Langsung ke konten
Tafsir As-Saadi - Swahili · Al-Baqara
Surah 2

Al-Baqara

Ini adalah terjemahan Tafsir as-Saʿdī sebagaimana diterbitkan IslamHouse.com di saadi.islamenc.com, dibaca dari halaman-halaman situs itu. Situs itu tidak menyebutkan siapa yang menerjemahkannya maupun edisi cetak mana yang diikutinya, dan tidak menyatakan ketentuan untuk mengambil teksnya, sehingga hak untuk menampilkannya belum diverifikasi. Belum ada yang membandingkannya dengan buku cetak, dan belum ada ulama yang meninjaunya. Setiap bagian berdiri di samping ayat-ayat yang diulasnya, yaitu teks Al-Qur’an dari Tanzil, ditampilkan sebagaimana adanya di sana; ayat yang tidak diberi ulasan tersendiri oleh situs itu berdiri bersama bagian sebelumnya, dan indeks menyebutkan setiap ayat semacam itu. Sabīl tidak menulis atau menerjemahkan satu pun darinya.

Teks darisaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)diambil 2026-10-22

Ayat 195

وَأَنفِقُوا۟ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ وَلَا تُلْقُوا۟ بِأَيْدِيكُمْ إِلَى ٱلتَّهْلُكَةِ ۛ وَأَحْسِنُوٓا۟ ۛ إِنَّ ٱللَّهَ يُحِبُّ ٱلْمُحْسِنِينَ 195

{195} Mwenyezi Mungu Mtukufu anawaamrisha waja wake watoe katika njia yake. Nako ni kutoa mali katika njia zinazofikisha kwa Mwenyezi Mungu. Nazo ni kila njia ya wema, kama vile kuwapa masikini sadaka, au jamaa, au kupeana matumizi kwa yule ambaye inalazimika kumpa matumizi. Na kubwa zaidi katika hilo, na la kwanza linaloingia katika hilo ni kutoa katika jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kupeana matumizi katika hilo ni kufanya jihadi kwa mali, na ni wajibu kama kufanya jihadi kwa mwili. Na ndani yake kuna manufaa makubwa, kama vile kusaidia kuwaimarisha Waislamu, na kudhoofisha ushirikina na watu wake, na kusimamisha Dini ya Mwenyezi Mungu na kuipa nguvu. Kwa hivyo, jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu haisimami isipokuwa juu ya shina la kutoa (mali). Kwani, kutoa ni kama roho kwake, haiwezekani kuwepo kwake bila ya hiyo (roho). Na katika kuacha kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu ni kubatilisha jihadi, kuwapa nguvu maadui, na kukithirisha mashambulizi yao. Kwa hivyo inakuwa kauli yake Mola Mtukufu, “wala msijitupe katika maangamivu kwa mikono yenu” ni kubainisha sababu ya hilo. Na kujitupa katika maangamivu kwa mkono kunarudi kwa mambo mawili: Mja kuacha yale aliyoamrishwa, ikiwa kuyaacha kunaleta au kunakaribia kuleta maangamivu kwa mwili au roho. Na (pili) kufanya lile ambalo ni sababu inayopelekea kuharibika kwa nafsi au roho. Kwa hivyo, mambo mengi sana yanaingia chini ya hayo .Na katika hayo ni kuacha jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, au kupeana matumizi juu yake ambako kunasababisha kuwapa nguvu maadui. Na katika hayo ni mtu hujidanganya kwenda katika vita au safari yenye kuhofisha, au mahali penye wanyama pori, au nyoka. Au kukwea miti au majengo hatari, au kuingia chini ya kitu ambacho ndani yake kuna hatari, na mfano wa hayo. Basi haya na mfano wake ni miongoni mwa wale waliojitupa katika maangamivu kwa mikono yao. Na katika kujitupa katika maangamivu kwa mkono ni kudumu katika kumuasi Mwenyezi Mungu, na kukata tamaa ya kutubu. Na katika hilo ni kuacha yale aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu ya faradhi, ambayo katika kuyaacha kuna kuangamiza roho na dini. Na kwa kuwa kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu ni aina katika aina za wema, akaamrisha kufanya wema kwa ujumla, akasema: “Na fanyeni wema. Hakika, Mwenyezi Mungu huwapenda wanaofanya wema.” Na hili linajumuisha kila aina ya wema, kwa sababu hakulifanya kuwa mahususi kwa kitu fulani kando na vitu vinginevyo. Kwa hivyo kunaingia humo kufanya wema kwa mali kama ilivyotangulia hapo awali. Na inaingia ndani yake kufanya wema kwa kupitia heshima ya mtu, kwa kufanya uombezi na mfano wa hilo. Na inaingia katika hilo kufanya wema kwa kuamrisha mema na kukataza maovu, na kufundisha elimu yenye manufaa. Na inaingia katika hilo kuwatimizia watu mahitaji yao kama vile kuwaondolea dhiki zao na kuwaondolea ugumu wao, kuwatembelea wagonjwa wao, kuhudhuria mazishi yao, kuwaongoza waliopotea wao, kuwasaidia wanaofanya kazi ambayo hawawezi kuifanya vizuri na mfano wa hayo, ambayo ni katika wema ambao Mwenyezi Mungu aliamrisha. Na inaingia katika wema pia kufanya wema (vizuri) katika kumwabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu. Nalo ni kama ilivyotaja Nabii rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, “Ihsan ni kumuabudu Mwenyezi Mungu kana kwamba unamwona. Na ikiwa humwoni, basi Yeye kwa hakika anakuona.” Basi mwenye kusifika kwa hizi sifa, atakuwa miongoni mwa wale ambao Mwenyezi Mungu alisema kuwahusu, “kwa wale wanaofanya wema ni wema na zaidi.” Na Mwenyezi Mungu atakuwa pamoja naye, akimweka sawasawa, akimuongoa, na kumsaidia katika mambo yake yote.