Al-Kahf
Voici une traduction du tafsîr d’as-Saʿdī, telle qu’IslamHouse.com la publie sur saadi.islamenc.com, lue dans les pages de ce site. Le site ne dit ni qui l’a traduite ni quelle édition imprimée elle suit, et n’indique aucune condition pour en reprendre le texte, si bien que le droit de la montrer n’est pas vérifié. Personne ne l’a comparée à un livre imprimé, et aucun savant ne l’a relue. Chaque passage se tient à côté des versets qu’il commente, qui sont le texte coranique de Tanzil, montré tel qu’il y est ; un verset auquel le site ne donne aucun commentaire propre se tient avec le passage qui le précède, et l’index nomme chacun de ces versets. Sabīl n’en a rien écrit ni traduit.
Texte desaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)pris le 2026-10-22
وَقُلِ ٱلْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ ۖ فَمَن شَآءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَآءَ فَلْيَكْفُرْ ۚ إِنَّآ أَعْتَدْنَا لِلظَّـٰلِمِينَ نَارًا أَحَاطَ بِهِمْ سُرَادِقُهَا ۚ وَإِن يَسْتَغِيثُوا۟ يُغَاثُوا۟ بِمَآءٍ كَٱلْمُهْلِ يَشْوِى ٱلْوُجُوهَ ۚ بِئْسَ ٱلشَّرَابُ وَسَآءَتْ مُرْتَفَقًا 29
{29} Yaani, "Sema" uwaambie watu, ewe Muhammad, "Hii ni haki itokayo kwa Mola wenu Mlezi." Yaani, tayari uwongofu umeshabainika kutokana na upotovu, na usawa kutokana na ukengeufu, na sifa za watu wa furaha na sifa za watu wa mashaka, na hayo ni kupitia yale ambayo Mwenyezi Mungu aliyabainisha juu ya ulimi wa mtume wake. Na ikishabainika na ikawa wazi, na isibakie na shaka yoyote, "Basi anayetaka, na aamini, na anayetaka, na akufuru." Yaani, haikubakia isipokuwa kufuata moja kati ya njia mbili hizo kulingana na mja kuwezeshwa au kutowezeshwa. Na Mwenyezi Mungu alimpa utashi ambao kwa huo anaweza kuamini na kukufuru, na kufanya heri na maovu. Kwa hivyo, mwenye kuamini, basi atakuwa amewezeshwa kufikia usahihi. Na mwenye kukufuru, basi tayari imekwisha msimamia hoja, wala hawezi kulazimishwa kuamini, kama Mwenyezi Mungu Mtukufu alivyosema, "Hapana kulazimisha kokote katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka kutokana na upotovu." [Na hakuna katika kauli yake, "Basi anayetaka, na aamini, na anayetaka," idhini yoyote ya kufanya mawili hayo. Lakini hilo ni tishio na onyo kali kwa anayechagua ukafiri baada ya ubainisho kamili, kama vile hakuna katika hilo kuacha kwake kupigana na makafiri]. Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu akataja mwisho wa makundi hayo mawili, akasema, “Hakika Sisi tumewaandalia wenye kudhulumu” kwa kukufuru, kuvuka mipaka, na kuasi. “Moto ambao utawazunguka kama hema” na hawana sehemu ya kutokea wala njia, wala kuokoka na hayo. Watachomwa na moto mkali. "Na wakiomba msaada;" yaani, wanapoomba kinywaji ili kutuliza kiu kikali kilichowapata, "watasaidiwa kwa kupewa maji kama mafuta yaliyotibuka." Kwa sababu ya joto lake kali, "yatakayowabambua nyuso zao." Basi yatakuwa vipi matumbo na tumbo zao? Kama alivyosema Mwenyezi Mungu, "Kwa maji hayo vitayeyushwa vilivyomo matumboni mwao, na ngozi zao pia. Na wana marungu ya chuma." "Ni kinywaji kiovu mno kilioje hicho" ambacho kinakusudiwa kuzima kiu na kuwaepusha baadhi ya adhabu hiyo! Basi itakuwa ni ongezeko la adhabu yao na ukali wa adhabu yao. "Na matandiko mabaya mno ya kupumzikia yaliyoje hayo!" Na huku ni kushutumu hali ya Moto huo. Kwamba ndipo mahali pabaya zaidi pa kupumzikia. Kwa maana, hapo hakuna kupumzika kokote, bali humo kuna adhabu kubwa na ngumu hawapumzishwi kutokana nayo hata kwa saa moja, nao humo watakata tamaa ya heri yoyote, na Mwingi wa rehema atawasahau katika adhabu hiyo kama walivyomsahau.