Ash-Shu'araa
این ترجمهٔ تفسیر سعدی است، همانگونه که IslamHouse.com آن را در saadi.islamenc.com منتشر میکند و از صفحههای آن سایت گرفته شده است. سایت نمیگوید چه کسی آن را ترجمه کرده و از کدام چاپ پیروی میکند، و برای برداشتن متن آن شرطی بیان نمیکند، پس حق نمایش آن تأیید نشده است. کسی آن را با کتاب چاپی مقایسه نکرده و عالمی آن را بررسی نکرده است. هر بخش در کنار آیههایی آمده که دربارهٔ آنها توضیح میدهد و این آیهها متن قرآن از Tanzil است، همانگونه که آنجا هست؛ آیهای که سایت توضیح جداگانهای برایش نمیدهد با بخش پیش از خود میآید، و فهرست هر چنین آیهای را نام میبرد. سبیل چیزی از آن را ننوشته و ترجمه نکرده است.
متن ازsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)برداشتهشده در 2026-10-22
وَٱلشُّعَرَآءُ يَتَّبِعُهُمُ ٱلْغَاوُۥنَ ۲۲۴ أَلَمْ تَرَ أَنَّهُمْ فِى كُلِّ وَادٍ يَهِيمُونَ ۲۲۵ وَأَنَّهُمْ يَقُولُونَ مَا لَا يَفْعَلُونَ ۲۲۶
{224 - 226} Na alipomtakasa mbali na suala la kuteremkiwa na mashetani, akamuweka mbali na mambo ya ushairi. Akasema, "Na watungaji mashairi." Yaani, je, niwaambieni pia juu ya hali yao na sifa zao madhubuti? Wao hakika, "ni wapotofu ndio wanawafuata," kwa kufuata njia ya upotofu ambayo ni mbaya. Kwa hivyo, wao wenyewe wamepotoka, na wafuasi wao ni kila aliyepotea aliyeharibika. "Je, huwaoni" kwa sababu ya ukubwa wa upotofu wao "kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde," miongoni mwa mabonde yenye mashairi? Mara wanasifu, na mara wanashutumu, na mara wanasema ukweli, na mara wanadanganya, mara wanasema mashairi ya mapenzi, na mara wanadhihaki, mara wanafurahia na mara wanahuzunika; kwa hivyo hawatulii kwa kitu kimoja wala hali moja. "Na kwamba wao husema wasiyoyatenda?" Yaani, hii ndiyo sifa ya ushairi, kwamba kauli zao zinahalifu matendo yao. Na ukimsikia mshairi anasema mashairi laini ya mapenzi, utasema: Huyu ndiye ndiye mwenye mapenzi zaidi ya watu wote, ilhali moyo wake hauna kitu katika hilo. Na ukimsikia akisifu au akikashifu, utasema: Huu ni ukweli, ilhali ni uongo. Na mara anasifu kwa matendo ambayo hakufanya, na kwa mambo ya kuwachwa ambayo hakuacha, kwa ukarimu ambao hata hajawahi kukaribia uwanja wake, na kwa ujasiri ambao anainua anawashinda mashujaa wapanda farasi, na ilhali utamwona yeye ndiye mwoga zaidi kuliko waoga wote. Basi hii ndiyo sifa yao. Kwa hivyo, angalia; je inaingiana hali yao hii na hali ya Mtume Muhammad - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - mwongofu, mwema, ambaye anafuatwa na kila mtu mwongofu, ambaye amenyooka juu ya uwongofu na akajiepusha na maovu, na wala matendo yake hayakupingana, [na maneno yake hayakupingana na matendo yake]; ambaye haamrishi isipokuwa heri, na hakatazi isipokuwa maovu tu, wala hasemi chochote ila ni mkweli tu, wala hakuamrisha kitu isipokuwa anakuwa yeye ndiye wa kwanza kukifanya, wala hakukataza kitu isipokuwa alikuwa wa kwanza kukiacha. Basi je, hali yake inafailiana na hali ya wanamashairi au hata kuwakaribia? Au ni kinyume chake katika mambo yote? Basi rehema za Mwenyezi Mungu na salamu zake ziwe juu ya Mtume huyu aliyekamilika kabisa, na kiongozi bora zaidi, milele na milele, na zama baada ya zama, ambaye si mshairi, wala mchawi, wala mwendawazimu, wala haimfailii isipokuwa kila ukamilifu.