Al-Baqara
این ترجمهٔ تفسیر سعدی است، همانگونه که IslamHouse.com آن را در saadi.islamenc.com منتشر میکند و از صفحههای آن سایت گرفته شده است. سایت نمیگوید چه کسی آن را ترجمه کرده و از کدام چاپ پیروی میکند، و برای برداشتن متن آن شرطی بیان نمیکند، پس حق نمایش آن تأیید نشده است. کسی آن را با کتاب چاپی مقایسه نکرده و عالمی آن را بررسی نکرده است. هر بخش در کنار آیههایی آمده که دربارهٔ آنها توضیح میدهد و این آیهها متن قرآن از Tanzil است، همانگونه که آنجا هست؛ آیهای که سایت توضیح جداگانهای برایش نمیدهد با بخش پیش از خود میآید، و فهرست هر چنین آیهای را نام میبرد. سبیل چیزی از آن را ننوشته و ترجمه نکرده است.
متن ازsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)برداشتهشده در 2026-10-22
سَيَقُولُ ٱلسُّفَهَآءُ مِنَ ٱلنَّاسِ مَا وَلَّىٰهُمْ عَن قِبْلَتِهِمُ ٱلَّتِى كَانُوا۟ عَلَيْهَا ۚ قُل لِّلَّهِ ٱلْمَشْرِقُ وَٱلْمَغْرِبُ ۚ يَهْدِى مَن يَشَآءُ إِلَىٰ صِرَٰطٍ مُّسْتَقِيمٍ ۱۴۲
Aya ya kwanza inajumuisha muujiza, na kufariji, na kutuliza nyoyo za Waumini. Na (pia ina) pingamizi na jawabu lake kwa namna tatu, na sifa za mwenye kupinga, na sifa za anayeisalimisha dini yake kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu. Basi, Mwenyezi Mungu Mtukufu akajulisha kuwa wajinga miongoni mwa watu watapinga. Nao ni wale wasioyajua masilahi ya nafsi zao. Bali wanayapoteza na wanayauza kwa thamani ya chini kabisa. Nao ni Mayahudi na Manasara na wale wanaofanana nao miongoni mwa wanaopinga hukumu za Mwenyezi Mungu na sheria zake. Na hilo ni kwa sababu Waislamu walikuwa wameamrishwa kuielekea Baitul-Maqdis (katika) muda waliokuwa wamekaa huko Makka. Kisha baada ya kuhamia Madina - takriban mwaka mmoja na nusu - kwa sababu ya hekima za Mwenyezi Mungu katika hilo, ambazo ataashiria baadhi yake, na hekima yake ilikuwa inalazimu kuwaamrisha kuielekee Al-Kaaba. Kwa hivyo, akawajulisha kuwa hakuna budi kwamba wapumbavu katika watu watasema, "Nini kilichowageuza kutoka kibla chao walichokuwa wakikielekea?" Nako ni kuelekea Baitul-Maqdis. Yani ni kitu gani kilichowageuza kutoielekea? Na katika hilo, kuna upingamizi dhidi ya hukumu ya Mwenyezi Mungu na sheria yake, na fadhila yake na wema wake. Kwa hivyo, akawafariji, na akajulisha kutokea kwake. Na kwamba hilo linatokea tu kutoka kwa anayesifika kwa upumbavu, mchache wa akili, kutofahamu na dini. Basi msiwajali, kwa sababu chanzo cha hayo maneno tayari kilikwishajulikana. Kwa maana, mwenye akili timamu hajali pingamizi la mpumbavu, na wala hana wasiwasi nalo. Na Aya hii ilionyesha kuwa hazipingi hukumu za Mwenyezi Mungu isipokuwa mpumbavu, mjinga, na mkaidi. Ama Muumini mwenye busara na akili timamu, yeye huzipokea hukumu za Mola wake Mlezi kwa kuzikubali, kuzifuata, na kusalimu amri, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na hiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri katika jambo lao.” “Hapana! Ninaapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayohitalifiana” hadi mwisho wa Aya. “Haiwi kauli ya Waumini wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, isipokuwa ni kusema: Tumesikia, na tumetii!” Na kulikuwa katika kauli yake “wapumbavu” kinachotosheleza kuijibu kauli yao, na kutoijali. Hata hivyo, Yeye Mtukufu pamoja na hili, hakuiacha dhana hii potofu mpaka alipoiondoa na kuiweka wazi kwa sababu ya ule upinzani ambao huenda ukaingia katika baadhi ya nyoyo. Kwa hivyo, Yeye Mtukufu akasema, “Sema” ukiwajibu. “Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu. Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyonyooka.” Yani ikiwa Mashariki na Magharibi ni miliki ya Mwenyezi Mungu, na wala hakuna upande wowote katika pande zote unaotoka nje ya miliki yake .Na pamoja na hilo, Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyonyooka. Na katika hilo ni kuwaongoa nyinyi kwenye Kibla hiki ambacho ni katika mila ya baba yenu Ibrahim. Basi ni kwa kitu gani mpingani anafanya upinzani kwa sababu ya kuwaelekeza nyinyi kwenye Kibla kilichomo ndani ya miliki ya Mwenyezi Mungu? Nyinyi hamkuelekea upande usiokuwa miliki yake? Na hili, linalazimu kusalimu amri yake kwa hilo tu? Basi, itakuwa vipi ilhali katika fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu, na kuongoa kwake na wema wake ni kwamba aliwaongoa kwa hilo. Kwa hivyo, mwenye kuwapinga (katika hilo), basi anapinga fadhila za Mwenyezi Mungu kwa kuwahusudu na dhuluma. Na ilipokuwa kauli yake, “humwongoa amtakaye kwenye njia iliyonyooka.” Ni ya jumla (Al-Mutlaq), na cha jumla kinapaswa kueleweka kwa mujibu wa kile ambacho ni mahususi (Al-Muqayyad), basi uongofu na upotovu vina sababu ambazo ziliwekwa kwa hekima na uadilifu wa Mwenyezi Mungu. Na (Mwenyezi Mungu) ameeleza katika sehemu zaidi ya moja katika Kitabu chake sababu za uwongofu. Ambazo mja akizitekeleza, basi atapata uwongofu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu. “Mwenyezi Mungu huwaongoa kwacho wenye kufuata radhi yake katika njia za salama.” Katika Aya hii, (Mwenyezi Mungu) alitaja sababu za jumla ambazo zinauletea umma huu uwongofu katika aina zote za uwongofu. Na pia wema wa Mwenyezi Mungu juu yake. Akasema: