پرش به محتوا
Tafsir As-Saadi - Swahili · Al-Baqara
سورهٔ ۲

Al-Baqara

این ترجمهٔ تفسیر سعدی است، همان‌گونه که IslamHouse.com آن را در saadi.islamenc.com منتشر می‌کند و از صفحه‌های آن سایت گرفته شده است. سایت نمی‌گوید چه کسی آن را ترجمه کرده و از کدام چاپ پیروی می‌کند، و برای برداشتن متن آن شرطی بیان نمی‌کند، پس حق نمایش آن تأیید نشده است. کسی آن را با کتاب چاپی مقایسه نکرده و عالمی آن را بررسی نکرده است. هر بخش در کنار آیه‌هایی آمده که دربارهٔ آن‌ها توضیح می‌دهد و این آیه‌ها متن قرآن از Tanzil است، همان‌گونه که آنجا هست؛ آیه‌ای که سایت توضیح جداگانه‌ای برایش نمی‌دهد با بخش پیش از خود می‌آید، و فهرست هر چنین آیه‌ای را نام می‌برد. سبیل چیزی از آن را ننوشته و ترجمه نکرده است.

متن ازsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)برداشته‌شده در 2026-10-22

آیهٔ ۱۵۰

وَمِنْ حَيْثُ خَرَجْتَ فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ ٱلْمَسْجِدِ ٱلْحَرَامِ ۚ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّوا۟ وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُۥ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَيْكُمْ حُجَّةٌ إِلَّا ٱلَّذِينَ ظَلَمُوا۟ مِنْهُمْ فَلَا تَخْشَوْهُمْ وَٱخْشَوْنِى وَلِأُتِمَّ نِعْمَتِى عَلَيْكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ ۱۵۰

(150) “Na popote mlipo, zielekezeni nyuso zenu upande wake.” Na akasema: “Na hiyo ndiyo haki itokayo kwa Mola wako Mlezi.” Alisisitiza (hilo) kwa "anna" (hakika)’ na "Laam" (hakika)’ ili isije ikaingia fikira potofu hata kidogo kwa yeyote katika hilo. Na ili isije ikadhaniwa kuwa ni kwa njia ya mwenye kutaka (tu ndiyo afanye), na sio kwa njia ya kutekeleza (amri). “Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayoyatenda.” Bali Yeye anawaona katika hali zenu zote. Basi kueni na adabu mbele yake, na mchungeni kwa kutekeleza maamrisho Yake na kuacha makatazo Yake. Kwani, matendo yenu hayakughafilikiwa, bali mtalipwa juu yake malipo kamilifu. Ikiwa ni ya heri, basi kwa heri. Na ikiwa ni ya shari, basi kwa shari. Na hapa alisema, “ili watu wasiwe na hoja juu yenu”. Yani tuliwawekea sheria ya kuielekea Al-Ka'aba tukufu, ili hoja za watu wa Kitabu na washirikina zisisimame juu yenu. Kwa sababu, angebakia (Mtume) akielekea Baitul-Maqdis, basi hoja ingemwelekea. Kwa sababu, watu wa Kitabu wanapata katika kitabu chao kwamba kibla chake (Mtume) kilicho imara ni Al-Ka'aba, Nyumba tukufu. Nao washirikina wanaona kwamba katika yale wanayojifakhirisha nayo ni Nyumba hii tukufu. Na kwamba ni katika mila ya Ibrahim, na kwamba ikiwa Muhammad – rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake – hataielekea, basi hoja zao zitamwelekea, na waseme: Vipi anadai kuwa yeye yuko katika mila ya Ibrahim, naye ni katika kizazi chake, na ameacha kukielekea kibla chake? Kwa hivyo, kwa kukielekea kibla, hoja ikasimama juu ya watu wa Kitabu na washirikina, na hoja zao zikakatika juu yake; isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao. Yani yule miongoni mwao aliyetumia hoja ambayo yeye ni dhalimu ndani yake, na wala haina msingi wowote isipokuwa kufuata matamanio na dhuluma. Basi, huyo hakuna njia ya kumshawishi na kuweka hoja dhidi yake. Na vile vile hakuna maana ya kuzifanya fikira potofu wanazozitaja kwa njia ya kuweka hoja kuwa ni mahali pa kuzingatia, wala kuzijali. Ndio maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: “Basi msiwaogope wao”. Kwa sababu, hoja yao ni batili. Na batili (uwongo) kama jina lake, inaachwa, na mwenyewe pia huachwa. Hili ni tofauti na mwenye haki, kwani haki ina nguvu na heshima inayomlazimu yule aliye pamoja nayo kunyenyekea. Ambako ndiko kichwa cha kila heri. Hivyo basi, asiyemnyenyekea Mwenyezi Mungu, hawezi kuacha kumuasi, na hawezi kufanya amri yake. Na kulikuwa kuwaelekeza Waislamu kwenye Al-Ka'aba miongoni mwa yale ambayo fitina kubwa ilitokea. Ambayo ilienezwa na watu wa Kitabu, wanafiki, na washirikina, na wakazidisha mazungumzo na fikira potofu katika hilo. Na ndiyo maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akalipanua na akalifafanua ufafanuzi kamili kabisa. Na akalisisitiza kwa aina mbalimbali za kusisitiza ambazo Aya hizi zinajumuisha. Miongoni mwake ikiwa kuamrisha hilo mara tatu, licha ya kwamba mara moja tu ingetosha. Miongoni mwake ni kwamba inajulikana kuwa amri ima ni kwa Mtume, kisha umma uingie humo [kwa kumfuata yeye]. Au iwe kwa umma kwa ujumla. Na katika Aya hii, Mtume aliamrishwa yeye hasa katika kauli yake. "Uelekeze uso wako,” nao umma kwa ujumla katika kauli yake; “zielekezeni nyuso zenu”. Na miongoni mwake ni kwamba alijibu katika Aya hii hoja zote batili ambazo wakaidi walizileta, na akazibatilisha fikira potofu baada ya fikira potofu kama ilivyoelezwa hapo mwanzo. Na miongoni mwake ni kwamba alikata matumaini yao juu ya Mtume kukifuata kibla cha Watu wa Kitabu. Na miongoni mwake ni kauli yake: “Na hiyo kwa hakika ndiyo haki itokayo kwa Mola wako Mlezi.” Basi kwa kusema tu kwa aliye Mkweli Mkuu, hilo linatosha na linaponya. Lakini pamoja na haya, akasema, “na hiyo kwa hakika ndiyo haki itokayo kwa Mola wako Mlezi.” Na miongoni mwake ni kwamba alijulisha, na hali Yeye ndiye mwenye elimu ya siri zote kwamba Watu wa Kitabu walikwisha jua usahihi wa jambo hili, lakini wao wanauficha ushuhuda huu kwa kujua. Na pindi kulipokuwa kutugeuza kwake kuelekea kibla ni neema kubwa, na ukawa upole wake kwa umma huu na rehema yake haujaacha kuendelea kuongezeka. Na kila anapowawekea sheria, inakuwa neema ni kubwa. Akasema, “ili niwatimizie neema yangu.” Na asili ya neema ni uwongofu kwa dini yake kwa kumtuma Mtume wake na kuteremsha Kitabu chake. Kisha baada ya hayo, neema zinazokamilisha asili hii, ambazo hazihesabiki kwa sababu ya wingi wake. Na wala haziwekewi mipaka tangu Mwenyezi Mungu alipomtuma Mtume wake mpaka ilipokaribia kuondoka kwake duniani, na tayari Mwenyezi Mungu alikuwa ameshampa katika hali mbalimbali na neema. Na akawapa umma wake aliokamilisha kwacho neema yake juu yake na juu yao, na Mwenyezi Mungu akamteremshia,. “Leo nimewakamilishia Dini yenu, na nimewatimizia neema yangu, na nimewapendelea Uislamu uwe ndiyo Dini.” Basi sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu kwa fadhila zake, ambazo hatuzifikii kwa kuzihesabu, mbali na kuzishukuru; “ili mpate kuongoka.” Yani mnajua haki na mnaifanyia kazi. Kwani, Mwenyezi Mungu, mwingi wa baraka, Mtukufu kutokana na rehema zake kwa waja; amewafanyia wepesi sana sababu za uwongofu. Na amewatanabahisha wafuate njia zake, na akawafafanulia (hizo njia) kwa ukamilifu kabisa, kiasi kwamba miongoni mwa hayo ni kwamba anaiwekea haki wale wanaoipinga. Basi wakaijadili, kwa hivyo haki ikabainika kwa hilo, na Aya zake na ishara zake zikaonekana. Na ukabainika ubatili wa batili, na kwamba haina uhakika, na lau kuwa si kusimama kwake mbale ya haki, pengine hali yake isingebainika kwa viumbe wengi. Na kwa kinyume cha kitu, kitu hicho hubainika. Na lau kuwa siyo usiku, basi fadhila ya mchana isingejulikana. Na lau kuwa sio ubaya, basi fadhila ya wema isingejulikana. Na lau kuwa sio giza, basi faida ya nuru isingejulikana. Na lau kuwa sio batili (uwongo), basi haki isingebainika kubainika kuliko dhahiri. Basi, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu kwa hilo.