajumuisha kumtia dosari Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na ndiyo maana akasema akihukumu baina ya makundi mawili: wanaomkusudia Yeye peke yake, na wale wanaomshirikisha, maneno ambayo ndani yake kuna tishio kwa washirikina: "Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao katika yale wanayohitalifiana." Na tayari ilishajulikana kwamba Mwenyezi Mungu alishahukumu kuwa Waumini wanaomkusudia Yeye peke yake watakuwa katika Bustani zenye neema. Naye mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu amemharamishia Bustani za mbinguni, na mahala pake ni Motoni. "Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi" kwenye njia iliyonyooka "aliye mwongo, kafiri." Kwa maana anajiwa na mawaidha na ishara mbalimbali lakini haachani na sifa zake hizo. Na Mwenyezi Mungu anamwonyesha ishara mbalimbali lakini anazikanusha, anazikufuru na kuzikadhibisha. Basi huyu atawezaje kupata uwongofu ilhali ameshajifungia mlango na akaadhibiwa kwa Mwenyezi Mungu kuuziza moyo wake? Basi hawezi kuamini.