الحديد
هذه ترجمة لتفسير السعدي كما ينشرها IslamHouse.com في saadi.islamenc.com، مقروءةً من صفحات ذلك الموقع. لا يذكر الموقع من ترجمها ولا أي طبعة مطبوعة تتبعها، ولا يذكر شروطًا لأخذ نصّها، ولذلك لم يُتحقق من حق عرضها. لم يقارنها أحد بكتاب مطبوع، ولم يراجعها أحد من العلماء. يقف كل مقطع بجانب الآيات التي يعلّق عليها، وهي نص القرآن من Tanzil كما هو عنده؛ والآية التي لا يعطيها الموقع شرحًا خاصًّا بها تقف مع المقطع الذي قبلها، ويسمّي الفهرس كل آية من هذا النوع. لم يكتب سبيل شيئًا منها ولم يترجمه.
النص منsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)أُخذ في 2026-10-22
يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ ٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ وَءَامِنُوا۟ بِرَسُولِهِۦ يُؤْتِكُمْ كِفْلَيْنِ مِن رَّحْمَتِهِۦ وَيَجْعَل لَّكُمْ نُورًا تَمْشُونَ بِهِۦ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۚ وَٱللَّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ٢٨
{28} Maneno haya inawezekana kuwa wanaambiwa Watu wa Kitabu waliomuamini Musa na Isa, amani iwe juu yao. Anawaamuru kutenda kulingana matakwa ya imani yao. Kwamba wamche Mwenyezi Mungu na waache kumuasi na wamuamini Mtume Wake Muhammad – rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie – na kwamba wakifanya hivyo, Mwenyezi Mungu atawapa “sehemu mbili katika rehema yake.” Yaani, mafungu mawili ya malipo. Fungu moja kwa sababu ya kumuamini kwao kwa Manabii wa zamani, na fungu lingine kwa sababu ya kumuamini kwao Muhammad - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Na pia inawezekana kwamba hii ni amri ya jumla, ambayo wanaingia ndani yake Watu wa Kitabu na wengineo, na hili ndiyo maana iliyo dhahiri (sahihi), na kwamba Mwenyezi Mungu aliwaamrisha kuwa na imani na ucha Mungu, jambo ambalo linajumuisha dini yote, ya dhahiri yake na ya ndani yake, misingi yake na matawi yake, na kwamba ikiwa watatekeleza amri hii kubwa, [Mwenyezi Mungu] atawapa "sehemu mbili katika rehema yake" ambazo hakuna anayejua kiasi chake wala maelezo yake isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Malipo hayo ni kwa sababu ya imani yao na malipo mengine kwa sababu ya uchamungu wao. Au malipo kwa sababu ya kutii amri na malipo mengine kwa sababu ya kuepuka makatazo. Au uwili uliotajwa hapa unakusudiwa kwamba watapewa kwa kurudia mara baada ya nyingine. "Na atakufanyieni nuru ya kwenda nayo." Yaani, atakupeni elimu, uwongofu na nuru mtakayotembea kwayo katika viza vya ujinga, na atakusameheni mabaya yenu. "Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa." Si ajabu kuwa malipo haya ni mengi kama yanatolewa katika fadhila za Mwenye fadhila kubwa, ambaye fadhila zake zimeenea wakazi wa mbinguni na ardhini. Hakuna hata kiumbe mmoja asiye na fadhila zake hata kwa kiasi cha kupepesa jicho, wala kidogo zaidi ya hivyo.