Al-Anbiyaa
This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.
Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22
بَلْ قَالُوٓا۟ أَضْغَـٰثُ أَحْلَـٰمٍۭ بَلِ ٱفْتَرَىٰهُ بَلْ هُوَ شَاعِرٌ فَلْيَأْتِنَا بِـَٔايَةٍ كَمَآ أُرْسِلَ ٱلْأَوَّلُونَ 5
{5} Yeye Mtukufu anataja muungano wa wale waliomkadhibisha Muhammad - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - na yale aliyokuja nayo katika Qur-ani Tukufu, na kwamba wao walizua uongo kuhusiana naye, na wakasema kauli batili mbalimbali kuhusiana naye. Wakati mwingine walisema: Ni ndoto za ovyo ovyo sawa na maneno ya aliyelala usingizi anayeropokwa, ambaye hahisi anachokisema! Na mara wakasema: Aliizua, akaitunga na akaisema tu yeye mwenyewe! Na mara wakasema kwamba yeye ni mshairi na kwamba yale aliyokuja nayo ni mashairi tu! Lakini kila mtu ambaye ana elimu hata kidogo zaidi kuhusu hali halisi ya Mtume, na akayaangalia haya aliyokuja nayo, atakuwa na uhakika usiokubali shaka yoyote kwamba ni maneno matukufu zaidi na ya juu zaidi, na kwamba ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na kwamba hakuna yeyote miongoni mwa wanadamu anaweza kuleta mfano wa baadhi yake. Kama Mwenyezi Mungu alivyowapa changamoto maadui zake katika ili waipinge pamoja na kuwepo kwa sababu za kuipinga na kuifanyia uadui. Lakini hawakuweza kuipinga kwa chochote, nao wanalijua hilo. Vinginevyo, basi ni nini kilichowasimamisha na kuwakalisha na kuwalemeza maungo yao na kugongana kwa ndimi zao, isipokuwa haki ambayo hakuna chochote kinachoweza kusimama mbele yake. Lakini wao huyasema maneno haya kuhusiana naye pasi na kuyaamini, ili kuwaepusha watu wasiomjua mbali naye. Na hili ni katika ishara kubwa zaidi zinazoendelea zinazoonyesha usahihi wa yale aliyokuja nayo Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - na ukweli wake. Nayo yanatosheleza, na yanapoza. Kwa hivyo, kutafuta ushahidi usiokuwa huu au akapendekeza ishara miongoni mwa ishara, basi yeye ni mjinga, dhalimu, na ni mwenye kufananishwa na hawa wakaidi ambao walimkadhibisha (mtume), na wakataka ishara wanazopendekeza wao ambazo ndizo kitu chenye madhara zaidi kwao, na wala hawana masilahi yoyote ndani yake. Kwa sababu ikiwa nia yao ni kujua haki ushahidi wake unapobainika, basi tayari ushahidi wake umeshabainika bila ya hizo (ishara walizozipendekeza). Na ikiwa nia yao ni kumfanya Mwenyezi Mungu kushindwa, na kujiwekea udhuru ikiwa hatawaletea kile walichoomba, basi wao katika hali hii ikiwa itachukuliwa kwamba atawaletea kile walichoomba miongoni mwa ishara, bila shaka hawataamini. Na hata kama ishara zote zitawajia, hawataamini mpaka waione adhabu chungu. Na ndiyo maana Mwenyezi Mungu akasema juu yao, "Basi atuletee miujiza kama walivyotumwa wale wa mwanzo." Yaani, kama vile ngamia wa Swaleh na fimbo ya Musa na mfano wa hayo.