Skip to content
Tafsir As-Saadi - Swahili · Al-Baqara
Sūrah 2

Al-Baqara

This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.

Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22

Verse 220

فِى ٱلدُّنْيَا وَٱلْـَٔاخِرَةِ ۗ وَيَسْـَٔلُونَكَ عَنِ ٱلْيَتَـٰمَىٰ ۖ قُلْ إِصْلَاحٌ لَّهُمْ خَيْرٌ ۖ وَإِن تُخَالِطُوهُمْ فَإِخْوَٰنُكُمْ ۚ وَٱللَّهُ يَعْلَمُ ٱلْمُفْسِدَ مِنَ ٱلْمُصْلِحِ ۚ وَلَوْ شَآءَ ٱللَّهُ لَأَعْنَتَكُمْ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ 220

{220} Ilipoteremka kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Hakika, wale wanaokula 0700205910mali za mayatima kwa dhulu, bila shaka wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni.” Hayo yaliwawia magumu Waislamu, basi wakakitenga na chakula chao kando na chakula cha mayatima wakiziogopea nafsi zao kwamba wasije wakazila; hata katika hali hii ambayo ni desturi kushirikiana ndani yake. Kwa hivyo, wakamuliza Nabii rehema na amani za Mwenyezi Mungu kuhusu hilo. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu akawaambia kwamba kinachokusudiwa ni kutengeneza mali za mayatima kwa kuzihifadhi na kuzitunza, na kuzifanyia biashara. Na kwamba kuchanganyika kwao nao katika chakula au vitu vinginevyo kunaruhusika kwa namna ambayo haiwadhuru mayatima. Kwa sababu wao ni ndugu yenu, na katika mambo ya ndugu ni kuchanganyika na nduguye. Na marejeo katika hayo ni nia na matendo. Kwa hivyo, yule ambaye Mwenyezi Mungu anajua nia yake kuwa yeye ni mtengenezaji wa yatima, wala hana tamaa na mali yake. Basi kama kitu kitamuingia bila ya kukusudia, basi hakutakuwa na ubaya juu yake. Naye yule ambaye Mwenyezi Mungu anajua katika nia yake kwamba makusudio yake katika kuchanganya ni kuzila na kuzitumia, basi huyo ndiye aliyefanya ubaya na akapata dhambi. Na njia zina hukumu sawa na makusudio yake. Na katika Aya hii, kuna ushahidi wa kuruhusiwa kwa kila aina ya kuchanganyika, katika vyakula na vinywaji na mikataba na kadhalika. Na ruhusa hii ni upole kutoka kwa Mwenyezi Mungu [Mtukufu] na hisani, na kuwakunjulia Waumini. Na sivyo basi, “na Mwenyezi Mungu angelipenda, angeliwatia katika udhia.” Yani angewafanyia ugumu kwa kutoruhusu hilo, hivyo basi ukawa ubaya juu yenu, na akawafanyia kuwa ugumu na mkapata dhambi. “Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu.” Yani ana uwezo kamili, na kushinda kila kitu, lakini yeye pamoja na hayo, “ni Mwenye hekima”. Hafanyi isipokuwa kile kinachotakiwa na hekima yake kamilifu, na uangalizi wake timilifu. Kwa hivyo, nguvu zake hazipingani na hekima yake. Hivyo basi, haisemwi kwamba: Yeye atakalo, hulifanya, sawa linakubaliana na hekima yake au linapingana nayo. Bali inasemwa kwamba: Matendo yake na vile vile hukumu zake zinafuata hekima yake. Kwa hivyo, haumbi kitu bure tu. Lakini ni lazima kina hekima, tuijue au tusiijue. Kadhalika, hakuwawekea waja wake sheria yoyote isiyokuwa na hekima. Kwa hivyo, haamrishi chochote isipokuwa chenye masilahi tupu, au hayo ndiyo mengi zaidi. Na wala hakatazi isipokuwa chenye uharibifu mtupu, au huo ndio mwingi zaidi, kwa sababu ya ukamilifu wa hekima yake na rehema yake.